Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(TPDC) Bw. Yona Killagane akitoa ufafanuzi mbele ya waandishi wa habari
(hawapo pichani) kuhusiana na Kampuni ya Statoil yenye mkataba wa
kuchimba mafuta nchini Tanzania.
Kaimu Mkurugenzi Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
Bw. James Andilile (kushoto) akijibu maswali toka kwa waandishi wa
habari waliohudhuria Mkutano uliohusu Kampuni ya Statoil yenye mkataba
wa kuchimba mafuta nchini Tanzania baada ya kutokea kwa mkanganyiko kwa
baadhi ya vyombo vya habari kuandika habari zilizokinzana kuhusu Kampuni
hiyo. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC) Bw. Yona Killagane.
Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria Mkutano huo
wakifuatilia kwa makini taarifa ya ufafanuzi iliyokuwa ikitolewa na
baadhi ya Viongozi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
kuhusu Kampuni ya Statoil yenye mkataba wa kuchimba mafuta nchini
Tanzania.Picha na Benedict Liwenga-MAELEZO.
----
Na Benedict Liwenga na Winner Abraham-MAELEZO.
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli
Tanzania TPDC limetoa ufafanuzi kuhusiana na Kampuni ya Statoil yenye
mkataba wa kuchimba mafuta nchini Tanzania baada ya kutokea kwa
mkanganyiko kwa baadhi ya vyombo vya habari kuandika habari
zilizokinzana kuhusu Kampuni hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Bw. Yona Killagane ameeleza taarifa
zilizo sahihi kuhusu kampuni ya Statoil na mikataba yake mbalimbali na
Serikali katika upataji wa faida kutokana na utafutaji wa mafuta na
gesi .
Killagane ameeleza kuwa utaratibu
unaotumika katika kutafuta mafuta ni aghali sana na ni hatari kwa
maisha, hivyo serikali haiwezi yenyewe kuingia gharama hizo za utafutaji
na badala yake inatumia mifumo mbalimbali kama vile Concession agreement, Service agreement pamoja na Mkataba wa kugawana mapato
ambapo kati ya mikataba hiyo mitatu Serikali inatumia mkataba wa
kugawana mapato ambapo humpa mwekezaji kazi kisha rasilimali
zikigunduliwa hugawana na kampuni hiyo au mwekezaji aliyegundua. Hivyo
serikali inategemea kupata mrahaba na kodi toka kwa makampuni
inayoingianayo mikataba.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi
amevieleza vyombo vya habari kuwa ugunduzi wa gesi unategemea miundo
mbinu mingi sana na inategemea uwingi wa gesi hiyo ndiyo maana serikali
inaingia mikataba na makampuni makubwa yenye uwezo mkubwa wa kifedha ili
kuweza kufanya utafiti na kuchimba mafuta na gesi.
Aidha, Bw. Killigane amefafanua
kuwa mkataba walioingia kati ya Serikali na kampuni ya Statoil mwaka
2007 ulikuwa ni wa kutafuta mafuta na sio gesi lakini hapo mwaka 2012
mkataba mwingine wa kutafuta gesi ulifanyika kati ya kampuni hiyo na
Serikali.
“Statoil ilipendekeza kuwa kwenye
mgao wa mkataba wa mwanzo serikali ipate asilimia 5% statoil asilimia
95% kama zabuni iliyokuwa imeletwa, lakini baadaye kamati ikakaa na
kuzungumza na mwekezaji ambapo mwekezaji aliweza kusukumwa kutoka
asilimia 5% hadi asilimia 30% na hivyo hii ilijumuisha TPDC kuweza
kujiunga kwa asilimia 10%, kwa sasa katika mkataba wa mafuta serikali
inapata asilimia 56% na Statoil asilimia 44%, katika mkataba wa wagesi
serikali inapata asilimia 61% na mwekezaji asilimia 39% katika kipindi
cha mkataba”. Alisema Killigane.
Naye Kaimu Mkurugenzi Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Bw. James Andilile aliwahakikisha
waandishi wa habari kuwa serikali iko tayari kusaidiana na waandishi wa
habari katika kutoa taarifa sahihi ili kuweza kuwaeleza watanzania
kuhusiana na sekta ya mafuta na gesi na nini kinaendelea.
“Hii nchi ni yetu na kazi zote
tunazozifanya ni kwajili ya watanzania, jinsi waandishi wa habari
wanavyotoa taaarifa zisizo sahihi wanaharibu sura ya nchi yetu na kuwapa
hofu wawekezaji na hivyo kuleta hasara badala ya faida, kama kuna jambo
lisiloeleweka tunawaomba kwa wakati wowote mkituita tutakuwa tayari
kuwapa taarifa ili wote kuwa katika ufahamu mmoja”. Alisema Andilile.
0 comments:
Post a Comment