SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Monday, August 30, 2010

Sarrazin akosolewa vikali

Mwanachama wa Bodi ya Benki Kuu ya Ujerumani, Thilo Sarrazin.

Thilo Sarrazin,mwanachama wa Bodi ya Benki Kuu ya Ujerumani, amekosolewa vikali na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani,Guido Westerwelle na Baraza Kuu la Wayahudi kuwa anachochea ubaguzi na chuki dhidi ya Uyahudi.

 Chama cha SPD hakimtaki tena kama mwanachama na viongozi wa SPD wametoa mwito kwa Sarrazin kuondoka chamani. Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, amesema haiwezekani kabisa kuyakubali matamshi ya Sarrazin.

Kufuatia matamshi ya utata ya Thilo Sarrazin kuhusu wahamiaji wa Kiislamu nchini Ujerumani yaliyokosolewa vikali, sasa mwanachama huyo wa Bodi ya Benki Kuu ya Ujerumani "Bundesbank" na chama cha SPD, amekosolewa upya kwa maoni yake kuwa Wayahudi wana jeni ya aina moja.Vile vile amesema, wahamiaji wa Kiislamu barani Ulaya hawataki au hawawezi kujijumuisha katika jamii za nchi za magharibi.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel.Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema hayo ni matamshi yasiokubalika hata kidogo. Matamshi hayo yanavuka mpaka na yanaonyesha chuki dhidi ya makundi fulani katika jamii. Ubaya zaidi, Sarrazin anadai kuwa anashughulikia mada hiyo, lakini matamshi yake hayasaidii hata kidogo. Amesema:"Suala la kuwajumuisha wahamiaji ni mada iliyo muhimu sana katika jamii yetu. Nimewaalika ofisini kwangu wajumbe wanaoshughulikia mada hiyo na tumefanya kazi kubwa - na bado kuna kazi nyingi za kufanywa. Lakini vile anavyozungumza, atasababisha mgawanyiko katika jamii na hiyo itakwamisha majadiliano."Wakati huo huo, Naibu Kansela na Waziri wa Mambo ya Nje,Guido Westerwelle, amesema matamshi ya kuchochea ubaguzi au chuki dhidi ya Uyahudi hayana nafasi yo yote ile katika majadiliano ya kisiasa. Nae waziri wa ulinzi, Karl-Theodor zu Guttenberg, ameuliza iwapo Sarrazin anafaa kubakia katika Bodi ya Benki Kuu. Amesema, hata uchokozi una mipaka na ni dhahiri kabisa kuwa Sarrazin ameivuka mipaka hiyo kwa matamshi yake yasiofaa.Kilichozusha hasira ni matamshi mapya ya Sarrazin kuwa watu wenye asili mbali mbali wana jeni tofauti. Akawataja Wayahudi na Wabasque. Baraza Kuu la Wayahudi limesema, matamashi hayo ni chuki ya kibaguzi. Sasa hata katika chama cha SPD, sauti zinazidi kupazwa kupinga uanachama wa Sarrazin. Kiongozi wa SPD katika jimbo la Berlin, Michael Müller amesema, chama hakiwezi tena kumvumilia mwanachama anaekwenda kinyume na maadili ya chama chake. Viongozi wa ngazi za juu katika chama cha SPD wamemshauri Sarrazin kuondoka kwa hiyari, lakini mwanachama huyo amepinga pendekezo hilo.Mwandishi: Müller,Andrea/ZPR/P.Martin/RTRE

0 comments:

Post a Comment