Baraza
la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) limetangaza 6 Oktoba kuwa ni tarehe
ya kuanza kwa mafunzo ya stashahada ya ualimu wa shule za msingi
(Ordinary Diploma in Primary Education (ODPE)) katika vyuo teule vya
majaribio na Stashahada maalumu ya Ualimu wa Sekondari kwa waliomaliza
kidato cha nne (Hisabati na Sayansi) itakayoendeshwa katika chuo kikuu
cha Dodoma.
Zoezi
la uombaji wa mafunzo hayo kwa mwaka 2014/15 lilianza rasmi tarehe 23
June 2014 na litakoma 31 Agosti 2014 na mafunzo yataendeshwa katika vyuo
teule vilivyoteuliwa na Baraza (NACTE) ambavyo vitaendesha mafunzo
chini ya uangalizi wa karibu wa Baraza hilo, Taasisi ya Elimu na Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Katibu
Mtendaji wa Baraza hilo Dk. Primus Nkwera amesema waombaji wote
wanatakiwa kuzingatia utaratibu wa uombaji ambao ni kupitia njia ya
mtandao kupitia Mfumo wa Udahili wa Pamoja (Central Admission System -
CAS) inayopatikana kwenye tovuti ya CAS inayopatikana www.cas.ac.tz au Baraza www.nacte.go.tz na kwamba Baraza halitomtambua mwombaji yeyote atakayeomba kinyume na utaratibu uliowekwa.
Dk.
Nkwera amesema lengo la mafunzo hayo ni kutoa nafasi kwa walimu wa shule
za msingi kuongeza uwezo na kujiendeleza kwa masomo ya ngazi ya juu.
Kwa muda mrefu walimu wa shule wa shule za msingi wamekuwa hawana namna
ya kuongeza na kuboresha taaluma yao kutokana na kutokuwapo kwa kozi ya
namna hiyo. Stashahada hiyo haitamuhitaji mwalimu tarajali au yule
aliyepo kazini kufanya mafunzo ya kidato cha sita na badala yake
anatakiwa kufanya mafunzo ya kuendeleza ualimu wake kwa stashahada hiyo.
“Baraza
linapenda kuufahamisha umma na wahitimu wa kidato cha Nne na ngazi ya
cheti na stashadaha katika fani mbalimbali kwamba uombaji wa mafunzo ya
ngazi ya stashahada ya elimu ya ualimu wa shule za msingi kwa mwaka
2014/15 unakoma tarehe 31 Agosti 2014.”Alisema Dk. Nkwera
Amesema
kuwa maombi yatafanywa kwa njia ya mtandao kupitia Mfumo wa Udahili wa
Pamoja (Central Admission System) inayopatikana kwenye tovuti ya Baraza
www.nacte.go.tz au kwa kujaza fomu maalumu za maombi zinazopatikana
katika tovuti ya baraza na kwamba waombaji watakuwa na uwezo wa kuchagua
vyuo wanavyovipenda baada ya kulinganisha gharama za mafunzo na huduma
za ziada zitolewazo na vyuo husika. “Ili kudhibiti ubora katika programu
hii, Baraza limeweka mfumo wa udahaili wa pamoja ambao ndio pekee
utakaotumika katika kudahili wanafunzi kwenye vyuo husika, tunasisitiza
kwamba yeyote atakaekwenda kinyume na utaratibu huu Baraza
halitomtambua.”Alisisitiza
Dk.
Nkwera amewataka waombaji wote pamoja na vyuo kuzingatia taratibu za
uombaji na udahili zilizowekwa ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza
ikiwemo kutotambuliwa kwa wadahaliwa kwa kuwa vyuo kwa sasa haviruhusiwi
kudahili wanafunzi moja kwa moja kwa kuwa jukumu hilo sasa ni la
Baraza.
Kuhusu
walimu wa masomo ya sayansi, Dk. Nkwera amezungumzia jitihada
zinazochukuliwa na serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
katika kukabiliana na upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi ikiwemo
shule za msingi.
Amesema
serikali imeamua kuwa waombaji wote waliomaliza kidato cha Nne wenye
ufaulu wa daraja la kwanza na la pili na wenye ufaulu wa masomo ya
sayansi na walimu wenye cheti cha ualimu daraja la “A” wenye ufaulu wa
masomo ya sayansi na ambao wanafundisha masomo hayo watapatiwa mkopo na
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.
“Serikali
inaguswa sana na changamoto iliyopo ya uhaba wa waalimu wa masomo ya
sayansi na ina imani kuwa kwa kuwapatia mikopo waombaji wote wanaokidhi
sifa na vigezo ni chachu mojawapo ya kulipatia suluhu tatizo hilo kwa
kuwapa motisha wote wanaofaulu na walio tayari kufundisha masomo
hayo.”Aliongeza Katibu Mtendaji huyo wa NACTE.
Amesema
maelezo ya kina kuhusu sifa za udahili, nafasi za udahili kwa kila chuo
pamoja na ada inayotozwa yanaonekana katika mtandao mara mwombaji
anapobofya kitufe cha uchaguzi wa chuo.
Waombaji
wote wanaweza pia kutumia ofisi za kanda za NACTE zilizofunguliwa hivi
karibuni Zanzibar na Arusha (Kwa mikoa Kaskazini), Mbeya (Mikoa ya
Kusini), Dodoma (Mikoa ya kanda ya kati) na Mwanza kwa ajili ya mikoa ya
kanda ya Ziwa.
Wadau
wote walio jirani na mikoa hiyo wanaweza kupata huduma zote pasipo
kulazimika kwenda Dar es Salaam. Pia waombaji wote wa programu za
shahada wanaoendelea kutuma maombi yao kwa njia ya mtandao wanashauriwa
kuwasiliana na ofisi za kanda kwa kupata msaada wa haraka zaidi pale
wanapokutana na matatizo ya kiufundi. Namba za simu na mahali ofisi
zilipo vinapatikana kwenye tovuti.
0 comments:
Post a Comment