SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Tuesday, August 28, 2012

WALIOJIFANYA POLISI WAMTEKA MTU BAA

Stori: Makongoro Oging'
MKAZI wa Yombo Buza Wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam, Fredy Galus, 24, (pichani)ameokolewa na wananchi baada ya kutekwa katika baa iitwayo Cape Town wakati akizungumza na wenzake.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Jumapili Agosti 5, mwaka huu saa 9 alasiri ambapo inadaiwa watu hao wawili walijifanya askari polisi waliomchukua kijana huyo na kumweka katika gari na kuondoka naye kusikojulikana.
Galus anasimulia mkasa mzima ulivyompata kama ifuatavyo:
“Nakumbuka siku hiyo tulikaa na shemeji aitwaye Denis Eliasaph na watu wengine wawili, jumla tulikuwa wanne, tulikuwa tukibadilishana mawazo.
“Huku tukiendelea na maongezi ghafla walifika watu wawili waliojitambulisha kuwa ni polisi, hawakuonyesha hata vitambulisho, mmoja alinikwida na kutoka nami nje ya baa hiyo na kuniingiza katika gari na kuondoka.
“Niliwauliza majina lakini hawakunieleza majina wala kituo chao cha polisi wanachotoka. Waliniweka katika kiti cha nyuma huku dereva akiendesha gari kwa kasi, niliamua kupiga kelele huku nikijirusha.
“Dereva wa pikipiki tuliyempita njiani aliniona ndani ninavyohangaika huku nikipiga kelele, aliendesha pikipiki kwa kasi huku kwa mbele alimweleza dereva wa gari lingine ili aweze kuzuia gari lililonichukua, ambapo alifanya hivyo.
“Mle ndani ya gari walikuwa wakinipiga sehemu mbalimbali za mwili huku mmoja akimwambia mwenzake atoe kamba ili wanifunge mikono na miguu.
“Mara baada ya gari lao kuzuiwa maeneo ya Tandika kwa Rulenge, wananchi waliokuwa maeneo hayo walilizingira gari na nilichomoka na baada ya muda mfupi alifika askari polisi wa Kituo cha Makangarawe.
“Walipoulizwa vitambulisho vyao ili kuthibitisha ni askari kweli, hawakuonyesha. Wananchi pamoja na yule polisi waliwakamata na kuwapeleka Kituo cha Polisi cha Makangarawe.
“Kule kituoni polisi waliwabana na maswali ndipo waliamua kubadilisha usemi wakasema eti ninatembea na mke wao wakati ukweli ni kwamba siwajui na wala sijawahi kuwaona.
“Nafikiri walikuwa na nia mbaya nami inawezekana walitaka kuniua kwani walininyang’anya simu yenye thamani ya shilingi 320,000 na fedha shilingi 670,000, suala lilifikishwa Kituo cha Polisi Chang’ombe.
“Pale polisi watuhumiwa wameachiwa na wameondoka na gari lao, licha ya kufunguliwa jalada la kesi namba CHA/RB/6946 /2012.”
Naye mhudumu wa baa ya Cape Town aliyejitambulisha kwa jina la Charles Rite, alipohojiwa juu ya suala hilo alisema kuwa watu hao walifika hapo kwa kujitambulisha kuwa wao ni polisi na walimhitaji huyo kijana, hivyo wakaondoka naye .
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, David Misiime, alipoulizwa alisema watu hao hawakuwa polisi na wanaendelea kupepelezwa.
CHANZO: HIKI HAPA

0 comments:

Post a Comment