SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Friday, March 9, 2012

Uporaji Nje Nje Dar es Salaam!!

Mfanyabiashara ndogo akimuokoa mkazi wa Dar es Salaam, Charles Maina ambaye ni dereva wa kampuni ya Superdoll kutoka mikononi mwa vijana wanaodaiwa kuwa ni vibaka baada ya jaribio lao la kutaka kumpora mali zake kushindikana kama ilivyokutwa katika taa za kuongozea magari makutano ya barabara ya Nyerere na Kawawa.
 (Picha na Fadhili Akida).
****
MKAZI wa Dar es Salaam ambaye ni dereva wa Kampuni ya Superdoll, amenusurika kuuawa kutokana na kipigo cha baadhi ya vijana wa jijini humo, kwa madai ya kugonga mtu na kukimbia.
Charles Maina alinusurika katika tukio lilitokea juzi kwenye makutano ya barabara za Nyerere na Kawawa baada ya vijana hao wanaokadiriwa kuwa saba wengi wao wakidaiwa kuwa vibaka, kuzingira gari lake, kumshusha na kumshambulia huku wakimpekua mifukoni kutaka kumwibia mali zake.
Tukio hilo ambalo lilikusanya watu lilionekana kama sinema baada ya vijana hao kumshusha kutoka katika gari alilokuwa akiendesha mali ya kampuni hiyo na kumburuta wakimvusha ng’ambo ya barabara wakiendelea kumpiga. Vijana hao walisikika wakimwambia: “Umeua halafu unataka kukimbia, leo utaipata.”
Hata hivyo, Maina alijitahidi kupambana nao huku akipiga kelele za kuomba msaada kwa wapitanjia lakini hakuna aliyekuwa tayari kumsaidia.
Walipomdhibiti walionekana kuingiza mikono kwenye mifuko ya suruali na shati lake kwa lengo la kumpora kila alichokuwa nacho mifukoni lakini hawakufanikiwa azma yao.
“Walikuwa wakinituhumu kugonga mwendesha baiskeli, jambo ambalo si kweli. Ajali ile ilihusisha mwendesha pikipiki na mwendesha baiskeli, lakini wao wakaamua kunibambika mimi ili watimize azma yao ya kunipora,” alilalamika Maina.
Hata hivyo kijana mfanyabiashara ndogo wa eneo hilo alimwokoa kutoka mikono ya vijana hao ambao hata hivyo wengine waliendelea kumfukuza huku akikimbilia upande wa pili wa barabara, ambako kulikuwa na askari wa Usalama Barabarani.
Punde askari wa Usalama Barabarani na wale wa Doria waliwasili eneo la tukio na kutawanya vijana hao na kumchukua mkazi huyo na kwenda naye eneo ambako ilidaiwa aligonga na kukimbia.
Hata hivyo, baada ya kufikia eneo hilo ilibainika kuwa mwendesha pikipiki na mwendesha baiskeli ndiyo walikuwa wamegongana na hivyo askari kumwamuru aondoke aendelee na shughuli zake.
Kwa mujibu wa baadhi ya wapitanjia, eneo hilo limekuwa si salama kwa muda mrefu kutokana na kuwapo kundi la vijana wanaovizia kuiba kwenye magari na nyakati za jioni kukaba wapitao kwa miguu.
Wananchi hao walilitaka Jeshi la Polisi kuimarisha usalama katika eneo hilo, ikiwamo kuendesha operesheni maalumu ya kuwaondoa vijana hao.

0 comments:

Post a Comment