SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Saturday, October 5, 2013

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WANANCHI, TAREHE 4 OKTOBA, 2013


HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WANANCHI, TAREHE 4 OKTOBA, 2013

Ndugu Wananchi;

Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kumaliza mwezi Septemba salama na kuwasiliana kwa kutumia utaratibu wetu huu mzuri. Naomba radhi kuzungumza nanyi siku ya leo kwa sababu nilikuwa safari na nilirejea jioni ya tarehe 30 Septemba, 2013. Awali nilifikiria nisiseme, nisubiri mwisho wa mwezi wa Oktoba. Lakini, baada ya kupata taarifa ya yaliyojiri, nimeshauriwa na nimekubali angalau niyasemee baadhi ya mambo huenda itasaidia. Niwieni radhi nisipoyasemea baadhi ya mambo siyo kwa kuyapuuza, bali kwa kuepuka hotuba kuwa ndefu mno. Nitayatafutia mahali pengine pa kuyasemea.

Uhusiano na Rwanda

Ndugu Wananchi;

Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi wa Julai, nilizungumzia hali ya uhusiano wetu na Rwanda kutokuwa mzuri na tatizo la ujambazi na wahamiaji haramu katika Mikoa ya Kigoma, Geita na Kagera. Nafurahi kusema kuwa kwa yote mawili kuna maendeleo ya kutia moyo.(P.T)

Tarehe 5 Septemba, 2013, nilikutana na kuzungumza na Mheshimiwa Rais Paul Kagame wa Rwanda mjini Kampala. Tuliitumia fursa ya ushiriki wetu katika Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu kuzungumzia uhusiano baina yetu na nchi zetu. Mazungumzo yalikuwa mazuri na sote tulikubaliana kuwa yaliyopita si ndwele tugange yajayo. Kwa sababu hiyo tulielewana kuwa tutengeneze mazingira yatakayosaidia kutuliza hali na kurudisha nchi zetu katika uhusiano mwema kama ilivyokuwa siku zote. Nawaomba ndugu zangu hususan wanasiasa, watumishi wa umma, wanahabari na wenye mitandao ya kijamii na blog na wananchi kwa ujumla tusaidie kuimarisha uhusiano mwema baina ya Rwanda na Tanzania na watu wake.

Majambazi na Wahamiaji Haramu

Ndugu Wananchi;

Katika hotuba hiyo pia nilisema kuwa tutachukua hatua thabiti dhidi ya majambazi na wageni wanaoishi nchini bila ya kuzingatia taratibu zinazohusika. Niliwataka majambazi wajisalimishe wao na silaha zao kwa hiari. Wale wanaoishi nchini bila ya kuwa na kibali halali wahalalishe ukaazi wao au warejee makwao. Nilitoa siku 14 kuanzia tarehe 29 Agosti, 2013 wafanye hivyo kwani baada ya hapo tungeanzisha operesheni maalum ya kushughulika na watu wa makundi yote mawili.

Ndugu Wananchi;

Kumekuwepo na mafanikio ya kutia moyo. Kwa upande wa wahamiaji wanaoishi nchini kinyume cha sheria watu wapatao 21,254 waliondoka kwa hiari. Hali kadhalika zaidi ya ng'ombe 8,000 waliondolewa na silaha 102 zilisalimishwa. Baada ya operesheni kuanza tarehe 6 Septemba, 2013 na kumalizika tarehe 20 Septemba, 2013, wahamiaji haramu 12,828 walirejeshwa makwao na watuhumiwa 279 wa unyang'anyi wa kutumia silaha walikamatwa. Aidha, mabomu 10 ya kutupa kwa mkono (offensive hand grenades), silaha 80, risasi 780 na mitambo 2 ya kutengeneza magobole vilikamatwa. Pia, ng'ombe 8,226 walikamatwa wakichungwa katika mapori ya hifadhi. Kwa upande wa mazao ya misitu, mbao 2,105 zilikamatwa pamoja na nyara mbalimbali za Serikali.

Ndugu Wananchi;

Agizo la kuwataka watu wanaoishi nchini isivyo halali wahalalishe ukaazi wao au waondoke kwa hiari au wataondolewa lilipotoshwa hasa na vyombo vya habari vya nje ya Tanzania. Walikuwa wanadai eti Tanzania ilikuwa inafukuza wakimbizi. Madai hayo si ya kweli hata kidogo. Hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2013 wakimbizi 68,711 walikuwepo kwenye Kambi ya Nyarugusu, Mkoani Kigoma. Hakuna mkimbizi ye yote aliyetakiwa kuondoka. Ukweli ni kwamba hakuna mtu ye yote kati ya wale watu walioondoka kwa hiari au kusaidiwa kuondoka wakati wa operesheni ambaye ni mkimbizi. Kama ingekuwa hivyo, wa kwanza kulalamika wangekuwa wenzetu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa. Bahati nzuri jambo hilo halikutokea.

