SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Thursday, December 26, 2013

Wadau wa michezo zanzibar watoa vifaa vya michezo kunogesha sherehe za miaka 50 ya mapinduzi

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akipokea vifaa mbali mbali vya michezo kutoka kwa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Hassan and Sons kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake Mhe. Mohamed Raza kusaidia mashindano ya Kombaini  za wanafunzi wa Wilaya 10 za Zanzibar kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Baadhi ya vifaa na vyakula vilivyotolewa na Kampuni za Hassan and Sons, Zat pamoja Zanzibar Ocean View hapo Wizara ya Elimu Maziri kusaidia mashindano ya Kombaini za wanafunzi wa skuli za Zanzibar.

Seti za Jezi tofauti zilizotolewa na wafanyabiashara kwa ajili ya wanamichezo watakaoshiriki mashindano ya Kombani za Maskuli ya Zanzibar yanayotarajiwa kuanza rasmi tarehe 29 mwezi huu katika uwanja wa Uzini Wilaya ya Kati
Baadhi ya walimu wa skuli mbali mbali nchini walioshiriki hafla ya makabidhiyano ya vifaa mbali mbali vitakavyotumika kwa ajili ya mashindano ya Kombaini za Maskuli Nchini.
Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Hassan and Sons Mhe Mohamed Raza  akimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa ajili ya kutumika katika mashindano ya kombe la Mapinduzi yanayotarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki hii.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali akizungumza mara baada ya kupokea msaada wa vifaa mbali mbali kwa ajili ya mashindano ya kombe la Mapinduzi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kombe la Mapinduzi ambae pia ni Mwenyekiti wa BTMZ Ssharifa Khamis akitoa shukrani zake mara baada ya kupokea msaada wa vifaa mbali mbali kwa ajili ya mashindano ya kombe la Mapinduzi. 
Picha na Hassan Issa wa  OMPR, ZNZ.
--------------------------------------------
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar  imedhamiria kufufua upya vugu vugu la michezo Nchini ili kuirejeshea hadhi yake Zanzibar katika Nyanja za Michezo Kimataifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo katika hafla fupi ya kukabidhiwa  vifaa vya michezo pamoja na vyakula kwa ajili ya washiriki wa mashindano ya Kombaini za wanafunzi za Wilaya 10 za Zanzibar kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar hafla iliyofanyika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema  heshima ya Zanzibar  kimichezo lazima  iwepo kwa kuhakikisha  Vijana wanaandaliwa vyema Maskulini ambako ndiko kunakopatikana  vipaji vya michezo mbali mbali vinavyoweza kuirejeshea heshima yake Zanzibar.

Alifahamisha kwamba jamii popote pale hapa Nchini inahitajika kuongeza ari ya kuwaamsha vijana kwenye mitaa yao katika kupenda na hatimae kushiriki kwenye michezo tofauti kulingana na uwezo wa vijana wenyewe.

“ Zanzibar inaweza kurejea tena katika hadhi yake ya kimichezo Kimataifa kama mpango utakaoandaliwa wa kuamsha vugu vgugu la michezo utapokelewa vyema katika maskuli mbali mbali hapa nchini “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  aliupongeza Uongozi wa  Kampuni ya Hassan and Son’s, Zat pamoja na ule wa Zanzibar Ocean View kwa uwamuzi wao wa kuchangia  sekta ya michezo nchini mbali ya kudumisha ushirikiano lakini pia husaidia kutoa ajira kwa wanamichezo nchini.

Akitoa Taarifa ya mashindano hayo ya Kombaini za wanafunzi za Wilaya 10 za Zanzibar kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar Mkuu wa kitengo cha michezo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mussa Abdullrabi Fadhil  alisema lengo la mashindano hayo ni kuibua vipaji vya vijana maskulini.

Abdullrabi Fadhil alisema tafiti zinaonyesha kwamba vipaji vingi katika sekta za michezo mara nyingi hupatikana miongoni mwa wanafunzi katika skuli mbali mbali hapa nchini.

Alieleza kwamba mashindano hayo yataoshirikisha michezo tofauti ikiwemo soka, Wavu, mchezo wa Bao, Pete pamoja na Table Tennis kwa kujumuisha wanafunzi wa unguja na pemba yanatarajiwa kufunguliwa rasmi  Tarehe 29 Disemba mwaka huu wa 2013 katika uwanja wa michezo wa Uzini Wilaya ya Kati na kumalizika tarehe 5 Januri mwaka 2014.

Mapema Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Hassan And Sons Mohd Raza kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake waliochangia vifaa hivyo vya michezo pamoja na vyakula alisema Serikal lazima iungwe mkono na wafanyabiashara pamoja na wananachi katika kusaidia kupunguza au kuondoa kabisa kero zinazoikabili jamii.

Alisema utaratibu huo kwa njia moja utaiwezesha Zanzibar  kurejea katika heshima yake kimichezo iliyokuwa ikitambulikana katika sehemu mbali mbali ulimwenguni.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amepokea vifaa vya michezo kwa ajili ya kuchangia maandalizi ya mashindano ya kombe la mapinduzi linalotarajiwa kushirikisha Timu 12 za soka za kitaifa na kimataifa pamoja na timu 27 za michezo mengine ya ndani.

Vifaa hivyo vilivyojumuisha vikombe vitatu kwa washindi wa mwanzo, medani, T. Shirts, Redio maalum kwa Mchezaji, mfungaji na Kipa bora wa mashindano hayo vimetolewa kwa pamoja na Kampuni ya Hassan and Sons, Zat pamoja na Hoteli ya Zanzibar Ocean View.

Akipokea vifaa hivyo hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliupongeza uongozi wa Makampuni hayo kwa michango yao hiyo itayosaidia kufanikisha vyema mashindano hayo.

Balozi Seif alisema michango ya uongozi wa Kampuni hiyo italeta changamoto kubwa kwa wanamichezo kuweza kujikita zaidi katika hamasa ya kuendeleza vyema mashindano hayo ya kimataifa kwa mwaka huu.

Mapema Mwakilishi wa makampuni hayo ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mohd Raza aliahidi kwamba yupo tayari wakati wowote kutoa mkopo wa dharura endapo yatajitokeza mapungufu wakati wa maandalizi ya sherehe hizo za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia Nusu Karne.

Alisema yeye kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake wakati wowote wataendelea kuiunga mkono Serikali kuu katika kutoa michango na misaada itayosaidia kupunguza  matatizo yanayowasumbua wananchi.

Akipokea vifaa hivyo Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kutafuta fedha kwa ajili ya kufanikisha mashindano hayo ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar Sharifa Khamis aliwakumbusha wafanyabiashara nchini kuiangalia pia michezo ya ndani katika misaada wanayotoa ili kwenda sambamba na ule mchezo uliozoelewa wa soka.

Timu kadhaa za mchezo wa zimeshathibitisha kushiriki mashindano hayo miongoni mwao zikiwemo timu za soka za Yanga , Simba na Azam za Tanzania Bara, timu za Nchi jirani za Afrika Mashariki, Ikiwemo Sudan ya Kusini, China pamoja na Vietnam.
 
Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

26/12/2013.

0 comments:

Post a Comment