Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Serikali ya Mapinduzi ya zanzibar (SMZ), Ali Juma Shamuhuna.
Na GPL Ripota - ZanzibarBAADHI wa walimu wa ngazi mbali mbali kisiwani Pemba wamekuwa wakilalamikia kitendo cha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar (WEMA) kuwakata mishahara yao kwa zaidi ya asilimia 30 hadi 50 bila kuwepo kwa ufafanuzi au maelezo kamili juu ya makato hayo.
Hali hii ambayo kwa sasa imekuwa kero kubwa kwa watumishi hawa wa serikali imekuwa ikiwakumba walimu wa wilaya zote nne kisiwan hapa tangu mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu.
Walimu kadhaa wa shule za msingi na sekondari wa wilaya ya Micheweni, ambao wanaonekana kuguswa na kuathiriwa zaidi na kadhia hii wametuma malalamiko yao kwa mwandishi wa habari hizi huku wakiwa wenye kukata tamaa ya msaada juu ya kadhia hii.
“Kwa hali hii ni bora niache kazi nijue kuwa si mtumishi wa serikali kuliko kudhulumuiwa kiasi hiki,” alisema mwalimu mmoja wa shule ya msingi Mtemani ambae hakutaka jina lake litajwe.
Malalamiko kadhaa yamekuwa yakipelekwa Wizara ya Elimu Pemba kupitia kitengo chake cha utumishi ambapo walimu hao wamedai kuwa hakuna lolote la kushika zaidi ya kukatishwa tamaa.
Wakati huohuo, mwalimu mwengine wa wilaya ya Micheweni alinukuliwa akisema: “Hii ni mara ya pili kukatwa mshahara wangu kwa zaidi ya asilimia 30 isivyo halali. Nilipofuatilia utumishi walikiri kuwepo kwa tataizo hili na kuahidi kulifanyia kazi, lakini mwezi huu pia nimekatwa zaidi ya fedha za mwezi uliopita bila kurejeshewa makato yangu ya awali ya mwezi uliopita. Hii inakatisha tamaa kweli.”
Mwandishi wa habari hizi alizungumza na Afisa wa Elimu Wilaya ya Micheweni, Maalim Mbwana Shaame Hamad, ambapo ofisa huyo alikiri kuwepo kwa uzembe na mapungufu makubwa katika kitengo cha utumishi cha Wizara ya Elimu hapa Zanzibar.
“ Ni kweli kabisa kuwa watu wa utumishi wa Wizara ya Elimu wanafanya makato yasiyo halali katika mishahara ya walimu hasa hapa kisiwani Pemba. Cha kushangaza tunapofuatilia hawatupi majibu mazuri, majibu yao yanakuwa ya mkato na ya kifedhulifedhuli tu. Hayasaidii kabisa,” alisema ofisa huyo.
Katika fuatilia fuatilia yetu, pia mwandishi wa habari hizi alimhoji Afisa wa Elimu huyo sababu hasa zilizopelekea makato hayo naye alijibu:
“‘Wanadai kwamba kuna walimu ambao wamekuwa wakilipwa mishahara isiyostahiki viwango vyao vya kitaaluma na walitakiwa wapeleke ithibati ya vyeti kuthibitisha hilo. Cha kushangaza walimu wote hao waliokatwa mishahara wamepeleka ithibati hizo lakini bado kadhia hii inaendelea. Hii inashangaza sana.”
Kuna taarifa kuwa walimu kadhaa wa shule ya msingi Wingwi Mtemani wamekatwa viwango vikubwa vya mishahara tangu mwezi Julai. Kadhia hii pia imejitokeza kwa kiasi kikubwa katika shule ya msingi Wingwi A na B na pia Wingwi Sekondari.
Mwandishi wa habari hizi amefanikiwa kuorodhesha majina kadhaa ya walimu wa shule ya msingi Mtemani Wingwi ambao wamekuwa ni waathirika wakubwa wa kadhia hii. Katika fuatilia yetu tumefanikiwa kupata orodha fupi ya majina ya walimu na viwango vyao vya makato waliyokatwa katika mishahara yao. Ieleweke kuwa mishahara halisi ya walimu hawa ni kati ya laki moja hadi mbili za Kitanzania.
Orodha ya walimu wa shule ya msingi Mtemani na makato yao ni kama ifuatayo:
Bi Salma Haji amekatwa 55,000/- Julai na Agosti
Bi Maryam Juma -37,000/- Julai na Agosti
Bi Aminia Hamad -37,000/- Julai na Agosti
Bi Hadia Saidi -37,000/- Julai na Agosti
Bw. Ameir Ali- 37,000/- Julai na Agosti
Bw. Aminia Nassor – 60,000/- Julai na Agosti
Bw. Nassor Abdalla- 30,000/- Julai na Agosti.
Bi Maryam Nassor- 37,000/- Julai tu.
NB: Katika kutaka kufahamu ukweli wa jambo hili, mtandao huu ulifanya juhudi za kuwasiliana kwa njia ya simu na Afisa Mdhamini Elimu Pemba, ilikupata kauli yake pia, lakini haikuwezekana kumpata.
Hata hivyo, juhudi za kupata maelezo yake zinaendelea.
CHANZO: BOFYA
0 comments:
Post a Comment