Ndugu Wananchi;

Yalikuwepo pia madai kwamba tunawaonea na kuwatesa watu walioishi nchini miaka mingi. Ati iweje sasa ndiyo waambiwe kuwa siyo raia. Siku zote Serikali ilikuwa wapi? Uraia haupatikani kwa kuishi nchi ya kigeni kwa miaka mingi. Unapatikana kwa kutimiza masharti ya kuomba na kupewa uraia. Kama mtu hakufanya hivyo anabaki kuwa raia wa nchi aliyotoka au walikotoka wazazi wake. Ipo mifano ya watu mashuhuri ambao walilazimika kuachia nyadhifa zao baada ya kugundulika kuwa siyo raia. Hawakuwa wanaonewa, ndiyo matakwa ya Katiba na Sheria za nchi yetu.

Ndugu Wananchi;

Katika kutekeleza operesheni hii niliagiza kuwa wale watu ambao wameishi hapa nchini miaka mingi ambao wana nyumba, mashamba au mali mbalimbali au wameoa au kuolewa na wana watoto au hata wajukuu waelekezwe kuhalalisha ukaazi wao. Iwapo watakataa kufanya hivyo basi wasaidiwe kurejea kwao. Pia niliagiza watu wasiporwe mali zao wala kudhulumiwa. Sijapata taarifa ya kufanyika kinyume na maelekezo yangu. Lakini kama wapo watu waliotendewa tofauti, taarifa itolewe kwa Wakuu wa Wilaya na Mikoa au hata Ofisi ya Rais ili hatua zipasazo zichukuliwe. Hatutaki watu wadhulumiwe au kuonewa.

Napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Waziri wa Ulinzi na JKT, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi kwa uongozi wao mzuri katika zoezi hili. Pia, nawapongeza Makamanda na askari wa JWTZ na Polisi pamoja na maafisa wa Idara ya Uhamiaji, Idara ya Mifugo, Idara ya Wanyamapori, Idara ya Misitu na Idara nyinginezo za Serikali kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya. Najua awamu ya kwanza imeisha tarehe 20 Septemba, 2013 na kama nilivyosema kuwa safari hii operesheni itakuwa endelevu, muda si mrefu awamu ya pili itafuata. Nawaomba waendelee kuchapa kazi kwa bidii, maarifa na nidhamu ya hali ya juu.

Ziara ya Canada na Marekani

Ndugu Wananchi;

Kati ya tarehe 17 na 28 Septemba, 2013 nilifanya ziara ya kikazi katika nchi za Canada na Marekani. Nchini Canada nilitembelea Chuo Kikuu cha Guelph ambapo nilitunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu kwa kutambua jitihada zetu tuzifanyazo kujiletea maendeleo na mafanikio ya kutia moyo tunayoendelea kupata licha ya changamoto zinazotukabili. Katika mazungumzo yangu na uongozi wa chuo hicho wamekubali kuwa na ushirikiano wa karibu na Wizara zinazohusika na Elimu, Kilimo na Mifugo pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Morogoro na Chuo Kikuu cha Dodoma. Nimewataka Mawaziri wa Wizara hizo na viongozi wa vyuo hivyo kuchangamkia fursa hiyo bila kuchelewa.

Ndugu Wananchi;

Nchini Marekani nilikutana na kuzungumza na maafisa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya nchi hiyo wakiwemo Rais Barack Obama na baadhi ya Wabunge wa Bunge la Marekani. Mazungumzo yetu yalilenga kuimarisha ushirikiano baina ya nchi zetu na mambo yalienda vizuri. Wote walituhakikishia kuwa mambo tuliyoyazungumza na kukubaliana na Rais Barack Obama wakati wa ziara yake nchini yanaendelea kufanyiwa kazi. Miongoni mwa hayo maombi yetu ya kupatiwa vitabu milioni 2.4 vya sayansi na hisabati yamekubaliwa na utekelezaji umeanza. Upatikanaji wa vitabu hivyo utamwezesha kila mwanafunzi wa sekondari kuwa na kitabu chake.

Ndugu Wananchi;

Jambo lingine kubwa na la faraja kwetu ni kuwa mapendekezo yetu ya miradi ya umeme na barabara za vijijini za kugharamiwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika lao la Changamoto za Milenia yamepokelewa vizuri. Kinachosubiriwa ni miradi ipi itakubaliwa na Bodi ya MCC na kiasi gani cha fedha kitatengwa na Bunge la Marekani kwa ajili hiyo.

Tuzo ya Uhifadhi

Jambo lingine muhimu katika safari yangu ya Marekani ni kutunukiwa tuzo na "International Congressional Conservation Foundation" kwa kutambua juhudi zetu katika kuhifadhi wanyama pori na mafanikio tuliyoyapata. Licha ya changamoto mbalimbali tunazokabiliana nazo, tuzo hii imetupa moyo wa kuongeza nguvu katika jitihada tunazozifanya sasa kupambana na ujangili na matatizo mengine ya uhifadhi wa wanyama na misitu.

