SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Wednesday, January 25, 2012

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Aagana na Mabalozi na Aipongeza Benki ya Kiislamu (IDB)

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Mabalozi sita wapya walioteuliwa kuiwakilisha tanzania katika mataifa mbali mbali duniani.
Meneja Wa Benki Ya Maendeleo Ya Kiislamu {idb } Bwana Malik Shah akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { idb } uliofika ofisini kwake kuzungumza naye. IDB ni miongoni mwa benki inayofadhili wanafunzi wa kitanzania kupata elimu ya juu katika mataifa ya mashariki ya kati.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi wapya sita wlioteuliwa hivi karibuni.
*****
Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { IDB } imepongezwa kwa jitihada zake za kusaidia ufadhili kwa Wanafunzi wa Tanzania wanaopata fursa ya masomo ya juu katika Vyuo vikuu vya Mataifa ya Mashariki ya Kati.
Pongezi hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya mazungumzo na Ujumbe wa Benki hiyo ukiongozwa na Meneja wake Bwana Malik Shah hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Seif alisema Hatua ya Benki hiyo inafaa kuungwa mkono na Taasisi nyengine katika dhana ya kuona kizazi cha sasa kinapata taaluma ya kina kulingana na mabadilio ya Sayansi na Teknolojia Duniani.
“ Nimeshuhudia harakati za Wanafunzi wa Kitanzania katika miaka ya 80 wakipatiwa viza Mjini Nairobi kupitia ufadhili wa Benki hiyo, wakati huo mimi nikifanya kazi katika Taasisi ya Mambo ya nje ya Tanzania ”. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuelezea ujumbe wa Benki ya Maendeleo ya Kiislam kwamba licha ya Tanzania ikiwemo Zanzibar kwa jumla kuendelea kuongeza vyuo vikuu lakini bado wimbi la wanafuzi wanao sifa za kujiunga na vyuo hivyo ni kubwa.
Balozi Seif aliushauri Uongozi huo kuendelea kuongeza fursa zaidi wakilenga pia Fani ya sayansi ambayo inaonekana kukosa Wataalamu.
“ Tunahitaji nafasi za masomo zaidi katika fani ya sayansi kwa vile bado Taifa linaendelea kuhitaji Wataalamu wa fani hiyo ”. Alisisitiza Balozi Seif.
Naye Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kiislamu Bwana Malik Shah ameahidi Taasisi yake kuendelea kusaidia ufadhili wa Masomo ya juu kwa Wanafunzi wa Zanzibar.
Bwana Malik alimueleza Balozi Seif kwamba sulala la Wanafunzi wa Zanzibar ataliwasilisha kwenye uongozi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi hiyo kwa kuchukuliwa hatua zaidi.
Benki ya Mendeleo ya Kiislamu { IDB } imekuwa ikitoa ufadhili kwa Wanafunzi wa Kitanzania kupata elimu ya juu katika Mataifa ya Malaysia, Turky na Jordan.
Mapema mchana Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Mabalozi wapya sita walioteuliwa hivi karibuni kuiwakilisha Tanzania katika Mataifa mbali mbali Duniani.
Mabalozi hao ni Dr. Batilda Buriani anakwenda Nchini Kenya, Balozi Shamim Nyanduga anakwenda Msumbiji, Balozi Grace Majuma anaenda Zambia, Dr. Ladislaus Komba anakwenda Uganda Uganda, Dr. Deodorus Kamala anaenda Ubelgiji na Balozi Philip Marmo anaenda China.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Mabalozi hao kwamba changa moto kubwa inayowakabili ni kuhakikisha wanasimamia uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Nchi wanaozozisimamia.
Aliwataka kufuatilia kwa kina makubaliano au mikataba iliyopo kati ya pande hizo mbili ambayo wataikuta haijatekelezwa.
Balozi Seif alielezea faraja yake kutokana na Nchi zote sita kuwa na uhusiano mzuri na Tanzania kinachohitajika zaidi kwao ni ustahamilivu katika kutekeleza majukumu yao waliyopangiwa..
Akitoa shukrani kwa niaba ya Mabalozi wenzake Balozi Grace Mujuma ambaye ameteuliwa kuiwakilisha Tanzania Nchini Zambia alisema hivi sasa wana deni kubwa la kwenda kutekeleza jukumu walilopangiwa na Taifa.
Balozi Grace alisisitiza kwamba wanaahidi suala la kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Nchi wanazokwenda kutekeleza kazi zao litapewa nafasi kubwa zaidi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
24/1/2012.

0 comments:

Post a Comment