Kijana
Hafidh Masokola
AMA kweli hujafa, hujaumbika. Usemi huu una maana kubwa kwa kijana
Hafidh Masokola, mkazi wa eneo la National Housing mjini hapa ambaye kwa
miaka zaidi ya 40 alikuwa na ngozi isiyo na chembe ya tatizo, lakini
sasa amegeuka albino. Kwa mujibu wa Masokola, ambaye sasa ana umri wa
miaka 47, alipata tatizo hilo kutokana na madhara ya dawa ya malaria
aliyoimeza aina ya Metakelfin miaka minne iliyopita.
Na kutokana na tatizo hilo la kiafya lililobadilisha kabisa ngozi
yake, amelazimika kujiunga na Chama cha Maalbino Tanzania. Masokola,
mwenye mke na watoto watatu, anasema alipata uthibitisho wa kuathiriwa
na aina hiyo ya dawa baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara katika
hospitali kadhaa, ikiwemo ya KCMC iliyopo Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Katika mazungumzo na gazeti hili hivi karibuni, kijana huyo alisema
aina hiyo ya dawa ilimponza kwa kunywa vidonge vitatu tu katika dozi
yake ya kwanza mnamo Julai mwaka 2010. Akisimulia zaidi, alisema; “Baada
ya kupima malaria katika hospitali ya mkoa ya Kitete, nilikwenda duka
la dawa na kununua hii Metakelfin, sikuwahi kutumia dawa nyingine kabla
ya hapo.
“Hata kabla sijarudia dozi ya pili ambayo huwa ni baada ya siku saba,
damu ilianza kuvilia kwenye nyayo za miguu na viganja vya mikono.
Nikalazimika kwenda tena hospitali ya mkoa kwa ushauri wa daktari wangu,
George Msalale, nikaambiwa nitumie mafuta mazito kukabili mzio wa dawa.
“Sikuwa nawashwa, ila hali hii ya maumivu iliendelea kwa takribani
wiki nne. Hali ya kuvilia damu ikasambaa katika sehemu nyingine za mwili
huku ikianza kutoa madoadoa. Aidha, ngozi ilianza kubadilika ikawa na
makunyanzi na kavu, ikanibidi niwe mtu wa kutembea na mafuta mazito ya
Vaseline ili nijipake mara kwa mara.” Anasema pamoja na juhudi hizo,
hali haikubadilika na akaongeza kutumia losheni aina ya “hydrocortisone
cream”.
“Baada ya kutumia mafuta na cream hiyo, ngozi ilibadilika rangi na
kuwa nyeusi, iliyopauka kama mtu aliyemwagiwa gundi. Lakini mabadiliko
hayo hayakuathiri sehemu zake za nywele licha ya nyayo na viganja
kukakamaa mithili ya magome ya mti. Macho pia yaliathirika kwa kupunguza
nuru ya kuona, nikawa naona ukungu zaidi, huku nikiwa na homa za mara
kwa mara,” anasema.
Kutokana na hali hiyo, aliendelea kupata ushauri kutoka kwa wataalamu
wa afya ambapo walimbadilishia dawa na kumpa shampoo ya kuoga
iliyomsaidia kuondoa magamba kwenye ngozi yake ingawa aliendelea kuwa na
mabaka meusi na meupe.
Aidha, katika kipindi hicho anasema; “midomo yake ilipasuka pasuka
nikawa nashindwa kula chakula vizuri na wakati mwingine ilibidi kutumia
tishu au kitambaa kuzuia damu iliyokuwa ikitoka mdomoni wakati wa kula.”
Pamoja na kupasuka kwa midomo, nywele zake pia zilianza kukatika na
kung’oka huku kichwa kikiwa na kitu mithili ya ukoko na kutoa vidonda
vyenye maji. Na kufikia Januari mwaka 2011, mara nyingi akikumbana na
maumivu ya kichwa mara kwa mara, alijikuta hana nywele kabisa na badala
yake kichwa kikifunikwa na ngozi iliyokakamaa.
Kutokana na hali kuzidi kuwa mbaya, anasema alilazimika kurudi tena
hospitali ya Kitete alikoshauriwa kutumiwa sabuni za ngozi na losheni
aina ya “beta cort- N” anayosema ilimsaidia kuondoa ngozi ngumu na
kuotesha nywele, lakini zikiwa nyeupe badala ya nyeusi kama alizokuwa
nazo kabla ya kuugua malaria.
