Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zitto Kabwe
----
Kwa wiki ya tatu mfululizo kumekuwa na
malumbano kuhusiana na suala la ujenzi wa Bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar
es Salaam. Kumekuwa na madai yenye nguvu ya hoja kutoka kwa wananchi wa Mtwara
dhidi ya porojo kutoka kwa viongozi wenye dhamana ya kujibu madai haya ya watu
wa Mtwara. Watu wa Mtwara kwa umoja wao na kwa kuungwa mkono na viongozi wa
dini zote wamekuwa wakitaka Serikali ifikirie upya suala la mradi wa ujenzi wa
Bomba la gesi na badala yake kujenga mitambo ya kufua umeme mkoani Mtwara na kusafirisha
umeme huo kwenda maeneo mengine ya nchi. Kwenye moja ya maandishi yangu
(Serikali iwasikilize watu wa Mtwara) nimeshauri kuwa Taifa liwe na gridi
nyingine ya Taifa ambayo itatokana na Gesi tu na ianzie Mtwara.
Ikumbukwe kwamba katiba ya nchi, ibara ya 9
katika mabano J inataka mamlaka ya dola na vyombo vyake vyote kuhakikisha ya
kwamba shughuli zote za kiuchumi zinaendeshwa kwa namna ya kwamba pasiwe
mrundikano wa utajiri au shughuli za uzalishaji kwa watu wa chache. Katiba
inaendela kwa kuelekeza kwamba uchumi wa nchi upangwe katika uwiano sawia (9,
d). Watu wa Mtwara wanatekeleza matakwa haya ya katiba kwa kukataa mrundikano
wa shughuli za kiuchumi wa nchi na utajiri wa nchi kua kwenye mikoa michache na
hasa mkoa wa Dar-Es-Saalam.
Serikali imekuwa ikitoa majibu ya porojo na
kuwatusi watu wa Mtwara na kama ilivyozoeleka Rais Jakaya Kikwete na Mawaziri
wake wamekuwa wakisema suala la Mtwara linatumika na wanasiasa kujitafutia
umaarufu. Inasikitisha sana kuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwaambia
mabalozi wa nchi za kigeni waliopo hapa nchini kuwa yanayoendelea mkoani Mtwara
yanachochewa na Wanasiasa tuliosimama na wananchi wanaodai haki ya kufaidi
utajiri wa nchi yetu. Rais Kikwete na Mawaziri wake wameshindwa kabisa
kuonyesha uongozi katika suala hili na hatimaye kuhatarisha umoja wa kitaifa.
Kwa udhaifu wa serikali na tabia ya kutafuta
mchawi badala ya kutatua tatizo la msingi, wananchi wameendelea kukutana na
hata wengine sasa kuanza kusambaza ujumbe wa kukata kipande cha nchi na kuanzisha
Jamhuri ya Kusini. Nimeona kwenye mabango ya mkutano wa hadhara uliofanyika
19/1/2013 wananchi wakibeba mabango yanayoaishiria kuchoka kuwa sehemu ya
Tanzania na kuanzisha Jamhuri ya Makonde kuanzia jiwe la Mzungu wilayani Kilwa
mpaka mto Ruvuma. Haya yanatoka na kiburi cha Serikali kujishusha na
kuwasikiliza wananchi wanao dai haki yao ya kikatiba.
Ni Serikali iliyokosa uhalali wa kutawala
inayoweza kudharau hisia hizi za wananchi. Serikali ielewe kwamba kamwe
haitaweza kulinda kila nchi ya bomba hili iwapo italijenga kwa nguvu. Badala ya
kuzungumza na vyombo vya habari Serikali ifanye mazungumzo na wananchi wa
Mtwara na kukubaliana na matakwa yao. Kitendo cha Serikali kung’ang’ania
msimamo wake dhidi ya watu wa mtwara ni kitendo kinacho weza kuipasua nchi na
hivyo kwenda kinyume na masharti ya katiba ibara ya 28 ambayo inasema: “kila
raia ana wajibu wa kulinda uhuru wa nchi, uhuru mamlaka na umoja wa
taifa.”ibara ya 28, 1.
