Wafanyabiashara wawili mtu na mkewe, wamepigwa risasi na kumwagiwa tindikali huko Zanzibar kwa kuuza pombe.
Katika uvamizi huo uliofanyika Jumatano iliyopita mwanamke Bimal Alvind (36) alinusurika kupoteza ujauzito wake wa miezi minne baada ya kupigwa risasi ya tumbo na kumwagiwa tindikali.
Risasi hiyo ilitolewa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili bila kuathiri ujauzito huo lakini tindikali hiyo ilimjeruhi mwilini kuanzia usoni, kifuani kwenye matiti, mikono yote miwili na tumboni.
Mumewe, Alvind Asawla (42) alipigwa risasi kichwani kwenye paji la uso katikati ya macho iliyotokea nyuma chini ya shingo na sasa amepooza upande mmoja.
Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwa ndugu yake Upanga wiki hii, Asawla alisema walivamiwa Jumatano iliyopita saa 10:30 jioni katika Mtaa wa Hurumzi Mji Mkongwe.
Alisema wakati wakivamiwa, yeye na mkewe aliyeishi naye kwa miaka 17 sasa na kujaliwa watoto wawili; Priyanka (14) na Nidh (12), walikuwa wakitoka katika biashara yao wakirudi nyumbani eneo la Kiponda.
Alisema ghafla watu wawili walimvamia mkewe na kummwagia tindikali na yeye alipokuwa akijaribu kumsaidia, watu hao walimmwagia tindikali usoni.
Kwa mujibu wa Asawla, wakati wakitaharuki kwa hali hiyo, ghafla alitokea mtu mwingine na kumpiga risasi katika paji la uso akadondoka chini huku damu zikimtoka.
Alisema alijaribu kujikongoja kwa nia ya kuendelea kumsaidia mkewe lakini mtu huyo wa tatu alimpiga risasi ya pili mgongoni na mkewe akapigwa risasi ya tumbo.
Asawla alisema baada ya hapo hakujua kinachoendelea mpaka alipozinduka Kituo cha Polisi cha Malindi walipopatiwa PF3 na kupelekwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja walipopigwa picha za x-ray na kugundulika wana risasi mwilini.
Baada ya kipimo hicho, Asawla alisema hospitali hiyo haikuwa na vifaa vya kutoa risasi hizo, ndipo ndugu zake waliwasaidia usiku huo na kuwasafirisha kwa ndege hadi Dar es Salaam ambapo walikimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Alisema mkewe alilazwa katika wadi ya Kibasila namba tatu na yeye akahamishiwa katika Hospitali ya TMJ kwa ajili ya kipimo cha CT-Scan ambacho hakikupatikana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kwa mujibu wa Asawla, mke wake alitolewa risasi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na yeye kufanyiwa upasuaji wa kumtoa risasi ulifanyika katika Hospitali ya TMJ.
Alisema anamshukuru Mungu kwa kuwa ni mzima hadi sasa kwani alipigwa risasi sehemu mbaya na kukaa nayo kwa saa zaidi ya 12 ndipo ilipotolewa kichwani jambo lililowashangaza hata baadhi ya wauguzi.
“Nimepooza upande mmoja wa kichwa changu, sihisi jambo lolote lakini madaktari wameniambia nitarudi katika hali yangu ya kawaida polepole baada ya kufanya mazoezi,” alisema.
Alisema aliambiwa kuwa risasi hizo hazikupita katika mishipa mikubwa ndiyo maana yuko hai hadi sasa na mshipa mdogo uliomwaga damu, umefanya jicho la upande uliopooza kuwa jekundu licha ya kuona vizuri.
Mfanyabiashara huyo alisema kuwa watu hao wamempa ulemavu wa kudumu bila kutegemea huku akiamini siyo majambazi ingawa walichukua pochi ya mkewe iliyokuwa na fedha kidogo.
Alisema hospitalini wameambiwa tindikali waliyomwagiwa ni aina ya asidi sulfuriki (sulphuric acid) inayotumika katika magari.
“Unajua mwizi anataka fedha na siyo kumwagia tindikali au kukupiga risasi na sisi hatukuwa na silaha yoyote; nia ya watu hawa ni kutuua kwani tumekuwa tukipata vitisho vya mara kwa mara kutokana na biashara yetu ya kuuza pombe Zanzibar,” alidai.
Alidai mara kwa mara wamekuwa wakipata vitisho ikiwemo kukuta karatasi inayomtaka kuacha biashara hiyo vinginevyo utauawa; na wamekuwa wakitoa taarifa katika vituo vya Polisi vilivyopo karibu na biashara zao.
Alilalamika kuwa licha ya wafanyabiashara wengi wa pombe kufanyiwa vitendo vya kumwagiwa tindikali, kupiwa risasi na hata kuchomwa moto, hakuna aliyewahi kukamatwa na kuchukuliwa hatua.
“Sisi tunafanya biashara na mahoteli makubwa ya kitalii na tunalipa kodi zote stahiki, Serikali iseme wazi kama haitaki biashara hii Zanzibar au wawadhibiti watu hawa,” alisema.
Alidai kuwa matukio kama hayo ni ya muda mrefu na mwaka 2007 wakati wa Jumatatu ya Pasaka, baba yake mzazi, Ahandillal Asawla aliyekuwa akifanya biashara hiyo alimwagiwa tindikali usoni akafariki dunia.
“Hata baba yangu aliuawa lakini hakuna hata mtu aliyekamatwa na Serikali haikufanya jambo lolote, sasa umefika wakati Serikali itulinde tunaofanya biashara hii au itangaze kusitisha kwa manufaa yetu,” alisema Asawla.
Alisema cha kushangaza tangu ukoloni babu zake waliuza pombe kwa amani lakini sasa wanatumia pombe kama sababu za kisiasa ili kuangusha uchumi wa Zanzibar.
Gazeti hili liliwasiliana na uongozi wa Polisi katika Mkoa wa Mjini Magharibi bila mafanikio.
Kwanza Kamanda wa Polisi Mjini Magharibi, ACP Azizi Mohamed simu yake iliita bila majibu na simu ya Kamisha wa Polisi Zanzibar, CP Musa Musa haikupatikana pia.
Baadaye gazeti hili lilifanikiwa kumpata Ofisa Uhusiano Polisi Zanzibar, Asha Mzule lakini alisema kuwa ni mgonjwa kwa muda kidogo hivyo hajui kinachoendelea na kutoa namba ya simu ya OCD wa Wilaya ya Mji Mpya.
Hata hivyo OCD huyo alikataa kuzungumzia uvamizi huo wala kutaja jina lake lakini akashauri atafutwe ACP Azizi ambaye alidai yuko Uwanja wa Ndege akimsubiri Rais wa Zanzibar, Dk. Mohamed Shein anayetokea nje ya nchi.
Namba ya ACP Azizi ilipopigwa kwa mara ya pili, haikupatikana kabisa.
******
Picha via blogu ya Lukwangule, habari via HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment