THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Tanzania
haiwezi kuendelea kwa mijadala isiyoisha na vikao vya kulipana posho bali kwa
viongozi kufanya maamuzi na kuyatekeleza haraka.
Aidha, Rais Kikwete
amesema kuwa Tanzania inachelewa kupata maendeleo ya haraka kwa sababu kila mtu
anayepewa kazi anataka kwanza kujadili badala ya kuchukua maamuzi na
kuyatekeleza.
Rais Kikwete ametoa
tahadhari hiyo ya kuchelewesha maendeleo wakati alipozindua Kambi ya Vijana ya
Kilimo na Maarifa ya Mkongo, Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani kwenye siku yake
ya tatu ya ziara ya kikazi katika Mkoa huo leo, Jumamosi, Oktoba 5, 2013.
Akizungumza na wananchi
kabla ya kuzindua kambi hiyo na kukagua shughuli zinazofanywa na vijana 50
kutoka vijiji vya Wilaya ya Rufiji ambao wanajifunza mbinu na maarifa ya kilimo
bora katika kambi hiyo, alitaka kujua kama makampuni mawili yaliyoomba ardhi ya
kulima kisasa katika bonde la Mto Rufiji, yamepewa ardhi ya kuanza
kulima.
Awali katika maelezo
yaliyosomwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Bonde la Rufiji
(RUBADA), Bwana Aloyce Masanja yaliashiria kuonyesha kuwa makampuni hayo,
Frontline Development Partners na Lukurilo Holdings Company Limited yalikuwa
yamepewa ardhi na Mamlaka hiyo kama yalivyokuwa yameomba.
Lakini Rais Kikwete
alipotaka maelezo ya ziara kutaka ukweli kama makampuni hayo yamepewa ardhi na
ni kiasi gani, Bwana Masanja alithibitisha kuwa Frontline Development Partners
walioomba hekta 20,000 walikuwa hawajapewa hata hekta moja na kuwa Lukurilo
Holdings walioomba hekta 12,000 walikuwa wamepewa 4,000 tu.
Rais Kikwete
alishangazwa na hali hiyo na kusema: “Kwa miaka minne sasa tumekuwa tunazungumza
jambo hili bila kufikia uamuzi wake. Tumewahi kujadili suala hili pale Ikulu,
Dar Es Salaam, na kukubaliana. Imetokea nini? Tulikubaliana kutekeleza jambo
hilo sasa tunaendelea kujadili nini?”
Amesisitiza Rais
Kikwete: “Nchi yetu itachelewa sana kupata maendeleo kwa sababu kila mtu
anayepewa kazi anataka kuanza kujadili. Tanzania haiwezi kuendelea kwa mijadala
na kwa vikao vya kulipana posho visivyoisha. Hatuwezi kuendeleza nchi kwa
mwenendo huu – Frontline Company imeanza kuomba ardhi ya kulima kiasi cha miaka
mitano iliyopita…”
Rais Kikwete ambaye
amewaamuru viongozi wote wanaohusika na suala hilo kukutana wiki ijayo
amesema: “Nchi inakwamishwa na watu wa namna hii, kila siku kuzungumza na kujadiliana…hadithi
haiishi. Maendeleo yetu yanachelewa kwa sababu mizunguko – kila siku
mnazunguka, hamumalizi.”
Mapema Rais Kikwete
amewaambia viongozi wa kambi hiyo ambayo inamilikiwa na RUBADA kuwa kazi ya
kambi hiyo iwe ni kuandaa vijana wa kujiajiri kwa kilimo cha kisasa na siyo
kuandaa watu wa kutafuta kazi ya kuajiriwa katika kilimo.
“Tunaandaa wakulima
wazuri, vijana, na siyo tunaandaa kundi la watu wa kutafuta ajira ya kilimo.
Hatuwezi kuwa na kambi ya namna hii ikiandaa kundi la watu wa kutafuta
ajira…kijijini utaajiriwa na nani kama siyo kushiriki kilimo?”
Rais Kikwete, hata
hivyo, amesema kuwa amefurahishwa na uamuzi wa kuandaa vijana hao kushiriki
katika kilimo kwa sababu mageuzi ya kilimo yataletwa na vijana.
“Tukiingiza vijana
katika shughuli za kilimo basi mageuzi ya kilimo katika nchi yetu yanawezekana
kwa sababu ni dhahiri kuwa mageuzi ya kilimo yatakuwa magumu kuletwa na baba
zao, na magumu zaidi kuletwa na babu zao.”
Rais ambaye alikuwa
kwenye ziara ya Wilaya ya Rufiji pia amezindua mradi mkubwa wa maji mjini
Kibiti na amekabidhiwa boti ambazo zitafanya shughuli za kubeba wagonjwa katika
maeneo ya Nyamisati na visiwa vya jirani.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
5 Oktoba, 2013
CHANZO: NA H@KI NGOWI
0 comments:
Post a Comment