SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Monday, October 28, 2013

Rais Jakaya Kikwete na Mama Salma Kikwete Watoa Pole Kwa Mjane na Familia Ya Mwanadiplomasia na Mwanasiasa Mkongwe, Balozi Isack Sepetu

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete  akiweka saini katika kitabu cha maombolezo ya msiba wa Balozi Isaac Sepetu  alipokwenda  nyumbani kwa marehemu Sinza Mori, Dar es salaam, kutoa pole. Marehemu Sepetu aliyefariki jana katika jijini Dar es salaam.
 Mama Salma Kikwete  akiweka saini katika kitabu cha maombolezo ya msiba wa Balozi Isaac Sepetu  nyumbani kwa marehemu Sinza Mori, Dar es salaam. . Marehemu Sepetu aliyefariki jana katika jijini Dar es salaam.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimfariji  mjane wa Balozi Isaac Sepetu, Mama Miriam Sepetu, alipokwenda na Mama Salma nyumbani kwa marehemu Sinza Mori, Dar es salaam, kutoa pole kwa mjane huyo na familia ya Marehemu Sepetu aliyefariki jana jijini
Dar es salaam.
Mke wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete  akimfariji mjane wa Balozi Isaac Sepetu alipokwenda  nyumbani kwa marehemu Sinza Mori, Dar es salaam, kutoa pole kufuatia msiba Marehemu Sepetu aliyefariki jana katika jijini Dar es salaam.
 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitoa pole kwa wanafamilia wa Balozi Isaac Sepetu alipokwenda na Mama Salma nyumbani kwa marehemu Sinza Mori, Dar es salaam, kutoa pole kufuatia msiba Marehemu Sepetu aliyefariki jana  jijini Dar es salaam.
 
Picha na IKULU

****

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe kufuatia kifo cha Mwanadiplomasia na Mwanasiasa Mkongwe, Balozi Isack Sepetu aliyefariki dunia tarehe 27 Oktoba, 2013 katika Hospitali ya TMJ ya Jijini Dar es Salaam alikopelekwa kwa matibabu ya ugonjwa wa Kisukari na Kiharusi.
Marehemu Balozi Isack Sepetu, enzi za uhai wake, aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za juu Serikalini kuanzia miaka ya Sabini ambapo aliwahi kuteuliwa  kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, Waziri wa Habari, Utangazaji na Utalii katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
            Katika miaka ya Tisini, aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Mipango na Uchumi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliyoongozwa na Dr. Salmin Amour.  Akiwa Balozi wa Tanzania, Marehemu aliiwakilisha nchi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na uliokuwa Muungano wa Nchi za Kisovieti za Kisoshalisti za Urusi (USSR) ambayo kwa sasa ni Russia.
“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mwanasiasa na Mwanadiplomasia Mashuhuri, Balozi Mstaafu, Mheshimiwa Isack Sepetu aliyefariki dunia katika Hospitali ya TMJ Jijini Dar es Salaam alikopelekwa kwa matibabu ya ugonjwa wa Kisukari na Kiharusi tarehe 27 Oktoba, 2013”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.
Rais Kikwete amesema alimfahamu Marehemu Balozi Isack Sepetu, enzi za uhai wake, kama Mwanasiasa na Kiongozi mwenye bidii na uwezo mkubwa wa uongozi ambaye alidhihirisha uaminifu na uadilifu  wake katika nyadhifa mbalimbali alizowahi kushikilia katika Awamu zote za Uongozi Tanzania Bara na Zanzibar.  Balozi Sepetu aliwahi pia kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nafasi ya kuteuliwa na Mwenyekiti wa Chama, na kukitumikia Chama kwa uaminifu na uadilifu mkubwa.
“Natambua hata baada ya kustaafu, Marehemu Balozi Isack Sepetu aliendelea kuaminiwa katika utumishi wake, na hivyo kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, na pia Mjumbe wa Bunge la Afrika Mashariki hadi mauti yalipomkuta”, amesema Rais Kikwete, na kuongeza,
“Kutokana na msiba huo mkubwa, ninakutumia wewe Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe Salamu zangu za Rambirambi kwa kumpoteza Mwanadiplomasia na mmoja wa Viongozi shupavu katika nchi yetu, Marehemu Balozi Isack Sepetu”.
“Kupitia kwako, naomba pia Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi ziwafikie Wanafamilia ya Marehemu kwa kumpoteza Kiongozi na Mhimili Madhubuti wa Familia.  Nawaomba wote wawe na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo kwani yote ni mapenzi yake Mola”.
Rais Kikwete amewahakikishia Wanafamilia ya Marehemu Balozi Isack Sepetu kuwa yuko pamoja nao katika kipindi chote cha majonzi kufuatia kifo cha mpendwa wao.
 
  Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi Roho ya Marehemu Balozi Isack Sepetu, Amina.
 
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
28 Oktoba, 2013

0 comments:

Post a Comment