SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Wednesday, November 23, 2011

Homa Ya Lowassa CCM Yapanda

• Mwenyewe adaiwa kujipanga kufichua siri NEC
na Mwandishi wetu
Jina la Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, ndilo lililotawala mazungumzo miongoni mwa wajumbe vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), Tanzania Daima Jumatano limebaini.

Mbali ya kutawala mazungumzo, Lowassa amewagawa katika makundi mawili wajumbe wa vikao hivyo kwa kiwango ambacho baadhi ya wadadisi wa mambo wanakielezea kuwa ni cha hatari kubwa kwa ustawi wa chama hicho.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa kufanya mahojiano na watu mbalimbali unaonyesha kwamba ndani na nje ya vikao hivyo kumekuwa na harakati zinazoendeshwa na ama watu wanaomuunga mkono Lowassa au wale ambao wamejitoa mhanga kuhakikisha anaachia nafasi ya ujumbe wa NEC.

Hali hiyo ya mambo ilisababisha mara tu baada ya kuanza kwa kikao cha Kamati Kuu (CC) jana watu wanaotaka kujua hatima ya mwanasiasa huyo ambaye alijiuzulu uwaziri mkuu Februari mwaka 2008 kufuatilia kwa karibu mwenendo wa kikao hicho.

Wakati wajumbe wakiendelea na mkutano huo, habari ambazo chanzo chake hakijulikani zilisambazwa katika maeneo mbalimbali nchini na kisha zikachapwa katika mitandao ya kijamii zikieleza kwamba tayari CC ilikuwa imeshapendekeza kwa NEC uamuzi wa kuwavua uongozi Lowassa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.

Hata hivyo, Tanzania Daima Jumatano lilibaini kwamba uvumi huo ambao ulisambazwa pia ndani ya chumba chetu cha habari haukuwa na ukweli wowote.

Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho waliozungumza na gazeti hili walisema hadi walipokuwa wakienda katika mapumziko ya jioni jana walikuwa wamejadili mada moja tu kubwa ya uwekezaji kabla ya kuzungumzia ombi la viongozi wa CHADEMA la kuomba kukutana na Rais Kikwete.

Mmoja wa wajumbe hao alieleza kwamba, walikuwa wakitarajia kuizungumzia dhana ya kujivua gamba wakati watakapokuwa wamerejea katika kikao hicho jana jioni.

Kwa mujibu wa mjumbe huyo, hali ndani ya kikao hicho ilikuwa imetawaliwa na mazingira ya kile alichokieleza kuwa ni ‘kuviziana’ kila mjumbe akionyesha shauku ya kujua hatima ya suala hilo.

Mjumbe mwingine wa CC aliyezungumza na Tanzania Daima Jumatano aliyejitaja kuwa ni mtetezi wa Lowassa alisema walikuwa makini wakisubiri suala hilo ambalo walisema wanakusudia kulipinga kwa nguvu zao zote iwapo litachukua mwelekeo wa kutaka mwanasiasa huyo ang’olewe.

Mwanasiasa huyo alisema, tayari yeye na wajumbe wenzake aliosema wanazidi 10 walikuwa wamejitoa mhanga kuhoji sababu hasa za kufikiwa kwa maamuzi hayo ambayo wanayasubiri kwa shauku kubwa.

“Sisi tumejipanga vilivyo kulisubiri hili. Tutataka kupata maelezo ya kina na yanayojitosheleza kabla ya kulikubali pendekezo lolote lenye mwelekeo wa kutaka kumhujumu Lowassa au Chenge,” alisema mjumbe huyo wa CC.

Mjumbe huyo alisema wanajua kwamba Lowassa wanataka kumng’oa NEC wakitumia hoja ya Richmond ambayo tayari wameishaichambua na kujiridhisha kwamba haikupata kuthibitishwa kwa namna yoyote kwamba mwanasiasa huyo alishiriki katika matendo ya namna yoyote ya ukosefu wa maadili katika mchakato wake.

“Tumejipanga kuichambua Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyoichunguza Richmond ikiwa ni pamoja kuyapitia maazimio yote 23 ya Bunge kuhusu suala hilo ambayo hakuna hata moja linalomtia hatiani Lowassa,” alisema mjumbe huyo wa CC.

Mjumbe huyo alisema pia kwamba, iwapo ndani ya CC hoja hiyo itapitishwa basi ndani ya NEC wamejipanga kuwashawishi wajumbe wengi zaidi kuikabili.

Mbali ya hilo, mjumbe huyo wa NEC alisema tayari walikuwa wameshamshawishi Lowassa mwenyewe kutoa maelezo yake ya kina ikiwa ni pamoja na utetezi wake kuhusu ushiriki wake katika suala la Richmond ambalo limekuwa likitumiwa kumshambulia.

“Tumemweleza amekaa kimya kwa muda mrefu sana na kwamba huu ndiyo wakati wake wa kukata mzizi wa fitina. Ameahidi kusema kila ukweli anaoujua,” alisema mtoa habari wetu huyo.

