Mchezaji wa Chelsea Branislav Ivanovic (kushoto) alipoumwa na mchezaji Luis Suarez. 22 April 2013
Suareza alisema awali kuwa baadhi ya matukio yanayotokea uwanjani hayapaswi kugeuzwa kashfa
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Uruguay Luis Suarez amefungiwa mechi tisa na shirikisho la kandanda duniani Fifa baada ya kupatikana na hatia ya kumng'ta mlinzi wa timu ya Italia Giorgio Chiellini kwenye mechi yao ya kombe la dunia nchni Brazil.
Suarez pia amefungiwa kutojihusisha na shughuli yoyote ya kandanda kwa miezi minne na kutozwa faini ya dola elfu mia moja.
Kutokana na adhabu hiyo Suarez sasa hatashiriki tena kwenye mechi zilizosalia za kombe la dunia.
Kutokana na adhabu hiyo iliyochukuliwa na kamati ya nidhamu ya Fifa Suarez sasa hatashiriki kwenye mechi ya raundi ya pili kati ya Uruguay na Columbia Juni tarehe 28.
Adhabu hiyo pia inamaanisha Suarez hatashiriki kwenye mechi za Uruguay zijazo za kombe la dunia endapo timu itazidi kusonga mbele na zile zijazo za kufuzu kwa mashindano ya kombe la dunia.
Kamati hiyo ya nidhamu ya Fifa imesema Suarez hatakiwi kuingia kwenye uwanja wowote Uruguay inapocheza wakati wa adhabu hiyo ya kutocheza mechi tisa za kimataifa.
Mwenyekiti wa kamati ya nidhamu ya Fifa Claudio Sulser amesema:"Hatuwezi kuruhusu tabia duni kama hii uwanjani hasa wakati wa kombe la dunia kwani mamillioni ya mashabiki kote duniani wanafuatilia mashindano haya. Kamati ya Fifa imetilia maanani kila kitu kwenye kitendo hicho kabla ya uamuzi huo.Tayari tumemjulisha mchezaji huyo na shirikisho la kandanda la Uruguay.''
Mashabiki wengi duniani wamemshutumu vikali Suarez kwa kumng'ata mchezaji huyo wa Italia kwani hii ni mara ya tatu anapatikana na hatia hiyo.
Lakini mashabiki, waandishi wa habari wa Uruguay na shirikisho la kandanda nchini humo wamemtetea mchezaji wao,wakisema hizo ni njama za kumuangamiza Suarez ambaye huichezea Liverpool ya England
HABARI NA BBC