Ndugu zangu,
Mhariri wa gazeti la Uhuru anaitwa Jaqueline Liana. Hakika anastahili pongezi kwa kazi yake njema kwa taifa. Niweke wazi, katika magazeti yote niliyoyapitia siku ya jana Jumamosi, gazeti la Uhuru ndilo kwangu
lilitia fora.
Kati ya habari kadhaa zenye kumfumbua macho msomaji, gazeti Uhuru lilibeba habari tatu zenye umuhimu mkubwa kwa nchi yetu; habari kuuilikuwa na kichwa cha habari; “ Ripoti uozo TBS yavaiva- Njama za
kuizima zaandaliwa”. Nyingine ni; “ Majengo ya UDA kuhifadhi makontena”. Na mwisho ni wito; “Tumieni mitandao ya kijamiikuhabarisha”. Habari hizo mbili za mwisho nitazichambua katika siku za usoni kutokana na ufinyu wa muda kwa sasa.
Nianze basi na habari kuu iliyotokana na uchunguzi wa gazeti Uhuru; Mwandishi anabainisha, kuwa taarifa ya uozo wa ndani ya Shirika laViwango Tanzania ( TBS) imekamilika na imewasilishwa kwa Spika wa
Bunge kwa hatua zaidi.
Kwamba wakati ripoti hiyo ikiwa tayari na huku Watanzania wakisubiri hatua gani zitachukuliwa, gazeti Uhuru limebaini uwepo wa mipangokabambe inayosukwa ili kuzima na kuwalinda vigogo wa shirika hilo la
umma wanaotuhumiwa kufanya mambo kinyume na taratibu.
Uhuru linabainisha, kuwa Kamati ya Bunge ya Mahesabu ya Mashirika ya Umma ( POAC) imebaini matatizo mengi ndani ya TBS yakiwemo ukaguzi wa bidhaa usiokidhi viwango na mazingira ya rushwa miongoni mwa maofisa waandamizi. Na kutokana na kubainika kwa madudu hayo, Kamati
hiyo imependekeza baadhi ya maofisa waandamizi wa TBS, akiwemo Mkurugenzi Mkuu, Charles Ekelege, wasimamishwe kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.
Na licha ya Kamati ya Bunge kukamilisha ripoti yake hiyo, uchunguzi uliofanywa na gazeti la Uhuru unaonyesha kuwa kuna mipango inasukwa kwa kuwahusisha baadhi ya wabunge, ofisi ya bunge na wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha suala hilo halifikishwi katika mkutano ujao wa bunge na kuchukuliwa hatua.
Uchunguzi wa gazeti Uhuru unazidi kuonyesha , kuwa wahusika wa mpango huo ni baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali ( PAC) na maofisa wa bunge kwa kushirikiana na maofisa waandamizi wa wizara.
Kwa mujibu wa gazeti Uhuru, mmoja wa wajumbe wa POAC alithibitisha kuwepo mipango hiyo na kuongeza kuwa, baadhi ya wabunge wanatumiwa katika suala hilo.
Mjumbe mwingine wa kamati hiyo alisema, kwa uozo ndani ya TBS uko wazi kwa sababu hata wafanyakazi wa chini wamekuwa wakilalamika kuwa wanakwamishwa kufanya kazi ipasavyo na viongozi wao.
” Wafanyakazi walitueleza kuwa wanapogundua kuna bidhaa mbovu na kuzizuia, wafanyabiashara wanazungumza moja kwa moja na viongozi wa juu wa shirika na matokeo yake bidhaa zile ambazo ni mbovu zinaruhusiwa kutumika.
” Kama watu walioaminiwa na kupewa nafasi kuongoza shirika kubwa kama hili wanakiuka utaratibu, kuna imani gani tena? Hii inaonyesha watu hawa hawana nia njema na maisha yetu na wako tayari kuwaangamiza
Watanzania kwa sababu ya maslahi yao”. Alisema mjumbe huyo.
Kwa mujibu wa gazeti Uhuru, Makamu wa Mwenyekiti wa kamati hiyo ya bunge , Mbunge wa Ludewa , Deo Filikunjombe, ameweka bayana msimamo wa kamati yake, kuwa hawatakubali suala hilo kuzimwa au kumalizwa kinyemela kwa sababu kufanya hivyo ni kukubali Watanzania waendelee kuangamia kwa kutumia bidhaa mbovu.
Filikunjombe anasema;
” Upo ushahidi kwamba zipo bidhaa zisizo na viwango kama kondomu, mafuta ya kupikia, matairi, vyakula na blue band ambazo zina nembo ya TBS na zinatumika. Huu ni uoza mkubwa, ni lazima tufike mahali tuseme
basi. Ni lazima TBS isafishwe na wahusika wa mchezo huu mchafu lazima waondolewe haraka”. ( Deo Filikunjombe, Uhuru Februari 25, 2012)
Naam, kila Mtanzania mwenye mapenzi mema na nchi yake hana budi kuwaunga mkono wahariri wa mfano wa Jacqueiline Liana na wabunge wa mfano wa Deo Filikunjombe. Ni Watanzania wenzetu walioonyesha
utayari wa kujitoa muhanga kuipigania nchi yao dhidi ya vitendo vya kifisadi kama hiki cha TBS chenye hatari ya kuliangamiza taifa.
Maggid Mjengwa,
Iringa
Jumapili, Februari 26, 2012
0 comments:
Post a Comment