SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Wednesday, February 29, 2012

WABUNGE WATAKIWA KUACHA SIASA KATIKA AFYA ZA WATU

KUSHOTO NI KAIMU MKURUGENZI WA NHIF HAMIS MDEE AKIWA NA WAKUU WA WILAYA, WAKURUGENZI NA WENYEVITI WA HALMASHAURI ZA MKOA WA MBEYA LEO, AMBAPO KATIKATI WALIOKAA NI MKUU WA WILAYA YA MBEYA EVANCE BALAMA ALIYEMWAKILISHA MKUU WA MKOA WA MBEYA ABBAS KANDORO KUWA MGENI RASMI KATIKA SIKU YA WADAU KATIKA UKUMBI WA MKAPA JIJINI MBEYA.
****
WANASIASA wakiwemo Wabunge wametakiwa kuacha kuendesha vikao vya siasa pasipo kuzungumzia masuala ya wananchi wanaowaongoza kama ilivyo hivi sasa.
Hayo yameelezwa jana na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Bima ya Afya Ally Kiwenge wakati wa siku ya wadau mkoa wa Mbeya iliyofanyika katika ukumbi wa Mkapa uliopo Jijini Mbeya katika kutimiza miaka 10 ya kujituma na kuaminika tangu mwaka 2001-2011.
Amesema kuwa kwa sasa Madiwani kote nchini wamejiunga na mfuko wa jamii (CHF) lakini wabunge hawataki kujiunga na mfuko huo wala kuhamasisha wananchi kujiunga na mfumo kwa gharama isiyozidi 15,000 kwa mwaka kila kaya wakati wenyewe ndiyo waliotunga sheria.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa NHIF taifa Hamis Mdee amesema kuwa kwa mkoa wa Mbeya ni asilimia 3 pekee za kaya za wakazi wa mkoa mzima ndiyo waliojiunga na mfuko wa jamii(CHF) jambo ambalo linapaswa kujadiliwa kwa kina na kupatiwa ufumbuzi wa uhamasishaji kwa wananchi kujiunga na mfuko huo.
Mgeni Rasmi wa siku hiyo Kaimu Mkuu wa mkoa wa Mbeya Evance Balama ametanabaisha kuwa kutokana na asilimia hizo, Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya inawaagiza watendaji wote wa kila Halmashauri mkoani humo ni lazima agenda ya kujiunga na mfuko huo iwe ni lazima katika vikao na mikutano yao.
Amesema pamoja na maagizo hayo, pia watoa huduma katika Zahanati na Hospitali waache kutoa maneno ya kejeli kwa wanachama wa mfuko huo wa jamii na bima ya Afya kwa ujumla kwasababu hawatibiwi bure bali kwa fedha ambazo wamezichangia.
Ameongeza kuwa changamoto iliyopo kwa sasa ni ukosefu wa dawa katika Hospitali kwa wanachama wa bima ya Afya na upandaji wa gharama za dawa kila uchwapo jambo ambalo aliiomba Serikali kuu kulisimamia hilo na katika mkoa wa Mbeya Serikali imepanga kuwa kila Hospitali kuwe na dirisha maalum la dawa kwa wanachama wa bima ya Afya ya Taifa (NHIF) na mfuko wa jamii (CHF)
Naye Mkurugenzi wa Ushauri na tiba wa mfuko wa NHIF Dr. Frank Lekey amesema kuwa katika Tanzania wananchi wa mkoa wa Mbeya wanauelewa mkubwa wa masuala ya Afya lakini inashangaza kuona wananchi hao hawajajitokeza kujiunga na CHF.
''Umefika wakati wadau waelewe haki na wajibu wao katika mfuko huo ili waelimishe wananchi wengine kujiunga na mfuko wa CHF/NHIF'' amesema Dr.Lekey
Wadau waliokuwa wamehudhuria siku hiyo wamesema kuwa kikwazo cha wananchi kutoweza kujiunga na mfuko wa Afya ya jamii ni kutokana na wananchi hawajafikiwa na uhamasishaji wa kujiunga na mfuko huo hivyo uhamasishaji huo uhusishe viongozi wa dini na wanasiasa.
Meneja wa mfuko wa bima ya Afya ya Taifa mkoa wa Mbeya Celestin Muganga amewaonya wale wote wanaotumia vitambulisho visivyo vya kwao kwani wakibainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Kabla ya siku hiyo ya wadau, juzi viongozi wa mfuko huo walitoa mashuka 700 katika Hospitali ya mkoa wa Mbeya, Hospitali teule ya wilaya ya Mbeya Vijijini Mbalizi-Ifisi, Igawilo na Ruanda Jijini Mbeya.
Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa baadhi ya wananchi wanashindwa kujiunga na mfuko wa jamii (CHF) kutokana na kutopata huduma sahihi kupitia kadi za mfuko huo ikiwemo huduma za kulazwa hasa katika wilaya ya Mbeya Vijijini.

0 comments:

Post a Comment