SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Tuesday, September 24, 2013

SHAMBULIO LA KIGAIDI NCHINI KENYA

Baadhi ya wanausalama wakiwa nje ya jengo la Westgate jijini Nairobi.
  • Mateka wote wadaiwa kuokolewa
  • Vikosi vya usalama vinakamilisha zoezi la kudhibiti jengo zima la Westgate
  • Idadi ya magaidi waliouawa ni sita
  • Milio ya risasi ilisikika leo asubuhi, mchana kutoka ndani ya jengo
TAARIFA kutoka serikali ya Kenya zinadai kuwa mateka wote waliokuwa wanashikiliwa na magaidi katika jengo la Westgate wameokolewa.
Vikosi vya usalama nchini humo vinadai kuwa viko katika hatua za mwisho kukamilisha zoezi la kudhibiti jengo zima la Westgate. Magaidi wapatao sita wanadaiwa kuuawa usiku wa kuamkia leo.
Lakini taaria kutoka shirika la AFP zinadai kuwa majeshi ya Kenya yangali yanakabiliana na baadhi ya magaidi ambao wamesalia ndani ya jengo la hilo.
Inadaiwa kuwa magaidi hao walijitawanya ndani ya jengo hilo kila mmoja akijificha sehemu yake katika ghorofa ya juu za jengo hilo.
Katika shambulio hilo lililotokea Jumamosi iliyopita, watu 62 wanadaiwa kupoteza maisha wakati 175 wakijeruhiwa japo kuna taarifa kuwa idadi ya waliokufa ni 69 mpaka sasa. Katika shambulio hilo, mwanamke Samantha Lewthwaite anadaiwa kuwa miongoni mwa magaidi 10-15 waliohusika.

CHANZO- GPL



 
 Vikosi vya Kenya 'vimedhibiti' Westgate

Hatimaye vikosi vya usalama nchini Kenya vinasema vimelidhibiti jengo zima la Westgate mjini Nairobi, ikiwa ni zaidi ya siku tatu baada ya jengo hilo kuvamiwa na wanamgambo.
Milipuko ikifuatiwa na milio ya risasi imesikika kutoka ndani ya jengo hilo asubuhi ya leo huku duru zikisema kuwa vikosi vya usalama vinaelekea kukamilisha operesheni hiyo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, magaidi sita waliokuwa wamesalia wameuawa huku wengine watatu wakiuawa hapo jana.
Serikali imesema zaidi ya watu 60 wameuawa na wengine zaidi ya 170 kujeruhiwa katika shambulio hilo ambalo Al shabaab imekiri kulitekeleza.
Wizara ya mambo ya ndani imesema wanajeshi wanaendelea kulisaka jengo zima la Westgate kutoka orofa moja hadi nyengine kuhakikisha kwamba hakuna mateka aliyesalia
Wakati huohuo, waziri wa mambo ya nje amesema kuwa wawili kati ya wanamgambo watatu waliofanya shambulii hilo ni raia wa Marekani pamoja na mwanamke muingereza.
Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni nchini Marekani, Amina Mohamed alisema kuwa wamarekani walikuwa kati ya umri wa miaka 18 na 19 ingawa wenye asili ya kisomali au kiarabu na waliishi mjini Minnesota. Mshukiwa mwingine alikuwa mwanamnke Muingereza ambaye inasemekana alikuwa amefanya vitendo vingi vya aina hii kwa niaba ya Al Shabaab.
Shirika la Red Cross limeambia BBC kuwa watu 63 wangali hawajulikani waliko.
Wanajeshi wa Kenya katika juhudi za kuokoa mateka na kukomboa jengo la Westgate
Haijulikani idadi ya wanamgambo waliokuwa ndani ya jengo hilo , lakini maafisa wa usalama wamesema kuwa wanamgambo watatu wameuawa.
Kundi la kigaidi la al-Shabab limekiri kutekeleza mauaji hayo, kulipiza kisasi hatua ya Kenya kujihusisha kijeshi nchini Somalia.
Operesheni hiyo iliendelea usiku kucha ingawa kwa mujibu wa waziri wa usalama wa Kenya, ilikuwa katika mkondo wake wa mwisho.
"magaidi hawa huenda wanakimbia na kujificha katika sehemu mbali mbali za jengo hilo lakini ghorofa zote za jengo hilo zimedhibitiwa na majeshi,'' alisema Ole Lenku
Aliongeza kuwa mateka wote walifanikiwa kuokolewa.
Jumatatu jioni moshi mkubwa ulionekana ukifuka kutoka kwenye jengo la Westgate ukiambatana na moto mkubwa. Moto huo unasemekana uliwashwa na wanamgambo hao ili kutatiza vikosi vya usalama katika juhudi zao za kutaka kukomboa jengo hilo.
 CHANZO- BBC SWAHILI

0 comments:

Post a Comment