Ndugu Wananchi;

Kilichotupa moyo zaidi ni kauli za utayari wa kutusaidia katika mapambano hayo zilizotolewa wakati wa kupewa tuzo na katika mkutano wa mfuko wa Maendeleo wa Clinton na katika mkutano maalum wa kupambana na ujangili na biashara ya meno ya tembo duniani.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Ndugu Wananchi;

Shabaha kuu ya safari yangu ya Marekani ilikuwa kuhudhuria Mkutano wa 68 wa Umoja wa Mataifa unaoendelea jijini New York mpaka Desemba, 2013. Mada kuu ya mkutano wa mwaka huu ni kuandaa agenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 yaani: Post 2015 Development Agenda: Setting the Stage. Kama mtakavyokumbuka Malengo ya Milenia yaliyoamuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2000, yanafikia ukomo wa utekelezaji wake mwaka 2015.

Katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu mjadala umehusu nini kifanyike baada ya mwaka 2015. Hata hivyo, mjadala huo unaanza kwa kufanya tathmini ya utekelezaji wa yale Malengo Manane ya Milenia ya mwaka 2000 umefikia wapi mpaka sasa na utafikia wapi mwaka 2015 kwa kila nchi na kwa dunia kwa ujumla. Tathmini ya jumla inaonesha kuwa kumekuwepo na jitihada kubwa ya kutekeleza malengo haya katika kila nchi. Yapo malengo ambayo utekelezaji wake umefikia shabaha hivi sasa na yapo ambayo upo uwezekano wa shabaha kufikiwa ifikapo mwaka 2015. Vile vile yapo ambayo shabaha haitafikiwa.

Ndugu Wananchi;

Kwa upande wetu, Tanzania, tumefikia shabaha katika mambo yafuatayo:

(1) Lengo la Milenia namba 2 kuhusu uandikishaji wa watoto wenye umri wa kwenda shule ya msingi;

(2) Lengo la Milenia namba 3 hasa kuhusu usawa wa kijinsia katika Shule za Msingi na Sekondari. Ukweli ni kwamba, wasichana wanaanza kuwa wengi kuliko wavulana. Hatujafikia shabaha kwa upande wa usawa wa kijinsia katika elimu ya juu na ni vigumu kulifikia ifikapo 2015. Pia hatujafikia lengo kwa upande wa usawa wa Wabunge wanawake na wanaume. Hata hivyo, kwa kutumia mchakato wa Katiba unaoendelea sasa tunaweza kufikia lengo katika uchaguzi wa 2015 iwapo tutaamua iwe hivyo;

(3) Lengo la Milenia namba 4 kuhusu kupunguza idadi ya vifo vya watoto wachanga na wale wenye umri chini ya miaka mitano;

(4) Tumefikia shabaha kwa Lengo la Milenia Namba 6 kuhusu kupunguza maambukizi ya UKIMWI; na

(5) Kwa upande wa lengo namba 7 kuhusu mazingira, tumefikia shabaha kwa upande wa upatikanaji wa maji mijini. Bado tuko nyuma kwa maji vijijini ingawaje tunaweza kufikia lengo ifikapo mwaka 2015 kama tutaendeleza uwekezaji tulioamua kufanya katika bajeti ya mwaka huu. Lakini, hatutaweza kufikia shabaha kwa upande wa usafi wa mazingira mijini na vijijini ifikapo mwaka 2015. Safari bado ndefu sana.

Ndugu Wananchi;

Malengo ya Milenia namba 1 na namba 5 ambayo bado tuko nyuma sana ya shabaha hatutafikia lengo ifikapo 2015. Tumeendelea kutekeleza lengo la Milenia namba 1 kuhusu kupunguza umaskini na njaa kwa zaidi ya nusu kutoka kiwango cha mwaka 2000. Hatua tunazochukua kuleta mageuzi katika kilimo zina lengo la kuhakikisha usalama wa chakula na kuongeza mapato ya wakulima. Mafanikio yanaanza kuonekana lakini si ya kiwango cha kutufikisha kwenye lengo ifikapo mwaka 2015. Tunao, pia, mpango wa kupanua programu ya TASAF ya Conditional Cash Transfer ili tuwafikie watu wengi maskini. Hata kama tutafanikiwa kuutekeleza mapema mpango huu utatusogeza sana mbele lakini bado tutakuwa chini ya lengo kwa upande wa kupunguza umaskini ifikapo 2015.