Inawezekana Serikali inaogopa kuvunja
makubaliano na Wachina ya mkopo wa dola za kimarekani 1.2 bilioni ambao
imeuingia bila hata kushirikisha Bunge. Inawezekana Serikali na hasa watendaji
wa Serikali waliojadili mkopo huu wameshapata chao na hivyo kuogopa kusikiliza
madai halali ya wananchi. Lakini yote hayo hayawezi kuwa zaidi ya Umoja wa nchi
yetu. Hatuwezi kukubali nchi yetu ipasuke vipande vipande kwa sababu tu ya
kulinda mkataba wa bilioni 1.2 tuliokopa China, ambayo serikali inang’ang’ania.
Tunafahamu kwamba ubalozi wa China umeandika
barua serikalini kuwaondoa raia wa China waliopo Mtwara kwa hofu ya maisha yao.
Serikali inaficha ukweli huu kama ilivyoficha ukweli kwamba Naibu Waziri wa
Nishati na Madini bwana George Simbachawene alifukuzwa na wananchi wa Mtwara
alipokwenda hivi majuzi. Serikali itaficha ukweli mpaka lini? Lazima tupate
majawabu.
Kwanza Serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi
wa Bomba hili. Kamati ya Bunge ya POAC ilipokuwa inapitia mahesabu ya TPDC
iliomba mkataba na kwa mshangao mkubwa wabunge wakaambiwa Mkataba haupo TPDC
bali upo Wizarani. Kwa nini Mkataba huu wa matrilioni ya Fedha unafichwa?
Mkataba huu ulisainiwa pamoja mikataba mingine 2, mmoja wa kujenga nyumba za
wanajeshi wa thamani ya dola za kimarekani 400 milioni na mwingine wa
mawasiliano jeshini wa dola za kimarekani 110 milioni, na mikataba yote mitatu
imesainiwa kimya kimya bila kushirikisha wananchi kupitia Bunge. Lazima
mikataba yote hii iwekwe wazi.
Pili, Mkataba huu uchunguzwe kama unalingana
na thamani ya fedha maana kwa utafiti wa awali inaonyesha kuwa bei ya ujenzi wa
bomba imepandishwa maradufu. Wastan wa kujenga bomba
la gesi duniani ni dola za kimarekani 1.2 milioni kwa maili moja. Mradi huu wa
Tanzania utagharimu dola za kimarekani 2.2 milioni kwa kilomita moja (maili 1
ni sawa na kilomita 1.6).
Tatu, Serikali ibadilishe
Mkataba huu kuwa wa mkopo wa kujenga Mitambo ya kufua umeme Mtwara na ujenzi wa
Msongo wa Umeme kama gridi ya pili ya Taifa. Kwa sasa Tanzania ina gridi moja
ambayo inabebwa na bwawa la Mtera linalo tegemea mto Ruaha ambao hivi sasa
unakauka miezi 5 katika miezi 12 ya mwaka. Ni dhahiri kwamba kwa usalama wa
Taifa na hata kwa gharama Nchi itafaidika zaidi kwa kujenga gridi nyingine
kutokea Mtwara badala ya kusafirisha gesi kuja Dar-Es-Salaam.
Serikali haitashinda vita
hii kwa kuzusha kwamba ama wanasiasa wanaopinga wanatumika na makampuni mengine
au kwa mataifa ya magharibi kutaka kuvuruga nchi. Serikali ijitazame yenyewe. Bila
kufanya hayo tunayo pendekeza hapo juu, wananchi wataendelea kupigania hako
yao. Hii ni vita ya uwajibikaji. Wananchi wanataka kufaidika na rasilimali za
nchi yao. Kwa vyovyote vile upande wa wananchi utashinda. Vita ya uwajibikaji
kwenye rasilimali za nchi sio ya vyama vya siasa, ni vita ya wananchi. Chama
cha siasa kitakachokwenda kinyume na matakwa ya wananchi, kinajichimbia kaburi.
Zitto Kabwe
0 comments:
Post a Comment