Na.Mwandishi wetu, Dodoma. MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), amependekeza muswada wa mabadiliko wa sheria ya katiba mpya, usitishwe kwanza kwa kuwa hauna maoni ya wananchi. Ameliomba bunge kumwomba Rais Jakaya Kikwete kuondoa hati ya dharura ya kuwasilisha muswada huo ili kutoa fursa kwa wabunge kurudi kwenye majimbo yao kuzungumza na kupata maoni yao ndipo uwasilishwe tena bungeni. Kwa upande wake, serikali imesema kuwasilishwa kwa muswada huo pamoja na mambo mengine umelenga kuanzisha Tume itakayoratibu mchakato wa utungwaji wa Katiba mpya. Hayo yalijitokeza bungeni mjini Dodoma leo, wakati Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, alipomaliza kujibu swali la mbunge Fakharia Shomar Khamis (Viti Maalumu-CCM). Baada ya waziri huyo kumaliza kujibu swali hilo, mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa, alisimama na kusema watanzania wengi hawafahamu kuzungumza wala kusoma lugha ya kiingereza. Alisema kwa hali kama hiyo wengi hasa walio vijijini hawatapata fursa nzuri ya kuchangia muswada huo na kutoa maoni. Alisema mbali na watanzani walio wengine, lugha ya kiingereza imekuwa ikiwasumbua hata baadhi yetu na kwamba, muswada huo ulipaswa kuwa kwa lugha inayofahamika na wengi. “Huu muswada umeandikwa kwa kiingereza na watanzania wengi hawaifahamu lugha hii, watachangiaje na kutoa maoni yao,” alisema. Hoja hiyo ilimsimamisha Kabwe na kusema muswada huo umeletwa mbele ya wabunge mapema hata kabla ya wananchi kutoa maoni yao. “Wabunge wengi hawana mawazo ya wananchi ambao ndiyo wapigakura wetu. Huu muswada hautakuwa na ridhaa ya wananchi na ningependekeza usitishwe kwanza,” alisema. Spika wa Bunge Anne Makinda, alisimama na kuweka bayana kuwa Kabwe ni miongoni mwa wabunge waliopo kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge na alikuwa akihamasisha muswada huo kuwasilishwa bungeni haraka. Pia, wabunge Mohammad Ibrahim Sanya (Mji Mkongwe-CUF) na Mohamed Habib Mnyaa (Mkanyageni-CUF), nao walisimama kuhoji nafasi ya Zanzibar kupewa fursa ya kuwa na kituo cha kukusanya maoni ya wananchi. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema akijibu baadhi ya hoja za wabunge hao, alikiri upungufu uliotokana na muswada huo kuandikwa kwa lugha ya kiingereza.
0 comments:
Post a Comment