Mjumbe huyo alisema katika utetezi wao kwa Lowassa wamejipanga katika kuhakikisha kwamba Katibu wa Idara ya Uenezi na Itikadi, Nape Nnauye anashtakiwa mbele ya wajumbe wa NEC kwa kuchochea mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hicho tangu achaguliwe.

Hata hivyo, wakati mjumbe mwingine wa vikao hivyo vyote viwili alieleza kwamba taarifa ambazo zimesambaa miongoni mwa wajumbe wa CC na NEC ni kwamba baadhi ya watu wameshajipanga ili kuhakikisha Lowassa na Chenge wanawajibishwa kwa gharama zozote zile kama mbinu pekee ya kukinusuru chama hicho.

Wakati mjumbe huyo akitoa maelezo hayo pasipo kufafanua, mjumbe mwingine wa CC ambaye pia ni mkuu wa idara moja ndani ya CCM, alisikika akiwaeleza wajumbe wa NEC ambao si wajumbe wa kikao cha kamati kuu kuwa, watulivu kwani kila kitu kilikuwa kinakwenda sawa.

Kada huyo wa CCM alisema alikuwa ana imani kubwa kwamba dhana ya kujivua gamba itatekelezeka vyema baada ya mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete kubuni njia bora ya kuitekeleza. Hata hivyo hakuitaja njia hiyo.

“Wala hatuna sababu ya kuwa na wasiwasi. Lowassa na Chenge lazima watang’oka. Ni jambo jema kwamba mwenyekiti ameshakuja na njia nzuri ya kulitekeleza suala hili,” alisema mjumbe huyo wa CC.

Mbali ya hilo, mjumbe huyo alisema kwa jinsi mambo yalivyo walikuwa wakitarajia kupata upinzani mkali kuhusu suala hilo ndani ya NEC ambako Lowassa na Chenge wanaonekana kuwa na utetezi mkubwa.

“Tunajua kwamba wamejipanga kukabiliana na suala hili ndani ya NEC, lakini sisi tunaangalia maslahi ya chama zaidi kuliko yale ya mtu binafsi,” alisema kada huyo wa CCM.

Habari zaidi kutoka miongoni mwa wajumbe wa vikao hivyo zinaeleza kwamba, mmoja wa viongozi wa juu wa CCM ametangaza kwamba atajiuzulu nafasi yake ya uongozi ndani ya chama hicho iwapo maamuzi ya kujivua gamba yanayotakiwa kuwagusa Lowassa na Chenge yatafunikwa.

“Mwenzetu huyu (anamtaja) amesema waziwazi kwamba ameshajiandaa kujiuzulu nafasi zake zote za uongozi ndani ya CCM iwapo Lowassa na Chenge wataendelea kubakia kuwa wajumbe wa NEC baada ya kumalizika kwa vikao hivi. Tusubiri tuone,” alisema mjumbe mwingine aliyezungumza na Tanzania Daima Jumatano.

Wakati hayo yakitokea kumekuwa na taarifa za kuchanganya kuhusu msimamo wa Rais Kikwete katika suala zima linalohusu utekelezaji wa suala hili la kujivua gamba.

Taarifa ambazo gazeti hili linazo zinaeleza kwamba, katika matukio tofauti ya moja kwa moja au ya kutumia watu wake wa karibu, Kikwete amepata kukaririwa katika vikao visivyo rasmi akisema alikuwa ameshaachana na suala hilo la kujivua gamba.

Mmoja wa watu walio karibu na Kikwete amelieleza Tanzania Daima Jumatano kwamba hivi karibuni katika kikao cha siri kilichofanyika Dubai, kiongozi huyo alikutana na mmoja wa marafiki zake wa karibu na kumhakikishia kwamba hataendeleza tena utekelezaji wa suala hilo baada ya kubaini mambo kadha wa kadha.

“Huyu bwana mkubwa si mtu wa kuaminika kabisa, ingawa katika mawasiliano aliyoyafanya ana kwa ana na rafiki yake mkubwa (jina tunalo) Dubai hivi karibuni alisisitiza kwamba hakutakuwa na kitu kama hicho,” kilisema chanzo kimoja cha kuaminika.

Chanzo kingine cha habari kimelieleza gazeti hili kwamba, hivi karibuni Lowassa mwenyewe alipata kusikika akimueleza mtu wake wa karibu kuhusu kupokea ujumbe wa maandishi kupitia katika simu yake ya mkononi uliotoka kwa Rais Kikwete ukimhakikishia kwamba alikuwa hana sababu hata moja ya kumuandama kisiasa.

“Katika masuala kama haya unapaswa kujua mwelekeo wa mwenyekiti katika masuala yote makubwa kama haya. Mtu wa karibu na Lowassa ametuhakikishia kwamba Kikwete aliwasiliana naye kwa njia ya ujumbe wa simu ya mkononi na kumhakikishia kwamba alikuwa hana sababu ya kuwa na hofu kuhusu suala lolote,” alisema mtoa habari mmoja.
CHANZO: BOFYA

0 comments:

Post a Comment