Ni Mv.Skagit iliyozama Chumbe
25 wafariki,
145 waokolewa.
Zoezi la uokozi lasitishwa, bahari yachafuka
Dk. Shein afika Bandarini kuangalia hali
Na Waandishi wetu
IKIWA ni miezi 10 tangu Zanzibar ikumbwe na ajali mbaya ya kuzama kwa Mv. Spice Islander I, tukio jengine linalofanana na hilo limejirejea tena jana kwa kuzama meli ya Mv. Skagit ambapo idadi kamili ya waliokufa bado haijajulikana.
Hadi zoezi la uokozi linasitishwa jioni ya jana kutokana na giza na bahari kuchafuka, watu 25 wakiwemo Watanzania 24 na raia mmoja wa kigeni walithibitika kufariki na 145 kuokolewa wakiwa hai.
Meli hiyo ilizama kwa kubiruka chini juu, ilikuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea katika banadari ya Malindi iliyopo mjini hapa, ambapo taarifa zinaeleza
kuwa ilikuwa na watu 290, abiria 250 na watoto 31, pamoja na wafanyakazi wa meli tisa.
Majeruhi waliookolewa walikimbizwa katika hospitali kuu ya Mnazimmoja kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kwanza na matibabu.
Maiti walioopolewa kwenye ajali hiyo, walifikishwa katika viwanja vya Maisara kwa ajili ya kutambuliwa na ndugu na jamaa zao, ambao walifurika katika viwanja hivyo.
Majeruhi waliookolewa katika ajali hiyo walibebwa katika vyombo vilivyotengwa kwa ajili ya uokozi na kufikishwa katika hospitali ya Mnazimmoja kwa ajili ya kupatiwa huduma za matibabu.
Waandishi wetu waliokuwa katika eneo la uokozi baharini nje kidogo ya kisiwa cha Chumbe, walisema zoezi hilo lilikabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo uchache wa waokozi, ambapo wale waliokuwa wakifanyakazi hiyo walichoka haraka kutokana na kuelemewa na kazi hiyo.
Waokozi hao ambao wengi wao kutoka Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) na vikosi vya ulinzi na usalama, walifanyakazi hiyo katika mazingira magumu kutokana na kuchafuka kwa bahari kutokana na upepo mkali.
Aidha majeruhi waliookolewa ilishindikana kupatiwa huduma za mwanzo za haraka kutokana na kutokuwepo kwa madaktari na umbali wa eneo la tukio hadi hospitali ya Mnazimmoja.
Katika zoezi hilo kulikuwa na wafanyakazi kidogo wa ‘Red Cross’, ambao nao walilazimika kuchoka sio tu kutokana na kazi kubwa lakini hali mbaya ya bahari.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alifika katika Bandari ya Malindi kuangalia zoezi zima la uokozi.
Itakumbukwa kuwa Septemba 10 mwaka jana mamia ya wananchi waliokuwa wakisafiria meli ya Mv. Spice Islander I iliyokuwa imebeba abiria na mizigo ilizama katika mkondo wa Nungwi.
Katika siku za hivi karibuni hali ya usafiri wa bahari imekuwa ikiwatia hofu wananchi hasa ikikumbukwa kuwa meli moja ya usafiri iliyokuwa ikitokea Pemba ilipotea hadi kukaribia Tanga.
Kufuatia janga hilo, Baraza la Wawakilishi linaloendelea na kikao chake limesitisha kuendelea na mkutano wake, huku Wabunge wa Zanzibar walioko Bungeni walilazimika kutoka nje ya mkutano huku mjadala ukiendelea.
Baadhi ya mawaziri walioshiriki katika eneo la uokozi ni pamoja na Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud Mohammed, Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakary, pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Majimbo mbali mbali.
Akizungumza baada ya kurejea bandari ya Malindi, Waziri Masoud alipongeza juhudi zilizochukuliwa na boti mbali mbali za abiria na wavuvi, na zile za KMKM, Polisi na Shirika la Bandari, pamoja na helikopta ya Polisi kwa juhudi kubwa walizochukua kusaidia uokozi wa watu hao.
na OTHMAN MAPARA BLOG
0 comments:
Post a Comment