Maafisa wa afya wamesema zaidi ya watoto mia moja
wamefariki dunia kutokana na sumu ya madini ya risasi nchini Nigeria
katika majuma ya hivi karibuni.
Idadi ya vifo imekuwa ikiongezeka tangu mwezi
March, baada ya wakaazi kuanza kuchimba dhahabu kinyume cha sheria
katika maeneo yenye madini mengi ya risasi au lead.
Wengi wa waathiriwa ni kutoka maeneo ya vijijini
katika jimbo la Zamfara, kaskazini mwa nchi.
Jumla ya kesi 163 kati ya kesi 355 zimesababisha
vifo, kulingana na afisa wa afya kutoka Nigeria.
Dr Henry Akpan, afisa katika wizara ya afya,
alisema " waathiriwa walikuwa wakichimba dhahabu, lakini maeneo hayo
yana kiwango kikubwa cha sumu ya madini ya risasi".
Maafisa wa afya wameweka kambi mbili katika eneo
hilo kuwatibu watu wanaosumbuliwa na dalili za sumu hiyo ya madini ya
risasi.
Mwandishi wa BBC mjini Kaduna amesema vifo hivyo
viligunduliwa wakati wa chanjo ya kila mwaka inayofanyika nchini, baada
ya maafisa kutambua kuwa hakuna watoto katika maeneo ya vijijini ya
jimbo hilo la kaskazini mwa nchi.
Wanavijiji walisema kuwa watoto walikufa kwa
ugonjwa wa malaria, lakini baada ya kundi la madaktari kutoka shirika la
kimataifa la Medecins Sans Frontiers kufanya vipimo vya damu wakagundua
kuwepo kwa kiwango kikubwa cha sumu hiyo.
Jimbo la Zamfara hivi karibuni liliipatia
kandarasi kampuni kutoka Uchina kuchimba dhahabu katika eneo hilo.
Lakini wanavijiji nao walijaribu kujinufaisha
kwa kuchimba dhahabu bila ya idhini, jambo ambalo ni kosa nchini
Nigeria.
Mwandishi wa BBC anasema huenda wakaazi hao
waligonjeka baada ya sumu iliyotokana na mfumo wa kusafisha dhahabu hiyo
kuchanganyika na maji.
BBC SWAHILI
0 comments:
Post a Comment