Mkufunzi Emmanuel Mageni (kushoto) akikabidhi msaada wa mifuko 10 ya saruji kuchangia ujenzi kituo cha afya katika Kata ya Hungumalwa wilayani Kwimba. (Na Mpiga Picha wetu).
Na. Mwandishi wetu, Kwimba
Matumaini ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Hungumalwa wilayani Kwimba, Mwanza, yameongezeka baada ya Mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Murutunguru wilayani Ukerewe, Emmanuel Mageni, kuchangia mifuko 10 ya saruji.
Mageni alikabidhi mchango wake huo kwa uongozi wa kata hiyo jana, ikiwa ni miezi minne tangu alipotoa ahadi ya kusaidia ujenzi huo katika harambee iliyoongozwa na aliyekuwa Mkuu wa wilaya hiyo, Christopher Kangoye.
Mageni, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), alitoa msaada huo baada ya kuguswa na ukubwa wa tatizo la ukosefu wa huduma za afya za kitaalamu linaowakabili wakazi wa kata hiyo kwa muda mrefu.
Akikabidhi msaada huo jana, Mageni alitumia fursa hiyo kumpongeza Diwani wa Kata ya Hungumalwa, Shija Malando, kwa kubuni na kuhamasisha ujenzi wa kituo hicho cha afya huku akimhimiza kuongeza juhudi zaidi katika kushughulikia maendeleo ya wananchi.
“Ninakupongeza (Malando) kutokana na juhudi kubwa unazofanya katika kutafuta maendeleo ya wakazi wa Kata ya Hungumalwa, matumaini yangu ni kwamba wananchi wataendelea kukuunga mkono katika jitihada za kujiletea maendeleo,” alisema Mageni.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa kituo hicho cha afya, John Nkumba, alisema ujenzi huo ulianza mwaka jana kutokana na michango mbalimbali ya wananchi, ambapo kwa sasa umefikia hatua ya linta ukiwa umekwisha kugharimu zaidi ya sh. milioni 10.
Ujenzi wa kituo hicho unatarajiwa kuwaondolea wakazi 14,168 matatizo ya vifo visivyo vya lazima, wajawazito kujifungulia njiani na adha ya kutembea umbali wa kilomita 40 kwenda kutafuta matibabu wilayani Misungwi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Hungumalwa, Maneno Shaban, alimshukuru Mageni kwa kutekeleza ahadi hiyo akisema ni mfano mzuri unaopaswa kuigwa na wengine katika kuchangia maendeleo ya jamii.
Aidha, alimwomba Mageni kutosita kurudi katani hapo kujionea maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha afya pamoja na huduma za afya zitakazokuwa zinatolewa baada ya ujenzi huo kukamilika.
CREDIT TO DEWJI BLOG
0 comments:
Post a Comment