HAINAN AIRLINES
KAMPUNI ya Ndege ya Hainan ya China imekubali kufanya safari za ndege za moja kwa moja kutoka China hadi Tanzania ili kukuza sekta ya biashara na utalii baina ya nchi hizo mbili.
Ahadi hiyo imetolewa leo mchana (Alhamisi, Oktoba 24, 2013) na Mwenyekiti wa Shirika la Ndege la Hainan (Hainan Airlines), Bw. Chen Feng baada ya kuombwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye katika mazungumzo yao alimwomba akubali ndege za shirika lake ziwe zinatua Tanzania. Ndege za shirika hilo zinafanya safari kati ya China na Angola kupitia anga la Tanzania.
Waziri Mkuu ambaye yuko ziara ya kikazi nchini hapa, moja ya eneo ambalo amekuwa anaziomba kampuni za ndege za China ni kufikiria kufanya safari ya moja kwa moja kati ya nchi hizo mbili ili kukuza biashara pamoja na utalii pamoja na kuja kuweza katika ujenzi wa hoteli za kitalii. Pia alisema kuna Watanzania wengi ambao wanakuja China kuchukua bidhaa hapa China lakini wanalazimika kuunganisha safari mara tatu hadi nne kabla hawajafika China jambo ambalo alisema linawaongezea gharama mno.
Akijibu maombi hayo ya Waziri Mkuu, Bw. Chen alisema kutokana na urafiki uliopo baina ya nchi hizo mbili, maombi yake watayafanyia kazi na mojawapo ni hilo la kufungua safari za moja kwa moja za ndege kutoka China kwenda Tanzania.
Lakini alishauri kuwa ili njia hiyo iendelezwe ni lazima kuwepo na utaratibu wa kuhakikisha njia hiyo inakuwa ya kudumu kwa kuwa na abiria wengi na ikiwezekana Tanzania kiwe kitovu cha usafiri wa anga kwa abiria wanaotoka nchi jirani wanaokwenda na kutoka China.
Alisema ili kuweza kuwa kitovu cha usafiri wa China, ni lazima abiria kutoka nchi jirani wapate usafiri wa uhakika wa kuwafikisha katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam ambako wataunganisha safari yao wakitokea katika nchi zao.
Alisema dawa pekee ya kufanikisha hilo ni kuwa na shirika la ndege lenye nguvu la taifa ambalo litashirikiana na Hainan kuhakikisha safari hizo zinakuwa zenye tija na faida kwa kuwafikisha abiria hao kwenye kitovu cha usafiri wa kuunganisha kwenda China.
Pia alisema ili Dar es Salaam iwe kitovu cha usafiri wa anga ni lazima kuwe na uwanja wa ndege mkubwa na wa kisasa zaidi kuliko ilivyo sasa wenye kukidhi mahitaji ya kimataifa (international standards). Alisema kampuni yake iko tayari kuja nchini kushiriki katika kupanua uwanja wa ndege utakaotumiwa na shirika hilo ili uwe wa kisasa.
“Tuna wataaalam waliobobea katika eneo hilo, maana sisi wenyewe tu tunamiliki viwanja vya ndege vipatavyo 16, hivyo mkitushirikisha mtakuwa na uwanja ambao kila aina ya ndege inaweza kutua,” alisema mwenyekiti huyo wa Hainan Airlines.
Bw. Chen pia alisema suala la utalii ni la muhimu zaidi kwani anatambua kuwa Tanzania kuna vivutio vingi kama fukwe za bahari, mbuga za wanyama na vingine vingi na akaongeza kuwa shirika lake lina uzoefu wa biashara ya utalii kwani lina kampuni zinazofanya kazi ndani ya China na Hong Kong. “Tunaweza kusaidia kuwaleta Wachina waje kutalii Tanzania,” alisema Bw. Chen na kusisitiza kuwa wataangalia katika kuwekeza kwenye hoteli karibu na hifadhi za taifa.
Hainan ni moja ya mashirika makubwa ya ndege duniani. Ina ndege 470 na imeajiri wafanyakazi wapatao 1,000. Shirika hilo pia lina hoteli 500 za kitalii duniani na lina viwanja vya ndege vipatavyo 16 vikiwemo vitatu vya kimataifa.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu alimweleza mwenyekiti huyo kuwa Tanzania inafanya juhudi za kujikomboa kiuchumi; lakini bado inahitaji msaada wa China hasa katika masuala ya usafiri wa anga ili iweze kupiga hatua kutoka hapo ilipo.
Alisema Tanzania kuna shirika la ndege lakini liko taabani licha ya kuwa lina njia nyingi na akatumia muda huo kumwomba mwenyekiti huyo wa Hainan kufikiria pia namna ya kuweza kufufua ATC ili iweze kufanya kazi pamoja na Hainan.
“Ndio maana tunawakaribisha nyinyi Hainan ni shirika kubwa ambalo naamini linaweza kuisaidia Tanzania katika eneo hilo la usafiri wa anga ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kufanya safari za moja kwa moja hadi Tanzania; lakini pia na kuangalia namna ya kulifufua shirika la ndege la Tanzania (ATC),” alisema Waziri Mkuu.
Alimwomba Bw. Chen aangalie uwezekano kuja kujenga hoteli za kitalii karibu na viwanja vya ndege. “Iweje hoteli za utalii katika nchi yetu zijengwe na wafanyabiashara wa nchi za magharibi tu wakati na nyinyi mna uwezo wa kufanya vizuri zaidi hata kuliko wao? Alihoji.
NA MICHUZI MATUKIO BLOG
0 comments:
Post a Comment