SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Friday, November 2, 2012

NENO LA LEO: SI KILA AVAAE KANZU NA BARAGHASHEA APEWE KUKU ACHINJE!

Ndugu zangu, 
Hutokea kwa mwenye kuku kusubiri amwone anayepita akiwa na kanzu na baraghashea ili amwombe amchinjie kuku wake. Ni kuepuka kula haramu. Lakini, anachoshindwa kuelewa mwanadamu huyu, ni ukweli, kuwa si kila anayevaa kanzu na baragheshea anaweza kupewa kuku amchinje. Kwa wengine ni fasheni tu.
Vivyo hivyo, si kila avaae Rozari na msalaba shingoni anaweza kupewa biblia aendeshe ibada. Wengine ni fasheni tu. Na si kila avaae jezi ya Yanga anaweza kuulizwa ' uganga' wa kuisaidia Yanga. 
Mwingine atasema; anayevaa jezi ya Yanga anaipenda Yanga. Hapana, mimi nikivaa jezi ya Yanga ni utani tu, na si kitu kingine. Nimeipenda Simba sports hata kabla sijafikisha miaka saba, ni pale Ilala, Dar es Salaam. Na je, umewahi kujiuliza; kuwa ni lini ulianza kuwa mpenzi wa timu unayoipenda, na kwa nini?
Mimi ilikuwa ni mwaka 1975, kwenye Uwanja wa Karume. Simba vs Cosmo Politans, zote za Ilala. Ilikuwa ni mechi yangu ya kwanza kuiona tangu nizaliwe. Cosmo walivaa bluu na Simba walivaa nyekundu na nyeupe. Rangi za Simba zilinivutia sana. Na uchezaji wa Simba na hususan winga Willy Mwaijibe ulinivutia sana. Simba ilishinda 2-1. Na tangu siku hiyo nikawa mpenzi wa Simba Sports Club!
Na kitabu changu cha kwanza kukinunua kwa pesa zangu nilizozichanga kwenye kopo ni cha mwandishi Hadji Konde; Utani wa Simba na Yanga. Picha ya mbele kitabuni ilikuwa ni ya Abdalah Kibaden na Sunday Manara wakiwania mpira. 
Naamini, kuwa hakuna Yanga bila Simba, na kinyume chake. Simba na Yanga ni sehemu ya historia yetu. Ni utambulisho wetu pia kama Taifa. 
Leo niliingia Maktaba ya Mkoa hapa Morogoro. Nikakiulizia kitabu cha Hadji Konde cha Utani wa Simba na Yanga. Mkutubi ananiambia; " Sijapata kumsikia mwandishi huyo, na wala sijakisikia kitabu hicho!". Naam, ndipo tulipo. Hata kumbukumbu za kimaandishi za historia ya mpira wetu nazo zimepotea. Tumeishia kununua jezi za timu zetu mitaani. 
Mimi ninayo ya Simba, na ya watani zetu Yanga. Hiyo ya Yanga ni maalum kwa siku ninazoamua kuwatania, kama hii leo! Naam, Yanga Imara! (Sijui nani amewadanganya wakati kila siku ugomvi haushi klabuni kwao!)


Maagid Mjengwa, 

Morogoro. 

0 comments:

Post a Comment