SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Thursday, March 13, 2014

WAZAZI WEZESHENI WATOTO WAKIKE KUPENDA MASOMO YA SAYANSI - MAEMBE

Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bibi. Anna T. Maembe akisisita haja na umuhimu wa wazazi kuwawezesha watoto wao wa kike kuyapenda masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hesabu ( STEM) badala ya kuliachia jukumu hilo serikali au walimu. Alikuwa akizungumza katika mkutano wa pembezoni ulioandaliwa kwa pamoja kati ya Tanzania, Uingereza na Kampuni ya Kimataifa ya GlaxoSmithkline ili kujadili fursa na changamoto za mwanafunzi wa kike katika masomo hayo, kulia kwa Katibu Mkuu ni Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Bibi. Irina Bokova ambaye alikuwa modereta wa majadiliano hayo na pia alielezea nafasi na Mchango wa UNESCO katika kumsaidia mtoto wa kike. Kushoto ni Balozi Ramadhan Mwinyi , Naibu Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Waziri wa Wizara ya Wanawake na Usawa wa Uingereza, Bibi, Maria Miller ( Mb) akielezea uzoefu wa nchi yake katika kuwahamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya STEM, kulia kwake ni Bibi Nicola Yates, Makamu wa Rais wa UK and Ireland Phamarceuticals na Meneja Mkuu wa GlaxoSmithkline. Nyuma ya Waziri Miller na anayefuatilia kwa makini majadiliano hayo ni Mwanamitindo Bi. Flaviana Matata ambaye pamoja na kujikita fani ya mitindo na ambayo imemjengea heshima kubwa, lakini pia kupitia Taasisi yake ya Flaviana Matata Foundation ameonyesha mapenzi makubwa ya kuwasaidia wanafunzi kuipenda shule na kudumu shuleni.
Makatibu Wakuu kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bibi. Asha Ali Abdullah ( Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto) na Bibi. Mwanaidi Salehe Abdulla ( Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amari) wakifuatilia majadiliano hayo kuhusu fursa na uwezeshaji wa wanafunzi wa kike kujiunga na masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hesabu.

sehemu wa washiriki wa Mkutano wa 58 wa Kamisheni kuhusu Hali ya Wanawake, walioshiriki majadiliano hayo ambapo pia walipata fursa ya kuchangia kwa kuuliza maswali meza kuu iliyowahusisha Katibu Mkuu, Anna Maembe, Mkurugenzi Mkuu UNESCO, Irina Bokova, Waziri Maria Miller ( Mb) na Nicola Yates Meneja Mkuu GlaxoSmithkline ambao ndio waliokuwa wazungumzaji wakuu.
Katibu Mkuu Maembe akipeana mkono na Waziri Miller ( Mb) mwishoni mwa mkutano huo wa pembezoni.

Na Mwandishi Maalum

 Tatizo la wanafunzi wa kike kutochangamkia au kuyapenda  masomo ya  sayansi,  teknolojia,  uhandisi na hisabati (STEM) ni tatizo linalozikumba  nchini  nyingi duniani  zikiwamo  zilizoendelea.

 Na kwa sababu hiyo imeelezwa kwamba,  ushirikiano wa karibu kati ya serikali kuu,  sekta binafsi, wazazi , walimu   na wanafunzi wa kike unahitajika  hivi sasa  kuliko wakati mwingine wowote  na hasa wakati huu ambapo  Jumuiya ya kimataifa inajipanga  na kuandaa ajenda mpya za  malengo ya  maendeleo endelevu baada ya  2015.

Hayo yamejitokeza siku ya jumatano   wakati wa  mkutano wa pembezoni ulioandaliwa  kwa pamoja kati ya Tanzania,  Uingereza na   Kampuni ya Kimataifa ya   GlaxoSmithkline  na kuwashirikisha  wajumbe wanaohudhuria  mkutano wa 58 wa Kamisheni kuhusu Hali ya  Wanawake unaoendelea   hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu, kutoka Wizara ya  Maendeleo ya Jamii,   Watoto na  Jinsai, Bibi Anna Maembe kwa upande wa Tanzania,  Bibi  Maria Miller ( Mb) Waziri wa Wanawake na  Usawa  kwa upande na Uingereza na Bibi. Nicola Yates Makamu wa Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Madawa ya  Uingereza na Ireland   na Meneja Mkuu wa GlaxoSmithkline ndio waliokuwa wazungumzaji  wakuu wa mkutano huo ambao  dhumuni lake lilikuwa ni  kutafakari,  kubadilisna uzoefu, changamoto na kutafuta mbinu zaidi za kuwasaidia wanafunzi wa kike kupenda STEM. 

Mkutano huo ambao ulivutia washiriki wengi  hadi wengine kukosa nafasi ya kuingia,   modereta wake alikuwa ni  Mkurugenzi  Mkuu wa UNESCO,  Bibi. Irina Bokova.

Akielezea  uzoefu wa Tanzania na changamoto zake katika eneo hilo , Katibu Mkuu Anna Maembe, amesema,   pamoja na kwamba serikali kuu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwamo sekta binafsi kuweka mifumo mbalimbali  inayolenga kuwasaidia na kuwahamasisha watoto wa kike  kuchangamkia masomo hayo  bado  safari ni ndefu.

Akasema changamoto kubwa ni katika eneo la ufuatiliaji  ili kubaini kama wanafunzi waliosaidiwa na kujengewa uwezo wamefikia wapi  katika masomo yao na baada ya kuhitimu je wanafanya kile walichosomea. 

Akaongeza kuwa itakuwa ni  kazi bure kama serikali peke yake itaachiwa jukumu hilo pasipo wazizi wenyewe  kuhamasika na kuwajengea mazingira mazuri watoto wao wakike tangu wakiwa na umri mdogo wa kuyapenda masomo hayo.

“Sisi katika Tanzania  tunaishukuru sana serikali kwa mchango wake wa kuwasaidia wanafunzi wa kike kujiunga na masomo ya sayansi, hesabu,  uhandisi na teknolojia, lakini  serikali peke yake haiwezi kufanya kila kitu,  nafasi ya wazazi ni muhimu sana sana” akasisitiza.

Akaongeza pia  kuwa  Tanzania inao wanawake ambao ni wahandisi, wataalamu waliobobea katika  ufundishaji wa hesabu,  sayansi na  hata utafiti na wengine wanaongoza  Idara za Serikali au kampuni binafasi.

Akasema  hao wote wanaowajibu wa kujitokeza ili kutumia uzoefu wao kuwahamasisha wanafunzi wa kike kufikia pale walipofika wao.
Naye Waziri  wa Uingereza yeye alisema,  hata katika nchi yake, bado wanafunzi wengi wa kike hawapendi masomo hayo, na hata kama wakiyasoma, si wote waoishia kufanya kazi walizosomea.

Akasisitiza haja na umuhimu wa sekta binafsi  kusaidiana na serikali  katika eneo hilo na pia  umuhimu wa watoto wa kike kuhamasishwa na kujengewa uwezo wakiwa wangali wadogo ili kutambua vipaji  vyao.

Naye   Makamu Rais   na  Meneja Mkuu wa  GlaxoSmithKline yeye aliainisha program mbalimbali ambazo kama  sekta binafsi imekuwa ikichangi katika eneo hilo.

Akasema  uzoefu uonyesha kuwa  watoto wa kike wakiwezeshwa na kuhamasishwa wakiwa wangali wadogo wanayofursa kubwa ya kupenda hesabu, sayansi, uhandisi na  masuala ya teknolojia. Na pia inakuwa hamasa kwao wakiwaona wanawake waliofanikiwa katika  maeneo hayo.