Maalim Seif akiwa katika barza ya kwanza ya mazungumzo Radio One Darajabovu jana. (Picha, Hassan Hamad.Picha na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais-Zanzibar
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad ameanza utekelezaji wa mpango wake wa kutembelea baraza za mazungumzo kwa lengo la kuwa karibu zaidi na wananchi.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar ameanza ziara hiyo katika barza ya Radio One Darajabovu Zanzibar na kuzungumza na wananchi juu ya mambo mbali mbali yanayohusu maendeleo yao na taifa kwa jumla.
Amesema ameanza ziara hiyo katika Barza hiyo kwa kuelewa historia yake katika historia za siasa za upinzani Zanzibar.
“Nimeamua nianzie barza zangu hapa Radio One kwa kuelewa historia na na umuhimu wa barza hii katika ulingo wa siasa zetu”, alisema Maalim Seif.
Ziara hiyo inatoa changamoto kwa baadhi ya viongozi wa majimbo ambao wamekuwa wakilalakiwa kwa kukimbia majimboni mwao na hatimaye kuwa mbali na wananchi, jambo ambalo linawafanya wapiga kura wao kutoamini kile kinachotokea baada ya viongozi hao kuchaguliwa.
Mara kwa mara Maalim Seif amekuwa akiwahimiza viongozi wa majimbo kufanya bajeti ya muda ili kutenga muda kwa ajili ya kutembelea barza za mazungumzo na kushiriki shughuli za kijamii zikiwemo mazishi na harusi.
Katika mazungumzo hayo Maalim Seif alielezea juhudi zinazochukuliwa na serikali katika kuwakwamua na ukali wa maisha, licha ya kuonekana hali kuwa tofauti na hivyo kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa mbali mbali hasa vyakula.
Amesema serikali inatambua hali inayowakabili wananchi lakini inafanya juhudi kuona kuwa matatizo ya wananchi yanapatiwa ufumbuzi muafaka katika kipindi kifupi kijacho.
“kipindi cha mwaka mmoja uliopita serikali ilikuwa inajipanga kuangalia namna ya kukabiliana na matatizo haya, lakini nna matumaini kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ijayo hali itakuwa tofauti kabisa Insha-Allah”, alisema Maalim Seif.
Amesema serikali inafanya juhudi za kuwaalika wawekezaji kuja kuwekeza Zanzibar sambamba na kuimarisha huduma za kilimo na uvuvi kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi
Na Hassan Hamad
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais-Zanzibar
0 comments:
Post a Comment