Ndugu Wananchi;

Kwa upande wa Lengo la Milenia namba 5, kuhusu afya ya kina mama wajawazito bado tuko nyuma katika kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na kuongeza idadi ya wajawazito wanaojifungua chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya. Hatutaweza kufikia shabaha ifikapo mwaka 2015. Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (2007 – 2017) una nia ya kukabiliana na matatizo haya. Tumeongeza ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali, tumeboresha upatikanaji wa dawa na tumepanua sana mafunzo ya madaktari, wauguzi na wakunga mambo ambayo yamesaidia kutufikisha hatua tuliyopiga mpaka sasa. Naamini juhudi zetu tukiziendeleza zitatusogeza mbele zaidi ingawaje bado tutakuwa chini ya lengo. Miaka michache ijayo, tatizo hili nalo litakuwa historia.

Ndugu Wananchi;

Lengo la Milenia namba 8 linazihusu nchi tajiri kuongeza michango yao kusaidia nchi zinazoendelea kutekeleza Malengo ya Milenia. Bahati mbaya sana mataifa tajiri hayajafikia viwango wanavyotarajiwa kutoa na hata vile wanavyoahidi wenyewe kutoa katika majukwaa mbalimbali. Kama wangetimiza ahadi zao, sura ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia ingekuwa tofauti kabisa.

Ndugu Wananchi;

Hiyo ndiyo hali ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia hapa nchini. Hakuna nchi ye yote duniani iliyofanikiwa kutekeleza shabaha za malengo yote kwa ukamilifu. Ushauri wa viongozi wote waliozungumza ulitaka mataifa yaliyoendelea yatimize ahadi zao za kuchangia utekelezaji wa Malengo ya Milenia. Ilionekana suala la upatikanaji wa fedha halina budi kuangaliwa kwa makini sasa na baada ya mwaka 2015. Bila ya hivyo ufanisi utakuwa mdogo katika kuongeza kasi ya utekelezaji kwa pale paliposalia kufikia malengo ya 2015 na hata kwa Malengo ya baada ya mwaka 2015.

Mashambulizi ya Kigaidi ya Westgate, Nairobi

Ndugu Wananchi;

Wakati nikiwa safarini, tarehe 21 Septemba, 2013 kulitokea shambulilizi la kigaidi katika Jengo la Biashara la Westgate, huko Nairobi, Kenya. Watu 67 walipoteza maisha na zaidi ya 200 walijeruhiwa. Nilituma salamu za pole na rambirambi kwa Mheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta na wananchi wa Kenya na kuwahakikishia kuwa tupo pamoja nao katika wakati huu wa majonzi.

Nafahamu kuwa baada ya tukio hilo watu wengi hapa nchini wameingiwa na hofu kuhusu usalama wetu. Ni hofu ya msingi kwani tarehe 8 Agosti, 1998 Ubalozi wa Marekani hapa nchini ulishambuliwa na magaidi na ndugu zetu 11 wasio na hatia walipoteza maisha.

Ndugu Wananchi;

Napenda kuwafahamisha kuwa tangu shambulio la mwaka 1998, Serikali imekuwa inajenga uwezo wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kupambana na ugaidi katika nyanja mbalimbali. Tunaendelea kujiimarisha bila kusita siku hadi siku. JWTZ, Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa wamekuwa na ushirikiano wa karibu kwa ajili hiyo. Juhudi zetu hizo ndizo zinazotufanya tuwe salama hadi sasa.

Baada ya tukio la Kenya, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimeimarisha mikakati yao maradufu. Pamoja na kujizatiti kwetu huko hatuwezi kusema kuwa tukio la kigaidi halitaweza kutokea nchini. Uhakika huo hatuna kwani hata mataifa makubwa na tajiri yameshambuliwa. Kilicho muhimu ni kuendelea kuchukua tahadhari na wananchi kusaidia ili vyombo vyetu vifanikiwe zaidi.

Hali kadhalika, tumewataka watu wote wenye shughuli zinazokusanya watu wengi kama vile maduka, maofisi, mahoteli, migahawa n.k. waweke kamera za ulinzi nje na ndani ya maeneo yao. Pia waangalie uwezekano wa kuweka vifaa vya upekuzi (metal detectors and x-rays). Najua watu wanaweza kulalamikia usumbufu au gharama, lakini gharama na hasara ya kushambuliwa ni kubwa zaidi kuliko ya usumbufu huo.

Ndugu Wananchi;

Nawaomba muendelee kufanya shughuli zenu bila ya hofu ingawaje msiache kuwa makini na kuchukua tahadhari. Watu watoe taarifa kwa vyombo vya usalama wanapoona mtu au watu au kitu cha kutilia shaka. Ni muhimu kwa usalama wake, wa kila mtu, jamii na taifa. Maafisa husika wa vyombo vya ulinzi na usalama wataendelea kuelimisha umma kuhusu hatua mbalimbali za tahadhari za kuchukua. Sisi Serikalini tumejipanga kuchukua hatua zaidi kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu na watu wake.

Mchakato wa Katiba Mpya

Ndugu Wananchi;

Kama mtakavyokumbuka, Bunge lilitunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Novemba, 2011. Sheria hii imeweka mchakato mzima wa kupata Katiba hiyo na kuunda taasisi zake. Mwezi Mei, 2012, Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa na imekamilisha hatua tatu muhimu katika mchakato huo. Hatua hizo ni kupokea maoni ya wananchi, kutayarisha rasimu ya kwanza ya Katiba Mpya na kupokea maoni ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na ya taasisi. Hivi sasa Tume inaandaa mapendekezo ya Rasimu ya Pili ya Katiba itakayopelekwa kwenye Bunge Maalum. Baada ya tafakuri zake, Bunge Maalum litatoa rasimu ya mwisho ya Katiba ambayo itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya uamuzi wa mwisho kupitia kura ya maoni. Baada ya hatua hiyo, ndipo tutakapokuwa tumepata Katiba Mpya.

Ndugu Wananchi;

Baada ya Bunge la Novemba, 2011 kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kulikuwepo na madai ya kutaka sheria hiyo iboreshwe kutoka vyama vyote vya siasa vikiwemo vyama vya upinzani na Chama tawala. Majadiliano yalifanyika baina ya Serikali na vyama hivyo pamoja na shirikisho la asasi za kiraia. Makubaliano yalifikiwa kuwa marekebisho yafanyike kwa awamu. Awamu ya kwanza ihusishe Tume ya Mabadiliko ya Katiba kisha hapo yafanyike marekebisho yanayohusu Bunge Maalum na mwisho Kura ya Maoni.

Kama ilivyokuwa kwa mabadiliko yaliyohusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba, safari hii nayo vyama vya siasa vilitoa mapendekezo yao. Yalifanyika mazungumzo kati yao na Serikali na maelewano kufikiwa kuhusu maeneo ya kufanyiwa marekebisho. Serikali ilitayarisha rasimu ya Muswada na kuuwasilisha kwa wenzetu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Ndugu Wananchi;

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitoa mapendekezo yake na ushauri kwenye maeneo mawili. Kwanza kwamba uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum ufanywe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na kuafikiana na Rais wa Zanzibar. Pili walishauri kwamba kama Bunge Maalum litashindwa kufikia maamuzi ndani ya siku 70 zilizopendekezwa, liweze kuongezwa muda hadi kufikia siku 90. Maeneo mengine ya Muswada waliafikiana nayo.

Ndugu Wananchi;

Kwa kuzingatia utaratibu wa kutunga Sheria, Serikali ilifikisha Muswada kwa Spika wa Bunge ambaye nae aliuwasilisha kwenye Kamati ya Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala. Kama ilivyo ada, Kamati hiyo ilifanya vikao na wadau na kupokea maoni yao kuhusu Muswada. Nimeambiwa kulikuwa na mjadala wa kina na mapendekezo mazuri yalitolewa na wadau. Kisha hapo Wajumbe wa Kamati walikaa wenyewe kujadili Muswada walikuwepo pia Wabunge ambao si Wajumbe wa Kamati walioshiriki kwa vile Kanuni zinaruhusu. Nimeambiwa pia kwamba mjadala ulikuwa mpana na wa kina zaidi. Mapendekezo kadhaa yalitolewa na Wajumbe kuhusu vifungu mbalimbali vya Muswada.

Ndugu Wananchi;

Nimefahamishwa kuwa Wabunge wa vyama vyote walichangia na kwamba baadhi ya nyakati mambo yalipokuwa ugumu mawazo mazuri ya baadhi ya Wabunge wa upinzani yalisaidia kupata ufumbuzi. Nimeambiwa pia kwamba Wajumbe wa Kamati na upande wa Serikali walikubaliana kwa maeneo mengi isipokuwa machache ambayo walikubaliana kwa pamoja wayapeleke Bungeni ili Wabunge nao wayajadili na kuyapatia ufumbuzi.

Ndugu Wananchi;

Baada ya Kamati kumaliza kazi yake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Mathias Chikawe aliwasilisha Muswada Bungeni. Akafuatiwa na Mheshimiwa Gosbert Blandes kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, kutoa maoni ya Kamati. Baadaye Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Mheshimiwa Tundu Lissu alitoa maoni yake.

Ndugu Zangu;

Baada ya watu hao watatu kutoa maoni yao ilitarajiwa kuwa Wabunge wangeanza kujadili Muswada. Naambiwa mambo hayakuwa hivyo. Badala yake kukazuka malumbano baina ya Spika na baadhi ya Wabunge wa Upinzani wakitaka Muswada usijadiliwe. Ilifikia wakati hoja hiyo ikabidi iamuliwe kwa kura ambapo ilishindwa. Katika hali isiyotarajiwa, Wabunge wote wa upinzani wakatoka nje ya Bunge isipokuwa wawili. Kitendo hicho kimewanyima Wabunge wengi wa upinzani fursa ya kutetea hoja zao walizozitoa kupitia hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani. Pia wamejinyima nafasi ya kusema mambo mengine wakati wa mjadala na Kamati ya Bunge zima.

