Mtendaji
Mkuu Bodi ya Filamu Bi. Joyce Fisoo akiwasilisha Rasimu ya awali ya
Sera ya Filamu wakati wa moja ya kikao cha wadau cha kujadili rasimu ya
awali ya Sera ya Filamu kilichofanyika hivi karibuni, kulia ni
Mkurugenzi msaidizi kutoka Idara ya Sera na Mipango Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Verediana Mushi, na Kushoto ni mdau wa
filamu Bw. John Kitime.
Wadau
mbalimbali wa tasnia ya filamu wakijadiliana wakati wa kikao cha wadau
cha kujadili rasimu ya awali ya Sera ya Filamu kilichofanyika hivi
karibuni. (Picha na Genofeva Matemu).
Na: Genofeva Matemu – Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WHVUM
Serikali
ya Tanzania imejipanga kuendeleza kwa dhati TASNIA ya Filamu ili kuwa
chanzo kikubwa cha ajira kwa wasanii na pia kuongeza uchumi wa nchi.
Ni
dhahiri kuwa sekta ya filamu ni njia madhubuti ya kutambulisha jamii
kiutamaduni, kisiasa na kijamii na pia katika kukuza na kuongeza fursa
za nchi katika uwekezaji na utalii.
Filamu
na Makala za Filamu zikitumika vizuri zitaweza kuhamisha na kuondoa
tofauti mbalimbali zilizopo ndani ya jamii na hivyo kuongeza umoja na
mshikamano baina ya watu wa makabila na watu wenye asili mbalimbali,
hivyo kuutambulisha utamaduni wa Mtanzania.
Kazi
na shughuli za Filamu nchini zimekuwa zikisimamiwa na Sera ya Utamaduni
ambayo ilitayarishwa na kupitishwa mwaka 1997 pamoja na Sheria ya Filamu
na Michezo ya Kuigiza na 4 ya mwaka 1976.
Katika
kipindi cha kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 2013 kumekuwepo na maendeleo
makubwa katika Tasnia ya Filamu nchini hivyo kuisababishia Sera ya
Utamaduni ya Mwaka 1997 kutokidhi baadhi ya mahitaji ya tasnia ya filamu
na kupelekea mahitaji ya kurekebisha Sera ya Utamaduni kama Sera mama
na kutungwa kwa Sera ya Filamu.
Mnamo
Desemba 12 mwaka 2013, wadau mbalimbali kutoka Wizara ya Habari,Vijana
Utamaduni na Michezo, Bodi ya Filamu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi walishiriki katika kikao cha wadau
cha kujadili rasimu ya awali ya Sera ya Filamu.
Wadau
wengine ni Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Kazi na Ajira,
BASATA, Idara ya Sanaa na Sanaa za Maonyesho, Chuo Kikuu cha Dar Es
Salaam, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Mtandao wa Muziki, Swahili Films,
ROSAF, TAPAF, Umoja wa Mashirikiano wa Filamu, Filamu Cental, Chama cha
Hakimiliki Tanzania, Shirikisho la Sanaa za Maonyesho pamoja na G&S
Associates and Advocates.
Hata
hivyo wadau ambao hawakushiriki walipewa nafasi na Serikali kuwasilisha
maoni yao ambapo mwitiko umekuwa mzuri na maoni yanaendelea kupokelewa
ili hatimaye kuwa na Sera bora na shirikishi.
Katika
kikao hicho Rasimu ya awali ya Sera ya Filamu iliwasilishwa kwa
kuelezea historia fupi ya filamu nchini, vikao vya wadau vilivyofanyika
vya mapendekezo ya kuwa na Sera ya Filamu kati ya mwaka 2004 na 2013,
nyaraka kama Mpango Mkakati wa Bodi ya Filamu unaoonyesha haja ya kuwa
na Sera ya filamu pamoja na kuelezea malengo mahususi na matamko ya Sera
mpya inayopendekezwa kutungwa.
Aidha,
wadau walijadili uzoefu wa nchi nyingine kama Kenya, Nigeria, China,
Afrika Kusini, Marekani, Canada, India na Uingereza na matokeo ya tafiti
mbalimbali zilizofanyika pamoja na Changamoto zinazoikabili Tasnia ya
Filamu nchini.
Miongoni
mwa mapendekezo yaliyotolewa na wadau ni pamoja na kuwa Sera itamke
uanzishwaji wa Chuo cha Taifa cha Filamu, Sera itamke kuwepo kwa Mfuko
ambao utasaidia katika kuimarisha Sekta ya Filamu na Sanaa za maonyesho
kwa ujumla, Sera itoe tamko kuhusu kusimamia maadili katika tasnia ya
Filamu na kudhibiti ukatili wa kijinsia katika tasnia ya Filamu.
Pia
walipendekeza kuwa hoja na matamko yawe na takwimu zaidi, Sera itamke
namna ya kumlinda msanii wa Tanzania, mzalishaji wa ndani na wawekezaji,
pamoja na kupiga vita udhalilishaji wa watoto wa kike.
Kwa
upande mwingine, wadau hao walitoa pongezi kwa Wizara kwa kuandaa Rasimu
ya awali ya Sera ya Filamu iliyotokana na maoni mbalimbali ya wadau,
Sera ambayo itaiwezesha Tasnia ya Filamu kupata mwelekeo bayana na
kukidhi matakwa ya kila mdau katika tasnia ya filamu.
Wizara
inapenda kuujulisha umma kuwa imekua na inaendelea kushirikiana na
wadau wa Filamu kwa kila hatua ili hatimaye ifanikishe azma ya kuwa na
nyaraka zote muhimu katika kuendeleza, kusimamia, kuratibu na kukuza
tasnia ya filamu nchini.
0 comments:
Post a Comment