Na Zitto Kabwe
Kwa takribani wiki tatu sasa kumekuwa na
sintofahamu kuhusu muswada wa sheria uliopitishwa na Bunge ili kufanya
marekebisho ya sheria ya marekebisho ya Katiba ya mwaka 2011. Mjadala na
upitishaji wa sheria hii uliweka rekodi ya pekee katika nchi yetu kwa vitendo
vya kihuni kutokea Bungeni ambavyo nisingependa kuvirejea kutokana na aibu
kubwa ambayo Bunge liliingia.
Kiukweli kuna sintofahamu katika nchi kuhusu
kuandikwa kwa Katiba mpya. Hii imechangiwa na kurushiana maneno miongoni mwa
wanasiasa wa pande zote mbili, wanaopinga muswada ulivyo na wanaounga mkono
muswada ulivyo. Masuala ya Tume imalize kazi yake lini, ushiriki wa Zanzibar na
idadi ya wajumbe kutoka Zanzibar kwenye Bunge la Katiba, Wajumbe wa Bunge
Maalumu wanapatikanaje na kadhalika ni masuala ambayo yanaweza kupatiwa mwafaka
kwa viongozi kukaa na kuzungumza. Haya sio masuala ya kushindwa kujenga mwafaka
labda kuwe na nia mbaya dhidi ya mchakato wa kuandika Katiba mpya. Katiba sio
suala la kufanyia siasa. Katiba ni uhai wa Taifa.
Ni wazi kuna kundi kubwa ambalo halijitokezi
waziwazi ambalo lingependa pasiwe na katiba mpya ya Wananchi. Kuna kundi
lingine ambalo lingependa mchakato wa kuandika Katiba uendelee kwa miaka
mingine zaidi ili kuweza kupata Katiba bora. Kuna kundi la Wabunge ambao kwa
chinichini wanataka mchakato uendelee, uchaguzi uahirishwe mpaka mwaka 2017 na
wao waendelee kuwa wabunge.
Naamini watu hawa wanaota ndoto za mchana
kwani hakuna mahusiano yeyote kati ya uchaguzi mkuu na kuandika katiba mpya.
Kama Bunge hili la sasa na Serikali hii itashindwa kukamilisha zoezi hili,
Bunge linalokuja na Serikali itakayoingia madarakani itaendelea nalo.
Hivyo sio lazima kupata Katiba mpya kabla ya
uchaguzi mkuu wa 2015. CHADEMA imependekeza kuwepo na marekebisho ya mpito
kwenye Katiba ya sasa ili kuwezesha Tume huru ya Uchaguzi, masuala ya wagombea
binafsi na kadhalika. Vyama vingine vya siasa vinaweza kuwa na mapendekezo yao
ya mpito na hivyo kutoa nafasi ya kutosha kabisa wa kuandika Katiba makini.
Changamoto kubwa sana ya siasa za Tanzania ni
kelele. Wanasiasa hatuzungumzi kwenye masuala yanayohusu uhai wa Taifa. Kila
chama kinakuwa na misimamo yake na kuishikilia na hatimaye kujikuta tunapoteza
fursa ya kuzungumza na kujadiliana kama Watanzania. Mwaka 2011 hali ilikuwa
hivi hivi mpaka kundi la Wazee viongozi wastaafu walipoingilia kati na
kupelekea wanasiasa kukaa na kuzungumza.
Bahati mbaya sana viongozi wale ndio sasa
wamepewa usukani wa kuandika Katiba kwa kuwa kwenye Tume. Hawawezi tena kufanya
kazi ile ya kutafuta suluhu iliyopelekea Rais kuzungumza na viongozi wa vyama
vyote vya siasa ikulu jijini Dar es Salaam.
Vyama vya Upinzani nchini sasa vimeungana
kupinga muswada wa marekebisho ya Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya mwaka
2011. Waziri wa Sheria na Katiba, Waziri wa Nchi ofisi ya Rais mahusiano na
Uratibu, viongozi waandamizi wa CCM wote nao wameungana kuunga mkono muswada
kama ulivyo. Badala ya kutafuta mwafaka, kumekuwa na kurushiana maneno ya
kejeli na kadhalika.
Taifa halijengwi namna hii. Taifa linajengwa
kwa mwafaka na Katiba ni moja ya nyenzo wa Mwafaka wa Taifa. Niliwahi kuandika
huko nyuma kuwa Katiba haiandikwi barabarani bali huandikwa mezani kwa watu
kukaa na kukubaliana masuala ya Taifa dhidi ya maslahi ya kivyama ya wanasiasa.
Hakuna kilichoharibika. Bado tunayo nafasi
kama Taifa kukaa na kukubaliana. Kwa hali ya sasa nafasi hii ipo mikononi mwa
Mkuu wa Nchi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais ana wajibu wa
kikatiba wa kuhakikisha umoja wa kitaifa unaendelea kuongoza mchakato huu wa
katiba ya nchi yetu.
Hata hivyo ni vizuri kutahadharisha kuwa sio
sahihi kwa wanasiasa wa pande zote kujaribu kumlazimisha Rais kuridhia ama
kutoridhia sheria hiyo. Si sawa kisiasa kwa wanasiasa wa upinzani kujaribu
kumlazimisha Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama chenye wabunge wengi
bungeni kwenda tofauti na wabunge wake na wakati huohuo ni utovu wa nidhamu kwa
Waziri wa Sheria kujaribu kumshauri hadharani Rais wake kuridhia sheria hiyo
kwani ni kinyume cha misingi ya uongozi na pia kinatafsirika kama kumshurutisha
(blackmail) Rais wake.
Kutosaini muswada huu kunaweza kuleta mgongano
kati ya Wabunge wa CCM na Rais. Hata hivyo Rais lazima aweze kushawishi chama
chake kwamba umoja wa kitaifa ni muhimu ziadi kuliko maslahi ya kisiasa ya
chama chao. Pia kikatiba Rais anasaini miswada kuwa sheria akiwa Mkuu wa Nchi
na sio Mkuu wa Serikali ya Jamhuri. Akiwa Mkuu wa Nchi maslahi mapana ni kuweka
mwafaka wa pamoja miongoni mwa wananchi.
Rais Jakaya Kikwete anapaswa kutumia mamlaka
yake kama Mkuu wa Nchi kuiweka nchi pamoja kwa kuurejesha muswada bungeni ili
uweze kujadiliwa upya na wadau wote na kupitishwa tena na Bunge. Ibara ya 97 ya
Katiba ya sasa imeweka masharti ya utaratibu wa kutunga sheria na iwapo Rais
ataurudisha muswada huu Bungeni pamoja na maelezo ya hatua hii, upitishwaji
wake utahitaji theluthi mbili ya wabunge wote. Hii itakuwa hatua muhimu sana
katika historia ya demokrasia yetu. Rais afuate ushauri huu kwani una manufaa
makubwa.
CHANZO: NA MICHUZI MATUKIO BLOG
0 comments:
Post a Comment