Wabunge waliokuwepo waliendelea kuujadili Muswada na kutoa hoja na mapendekezo ya kuuboresha. Walifanya hivyo wakati wa mjadala na wakati wa kupitia kifungu kwa kifungu. Baadhi ya hoja na mapendekezo yalikubaliwa na mengine yalikataliwa. Miongoni mwa yaliyokubaliwa na Wabunge, kwa mfano, ni kuhusu elimu ya mtu atakayekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum na lile la ukomo wa uhai wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Ndugu Wananchi;

Kwa maoni yangu madai ya Kambi ya Upinzani yanazungumzika na hata baadhi yangeweza kukubalika kama Wabunge wake wangekuwepo Bungeni na kushiriki mchakato wote wa kujadili na kupitisha Miswada Bungeni. Bahati mbaya hawakuwepo, hivyo hapakuwepo na mtu wa kusema mawazo yao. Baada ya kupoteza fursa yao halali, kutaka kupata ufumbuzi nje ya Bunge ni jambo lisilowezekana. Haya ni masuala yanayohusu Bunge ambayo hujadiliwa na kuamuliwa Bungeni na si vinginevyo. Kuandamana nchi nzima au kuchukua hatua za kutotii sheria kama Mwenyekiti wa CHADEMA, Mheshimiwa Freeman Mbowe anavyotaka, hakutaleta mabadiliko wanayoyataka katika sheria hii. Naamini na wao wanautambua ukweli huo.

Ndugu Wananchi;

Kuna msemo wa wahenga kuwa "historia hujirudia". Naomba hekima ziwaongoze viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi na zituongoze sote kutumia utaratibu tulioutumia mwaka 2012. Kulipotokea mazingira kama haya pande zote zilikaa pamoja na kuzungumzia hoja moja baada ya nyingine na kukubaliana nini kifanyike na kifanyike vipi. Baada ya kuridhiana hatua zipasazo za kisheria na kanuni zilichukuliwa na kumaliza mzozo.

Ndugu Wananchi;

Kufanya kinyume cha hayo hakutaleta ufumbuzi wa mzozo huu. Tutaliingiza taifa kwenye matatizo yasiyokuwa ya lazima. Tukikataa kufanya hayo Watanzania wanayo kila sababu ya kuhoji dhamira zetu na kutilia shaka nia zetu. Watakuwa na haki ya kuuliza nia ni hii yetu sote ya kupata Katiba Mpya kwa kutumia njia za kikatiba na kisheria au tuna dhamira nyingine iliyojifisha?

Kama dhamira yetu ni kutaka kupata Katiba mpya kwa mujibu wa Katiba na Sheria, ushauri wangu na rai kwa ndugu zetu wa CHADEMA, CUF na NCCR-Maguezi ni kuwa waachane na mipango ya maandamano na kufanya ghasia. Badala yake watumie njia halali zinazotambulika kikatiba na kisheria kujenga hoja za kufanya marekebisho wanayoyaona wao yanafaa kuboresha Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Tukifanya hivyo tutakuwa tunajenga badala ya kubomoa. Tutaliponya taifa. Sisi katika Serikali tuko tayari.

Ndugu Wananchi;

Napenda pia kuzisemea baadhi ya hoja zilizotolewa na Kambi ya Upinzani. Kwanza kabisa nasema kuwa nimesikitishwa sana na madai na tuhuma za uongo eti katika uteuzi wa Tume ya Katiba sikuheshimu mapendekezo ya TEC, CCT na walemavu.

Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;

Siyo tu kauli hiyo ya Mheshimiwa Tundu Lissu ni uzushi na uongo mtupu bali pia ni ya unafiki, fitina na uzandiki wa hali ya juu. Nasema hivyo kwa sababu, sipendi kuamini kuwa Mheshimiwa Mbunge amesema yale kwa kutokufahamu ukweli au kwa bahati mbaya. Amesema yale kwa makusudi mazima ya kupotosha ukweli ili pengine isaidie kujenga hoja yake ya kutaka Rais asiteue wale Wajumbe 166 wa Bunge Maalum.