“Na ngozi yangu yote ya mwili ilipoteza vinyweleo na kubadilika rangi
kutoka ya asili niliyokuwa nayo na kuwa nyeupe kama ya mzungu. Hapo
ikabidi nilazwe kwa uchunguzi wa kina hapo hospitali ya rufaa ya mkoa wa
Tabora. Mambo yalikuwa magumu, nikaandikiwa rufaa kwenda KCMC kwa
uchunguzi zaidi.
“Agosti 22 ya mwaka 2011 niliwasili KCMC na kuanza matibabu baada ya
kufanyiwa vipimo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kukatwa sehemu ya nyama
ya paja kwa uchunguzi. Vipimo vilionesha nimepatwa na madhara ya dawa
nilizotumia na kupata ugonjwa aina ya “Psonasis” ambao umesababisha
kupoteza rojo chembe yaani “melanin” inayosababisha kupotea kwa rangi ya
ngozi.
Mimi nilipoteza rangi nyeusi na kupata huu ualbino,” anasema na
kusisitiza kuwa, hakuwahi kutumia dawa nyingine zaidi ya Metakelfin.
Kutokana na kubainika kwa tatizo lake, alishauriwa kutumia mafuta
maalumu kwa lengo la kutakatisha ngozi, huku akielezwa kuwa kama
akifuata ushauri, baada ya muda ngozi inaweza kurudi katika hali yake ya
asili.
“Nilipotumia mafuta hayo mazito, magamba yaliyokuwa kwenye ngozi
taratibu yaliondoka na kubaki na ngozi nyeupe. Kucha za mikono na miguu
zilizokuwa zimeng’oka na ngozi za nyayo za viganja vilianza
kujitengeneza upya,” anaeleza.
Anaongeza kuwa, akiwa KCMC alipatiwa elimu ya kutunza ngozi kutokana
na michubuko na kujikinga mionzi ya jua ambayo inaweza kumsababishia
saratani ya ngozi.
Anasema alielimishwa namna ya kutumia losheni za aina mbalimbali ili
kutunza ngozi ikiwa ni pamoja na “betamethasone cream au beta cort- N
ambapo kwa sasa anatumia Sun block- SPF 60 cream, pia anatumia mafuta ya
Vaseline yenye mchanganyiko wa vitamin A na vidonge vya vitamin A.
Aidha, anatakiwa kuhudhuria kliniki maalumu ya ngozi katika hospitali
ya KCMC mara moja kwa mwaka. Akizungumzia athari anazozipata kutokana
na ulemavu wa ngozi alioupata akiwa mtu mzima, anasema kuwa ni pamoja na
unyanyapaa na kushindwa kufanya shughuli zake za ujasiriamali ambazo
kwa sehemu kubwa alikuwa akizifanya akiwa juani.
Kwa sasa, muda wake mwingine anautumia kuwa muelimishaji wa VVU na
Ukimwi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tabora huku pia akiutumia
muda wake mwingine katika shughuli za chama cha albino wilayani Uyui,
Tabora.
Anasema lengo lake kubwa ni kuendeleza harakati za kuelimisha umma
kutambua thamani ya utu wa binadamu kwani hakuna ajuae ni lini ataingia
kwenye kundi la watu wenye ulemavu. Baba huyo wa watoto watatu, Juma
(20), Sizya (16) na Radhia (15) aliozaa na mkewe Hanzelani Kauzu,
anasisitiza; “Mungu amenichagua mimi kuwa mfano kwa watu wengine ambao
wanaendeleza mauaji kwa albino, kwani hata wao wanaweza kubadilika na
kupata ulemavu wa ngozi kama yeye na kwamba hakuna haja ya kufanya
mauaji ya albino.”
Mkewe ameizungumzia hali ya mumewe kuwa ni changamoto kubwa kutokana
na baadhi ya watu kuihusisha na imani za kishirikina, huku akisisitiza
kama familia wamekubaliana nayo na wako imara katika kuhakikisha maisha
yanaendelea kama ilivyokuwa kabla ya ulemavu wa mumewe.
Akiizungumzia hali hiyo, mmoja wa madaktari bingwa nchini, Dk Ali
Mzige alisema matukio ya aina hiyo yapo. Dk Mzige aliyewahi kuwa Mganga
Mkuu wa Wizara ya Afya, alisisitiza kuwa Metakelfin na dawa nyingine
zenye salfa huwa na madhara kutegemea na mtu na mtu.
Alisema wakati mwingine hutegemea na afya ya mtu na historia ya
magonjwa mbalimbali. Hata hivyo, alishauri kwa yaliyomkuta Masokola, ni
vyema akazingatia ushauri wa madaktari, huku akimtaka kutopuuzia
matumizi ya losheni na kufanya mazoezi ili kujikinga na uwezekano wa
kupata ugonjwa wa saratani.
HABARI KWA HISANI YA HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment