Bingwa wa ngumi za kulipwa duniani, Francis Cheka ‘SMG’ akiwa amebebwa na mashabiki wake.(Picha na Maktaba).
Na Mwandishi wetu
Jeshi
la Polisi mkoani Morogoro linamshikilia bingwa wa ngumi za kulipwa
duniani, Francis Cheka ‘SMG’ kwa tuhuma za kumchapa Meneja wa baa ya
Vijana Social Hall iliyopo Kata ya Sabasaba, Manispaa ya Morogoro.
Kwa
mujibu wa maelezo ya meneja huyo, Bahati Kabanda ‘Masika’ (39), Cheka
alifika katika baa hiyo majira ya jioni na kuanza kumtukana na
kumshambulia kwa maneno machafu kisha kumvamia na kuanza kumchapa ngumi
na mateke sehemu za tumboni.
Kwamba ni tukio la Juni 2, mwaka huu katika baa hiyo inayomilikiwa na promota wa ngumi za kulipwa mkoani Morogoro, Zumo Makame.
Kabanda
amedai wakati akipewa kichapo na Cheka, hakuna mtu aliyesogea kuamulia
ugomvi huo kutokana na watu kumuogopa bondia huyo aliyewahi kuwapiga
mabondia wa ndani na nje ya nchi.
Alidai
Cheka alifika katika baa hiyo na dalili za kulewa pombe na baada ya
kuondoka, wasamaria wema walimchukua yeye hadi katika hospitali ya rufaa
ambako alilazwa na kupatiwa vipimo na matibabu ya maumivu aliyoyapata.
Kabanda
alidai kuwa hakuwa na ugomvi na bondia huyo, na hivyo hajui chanzo cha
kupigwa na kuongeza kuwa kama alikuwa na ugomvi nae angemfikisha kwenye
vyombo vya sheria na sio kujichukulia sheria mkononi.
Masika
alidai kuwa pamoja na kupatiwa matibabu, lakini bado hali yake kiafya
sio nzuri kutokana na maumivu aliyoyapata ya mbavu, hivyo kumfanya
ashindwe kutembea vizuri.
Baadhi
ya mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa walimuona Cheka akimuangushia
kipigo meneja huyo, lakini walishindwa kuamulia ugomvi huo kutokana na
kumwogopa Cheka ambaye ni bingwa wa ngumi duniani.
Mganga
Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, Ritha Lyamuya, alikiri
kumpokea Masika hospitalini hapo Juni 2, akiwa na maumivu ya mbavu na
walipompima X-ray ilionekana amepata maumivu, hivyo walimpatia matibabu
na kumruhusu kurudi nyumbani.
Alisema hadi anaruhusiwa hospitalini hapo, Masika alikuwa anaendelea vizuri.
Kamanda
wa Polisi mkoani hapa, Leonard Paulo, amekiri Cheka kufanya shambulio
hilo kwa meneja huyo kwa kumpiga sehemu za tumboni na kichwani.
Paulo
alisema Cheka amekamatwa na anashikiliwa na polisi kwa mahojiano na
kwamba katika maelezo yake, anadai kuwa yeye na Masika walikodi baa hiyo
na kufanya biashara kwa pamoja, lakini baadaye walianza kukosana katika
suala na mapato.
Cheka
aliendelea kudai kuwa siku ya tukio alifika katika baa hiyo kwa lengo
la kutaka kujua namna mauzo yanavyokwenda, lakini meneja huyo alimzuia
kuingia kaunta na ndipo ilitokea kutoelewana na baadae ugomvi huo
kutokea.
Kamanda
Paulo alisema pamoja na maelezo hayo ya Cheka, lakini ameiagiza timu ya
askari kuchunguza kwa kina tukio hilo ili sheria iweze kuchukua mkondo
wake.
0 comments:
Post a Comment