Napenda ieleweke kuwa siishabikii kazi hiyo, lakini kwa kutimiza wajibu na maslahi ya taifa nikiagizwa na Sheria za nchi nitafanya. Nasema hivyo kwa sababu nafahamu ni kazi ngumu. Kama kazi ya uteuzi wa Wajumbe 30 wa Tume haikuwa rahisi hata kidogo, hii ya uteuzi wa watu 166 itakuwa ngumu zaidi. Ile ya Tume ilikuwa ngumu kwa namna mbili. Kwanza, kwamba taasisi zilizoomba na waombaji walikuwa wengi mno kuliko nafasi za kujaza yaani 15 Zanzibar na 15 Bara. Zanzibar ziliomba taasisi zaidi ya 60 na waombaji walikuwa zaidi ya 200 wakati Bara kulikuwa na taasisi zaidi ya 170 zikiwa na waombaji zaidi ya 500. Kupata watu 30 kutoka orodha kubwa kiasi hicho si mtihani mdogo. Pili kwamba tulitakiwa kuunda Tume inayoasili sura ya taifa, yaani watu wa nchi yetu kwa maeneo, vyama vya siasa, dini, wanawake, vijana, walemavu, wafanyakazi, wasomi, Wabunge, Wawakilishi, wanasheria, wafanyabiashara, wakulima, asasi za kiraia n.k.

Ndugu Wananchi;

Pamoja na changamoto hizo, lakini tulifanikiwa kuunda Tume iliyopokelewa vizuri na jamii na kufanya watu wengi hata wale ambao hawakuteuliwa wahisi kuwakilishwa. Tulifanyaje? Kwanza kabisa tulihakikisha kuwa tunapata wawakilishi wa vyama vya siasa vyenye wawakilishi Bungeni na kwenye Baraza la Wawakilishi na tunapata wawakilishi wa mashirika ya dini zetu kubwa yaani, TEC, CCT na BAKWATA. Ndiyo maana nikasema kuwa kwa Mheshimiwa Tundu Lisu kudai kuwa mapendekezo ya TEC na CCT hayakuheshimiwa ni uongo wa mchana usiokuwa na kichwa wala miguu.

Baada ya hapo ndipo tukaangalia waombaji wa makundi na taasisi nyingine. Tulijitahidi sana kupata watu ambao wanawakilisha kundi zaidi ya moja. Tulifikiria hivyo kwa sababu ni ukweli ulio wazi kuwa si kila taasisi iliyoomba itapata mwakilishi kwani hata tungependa iwe hivyo nafasi hazikuwepo. Kwa kutumia utaratibu huu makundi mengi yamepata uwakilishi kutokana na watu waliopendekezwa na makundi mengi. Tumefanya kazi kubwa sana ya kuwianisha mambo na makundi ya maslahi mbalimbali nchini.

Ndiyo maana naiona mantiki ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akishirikiana na Rais wa Zanzibar wa kuwateua Wajumbe wa Bunge Maalum. Dhana kuwa kila kikundi kiteue chenyewe watu ingefaa sana kama kungekuwepo na nafasi za kutosha kila kundi nchini. Hilo haliwezekani, labda tuwe na Bunge Maalum lisilokuwa na ukomo wa wajumbe.

Ndugu Wananchi;

Mimi na Rais wa Zanzibar tumekuwa tunajiuliza baada ya kazi ngumu na nzuri tuliyoifanya na iliyopongezwa na wengi ya kuteua Tume ya Mabadiliko ya Katiba nini kilichoharibika sasa hata tuonekane hatuaminiki kuteua hawa 166? Kama ni kwa sababu za Mheshimiwa Tundu Lissu, nimeshasema hazina ukweli wowote. Ninapojiuliza kwa nini aseme uongo nashindwa kupata jibu linaloingia akilini. Wakati mwingine nafikiria kuwa ni hiana. Lakini nadhani ni hila za kisiasa zenye nia ya kutaka kupata watu wa kutetea maslahi ya chama chake. Kama hiyo ndiyo shabaha basi amekosea sana.

Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;

Hatutengenezi Katiba ya Chama fulani bali Katiba ya nchi, Katiba ya watu wa vyama vyote na wasiokuwa na vyama ambao ndiyo wengi kuliko wote. Lazima tuongozwe na ukweli huo na tuwe na msimamo huo wakati wote. Lazima tukumbuke kuwa si watu wote wanaostahili au kuwa na sifa ambao wataomba na kupata nafasi ya kuwa Wajumbe, hivyo wale wachache watakao bahatika lazima wawasemee wote. Wanatakiwa kusikiliza na kuwakilisha mawazo ya wote hata wale wasiokuwa wa Chama chao au kundi lao.

Ndugu Wananchi;

Bahati nzuri hii ndiyo sifa kubwa iliyooneshwa na Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Wamewasimamia na kuwasemea watu wote bila ya kubagua. Natambua kuwepo kwa baadhi ya watu ambao hawafurahii msimamo huo na matokeo ya kazi yao. Watu hao kuwalaumu Wajumbe wa Tume kwa ajili hiyo ni kuwaonea na kutowatendea haki. Tunataka watakaokuwa Wajumbe wa Bunge Maalum nao waige mfano huu mzuri. Wajali maslahi mapana ya taifa letu na watu wake badala ya kujali yale ya taasisi zao au makundi yao.

