SERIKALI ya Zanzibar imekiri kuwapo kwa upendeleo na kujuana katika suala la ajira kwenye wizara mbali mbali za serikali jambo linalolazimu kufanyia marekebisho sheria zake za utumishi.
Hayo yameelezwa na Mwanasheria Mkuu wa serikali, Othman Masoud Othman alipokuwa akifanya majumuisho na kujibu masuala mbali mbali katika muswada wa sheria mbali mbali na mambo yanayohusiana na hayo katika Kikao cha Baraza la Wawakilishi jana.
“Hoja ya uajiri ni kweli hilo hatuwezi kukataa kwa kweli mfumo wa utumishi ni mfumo tuliotoka nao huko nyuma, wapo wanaobadilisha vyeti ikiwa umri wao umepita, wapo wanaoajiriwa kwa urafiki na ukaribu hilo hatuwezi kulikataa yalikuwapo huko nyuma kabla ya sheria hii lakini ndio tunasema hivi sasa tunajipanga katika hilo kuondosha malalamiko hayo” alisema Mwanasheria Mkuu.
Kauli hiyo ya serikali imekuja kufuatia baadhi ya wajumbe hao kulalamikia mfumo uliopo waliosema, wapo baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakipata ajira kutokana na kujuana huku watendaji wenye kufanya hivyo katika chombo cha utumishi kinachotegemewa na wananchi kutoa ajira kikiwa kinakiuka misingi ya haki na uadilifu.
Mwakilishi wa Jimbo la Wete (CUF), Asaa Othman Hamad alisema katika wizara nyingi kumekuwapo na mkanyagano mkubwa ambao mara nyingi wanaofanya hivyo ni wale wafanyakazi wasio na ufanisi wa kazi lakini pia ajira zimekuwa zikitolewa kwa ubinafsi bila ya kuzingatia sifa zinazostahiki.
“Tunachukua watumishi wa umma na kuwapa mikataba ya kazi ya muda tu, serikali inawafundisha vijana na kuwasomesha lakini wanashindwa kufanya kazi hapa kutokana na sheria za utumishi zilivyo” alisema.
Alisema ipo haja ya kufanywa tathmini ya kila mwaka kwani watendaji na wafanyakazi wamekuwa wakitekeleza majukumu yao isivyo sahihi ambapo wapo walioajiriwa bila ya sifa na kutaja vitendo vya ubadhirifu wa fedha za umma ukifanyika chini ya kivuli cha wafanyakazi hewa.
“Kuna matatizo katika sekta hii ya utumishi wa umma, wapo watu wanataka kuajiriwa wenye sifa lakini badala yake wanachukuliwa wengine na kuachwa wenye sifa. Mheshimiwa Spika Wafanyakazi hewa wapo kila siku lakini wanaonekana upande mmoja tu, Pemba ndio inayoonekana kuwa kuna wafanyakazi hewa lakini hapa Unguja wapo lakini hilo halifanyiwi uchunguzi” alisema Asaa.
Naye Mwakilishi wa Ziwani (CUF), Rashid Seif Suleiman alisema kwa mujibu wa katiba ya Kamisheni ya Utumishi ndio chombo kikuu lakini inaonesha kwamba serikali inarudi tena katika utawala wa mtu binafsi na mwingine ambao mamlaka anapewa Katibu Mkuu Kiongozi, hivyo alishauri uamuzi utokane na chombo badala ya mtu mmoja.
“Wizara ya utumishi na utawala bora utafanya kazi gani ikiwa uamuzi kama huo anapewa katibu mkuu kiongozi, kwa kuwa yeye ni kiongozi basi ni bora akaendelea kuwa kiongozi wa wizara zote lakini kumuweka katika wizara moja tu ni kumuongezea msongamano” alisema mwakilishi huyo.
“Nashauri utafiti mkubwa ufanyike kuhusiana na utumishi wa umma kwani ubinafsi umetawala, umimi unatawala na ni bora kufanya uchunguzi mapema kuliko kusikia kuna ajira zimetolewa, tunataka maendeleo lakini bado tunaendelea kutoa ajira kwa upendeleo tu utasikia anatakiwa mtu mwenye shahada lakini wanachukuliwa mtu mwenye diploma wakati wenye shahada wapo mitaani” alisisitiza.
Aidha alisema kuna haja ya kutathimiwa kwa wafanyakazi kila mwaka, pamoja na Wakurugenzi, Makatibu Wakuu na hata Mawaziri wanaoteuliwa watizamwe kutokana na viwango vyao vinavyokubalika.
“Rais anatizama kusini sijachukua anateuliwa mmoja kaskazini sijateuwa anachukua mmoja na hachagui kwa kiwango na vigezo mpaka lini tutatumia utaratibu huo bila ya kuzingatia utumishi wa umma” alihoji mwakilishi huyo.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Micheweni (CUF) Subeit Khamis Faki alisema , serikali iwaache wastaafu na iwape fursa vijana maana kuwarudisha wastaafu ni kuwanyima fursa vijana kufanya kazi hasa kwa kuzingatia serikali inao vijana wengi wenye elimu na waliosoma katika fani mbali mbali.Aidha Mwakilishi huyo ameitaka serikali kuwa makini katika suala zima la kutoa ajiri ya mikataba kutokana na hali hiyo kuwakosesha vijana wenye uwezo kupata ajira.
Alisema wapo baadhi ya wastaafu ambao wanapewa mikataba ya kazi wakati utendaji wao hauna rekodi nzuri huko nyuma lakini pia kufanya hivyo ni kuwakosesha vijana kupata ajira serikalini na kuzalisha wafanyakazi wavuvi.
Alisema sheria nyingi zinatungwa lakini haziwasaidii waajiri na kumekuwa na ujanja wa wamiliki wa mahoteli wanawafukuza wafanyakazi bila ya sababu za msingi kutokana na marekebisho ya sheria ile ya mishahara kwa wafanyakazi.
Aliomba Serikali kuchukua hatua za kisheria kama zinavyozitungwa barazani hasa kwa hao wamiliki wa mahoteli ambao wanaofanya vitendo hivyo, sheria zifanye kazi na zisimamiwe kikamilifu kama zinavyotungwa maana kutungwa kwa sheria ni kuzifanyia kazi kwa ukamilifu.
source: Gazeti la Mwananchi
0 comments:
Post a Comment