Zanzibar Kutokushirikishwa

Ndugu Wanachi;

Nimeambiwa pia kuliwepo madai ya Zanzibar kutokushirikishwa ipasavyo. Nimeeleza kwa kiasi gani Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeshirikishwa na kutoa maoni yake yaliyojumuishwa katika Muswada. Hivyo basi napata tabu kuyaelewa madai kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikushirikishwa msingi wake nini! Labda kuna kitu sikuambiwa!

Nimeulizia kuhusu hoja ya Kamati kutokufanya vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau wa Zanzibar. Nimeambiwa kuwa Kanuni za Bunge hazina sharti hilo hivyo Kamati haistahili kulaumiwa. Kama hivyo, nashauri kuwa suala hili lirudishwe Bungeni ili Wabunge walizungumze na kulifanyia uamuzi muafaka. Vinginevyo watu wataendelea kulauminiana isivyostahili. Hivyo basi, kuligeuza jambo hili kuwa ni suala la kukataa Muswada au kususia vikao vya Bunge au kufanya maandamano sidhani kama ni sawa.

Ndugu Wananchi;

Nimeambiwa pia kuwa kulikuwa na hoja ya kutaka idadi ya Wajumbe wa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar iwe sawa kama ilivyo kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Sababu ya idadi ya Wajumbe wa Tume kuwa sawa inatokana na utaratibu wao wa kufikia uamuzi. Ni kwa maelewano ya wote (consensus) na siyo kwa kupiga kura. Ndiyo maana idadi imewekwa sawa ili sauti za pande zote zisikike sawia. Bunge Maalum lina sharti la kufanya uamuzi kwa theluthi mbili ya kura za kila upande kukubali. Bila ya hivyo hakuna uamuzi.

Hivyo basi, katika Bunge Maalum nguvu si uwingi wa kura ambazo upande fulani unaweza kupata bali ni ulinganifu sawa wa kura za kila upande peke yake. Huu ndiyo msingi unaotumika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi sasa kwa lengo la kulinda maslahi ya Zanzibar. Zanzibar ina Majimbo 50 ya uchaguzi na Tanzania Bara ina Majimbo 189, hivyo ukiamua kwa wingi kila wakati Wazanzibari watashindwa. Lakini, hapajakuwepo madai ya Zanzibar nao kutaka kuwa na idadi sawa ya majimbo kama Bara au kupunguza majimbo ya Bara yawe sawa na ya Zanzibar kwa sababu wingi si hoja. Msingi unaotumika ni kutoa nguvu sawa za uamuzi kwa kila upande wa Muungano wakati wa kuamua masuala ya Katiba. Hakuna mdogo wala mkubwa, wote wako sawa. Hakuna mdogo kumezwa na mkubwa. Ndiyo msingi unaopendekezwa kutumika kwenye Bunge Maalum hivyo hakuna kitakachoharibika kwa idadi ya Wajumbe kutokukulingana. Nadhani inafaa ibaki ilivyo. Lakini kama Wabunge wataamua waongeze idadi itakuwa kwa sababu nyingine siyo hii ya mfano wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Ndugu Wananchi;

Katika orodha ya madai ya ndugu zetu wa upinzani lipo suala la uhai wa Tume ya Katiba. Wanataka usiishe wanapokabidhi rasimu ya pili kwa Bunge Maalum bali waendelee kuwepo mpaka mwisho wa mchakato. Nimeulizia ilikuwaje? Nimeelezwa kuwa jambo hili halitokani na mapendekezo ya Serikali wala ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala. Limetokana na pendekezo la Mbunge katika Bunge wakati wa kupitia vifungu na kuungwa mkono na Wabunge wengi. Kwa hiyo kuilaumu Serikali si haki. Serikali inaweza kuwa mshirika katika hoja hii.

Nami naiona hoja ya Wajumbe wa Tume kuwa na wajibu wakati wa Bunge Maalum hasa wa kusaidia kufafanua mapendekezo ya Tume. Je ushiriki huo uwe vipi? Je ni Wajumbe wote au baadhi yao ni jambo linaloweza kujadiliwa.

Ndugu Wananchi;

Naomba nimalizie kwa kuwasihi viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kuongozwa na hekima iliyotumika wakati tulipokuwa na tatizo linalofana na hili kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Mimi naamini kama iliwezekana kufanikisha mambo wakati ule inaweza kufanya hivyo hata safari hii. Itatufikisha pale tunapopataka salama salimini bila maandamano, kushupaliana au uvunjifu wa amani. Kupanga ni kuchagua, naomba sote, mmoja mmoja na kwa umoja wetu tuchague njia ya mazungumzo na maelewano kwani itaihakikishia nchi yetu amani, usalama na utulivu. Tukifanya hivyo historia itatuhukumu kwa wema.

Mungu Ibariki Tanzania.
 Nawashukuru sana kwa kunisikiliza.

0 comments:

Post a Comment