Black Stars waaga Kombe la Dunia
Asamoah Gyan wa Ghana (kulia) akikosea mkwaju wa penalty wakati
wa robo fainali ya Kombe la Dunia, uwanjani Soccer City mjini
Johannesburg.
Pale mkwaju wa penalty wa Asamoh
Gyan katika dakika ya mwisho ya kipindi cha ziada ulipopaa juu ya lango
la Uruguay.....ilikuwa kama msumari wa moto katika nyoyo za Ghana na
Afrika kwa jumla.
Gyan ambaye goli lake safi dhidi ya Marekani liliwafikisha Black
Stars katika robo fainali ya dimba hili la kombe la dunia- alikuwa
nusura aandike historia nyingine- kuwaingiza Ghana katika nusu fainali.
Uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg ulianikizwa na milio ya
vuvuzela pale Sulley Muntari alipofunga bao la kwanza la Ghana katika
dakika za mwisho za kipindi cha kwanza. Black Stars walikuwa wameanza
vyema wakipania kuvunja historia kuwa timu ya kwanza kufika nusu fainali
ya Kombe la Dunia.
Kipa wa Ghana,Richard
Kingson (kushoto)na Diego Forlan wa Uruguay.
Lakini Uruguay
mabingwa mara mbili wa dunia- walirejea kwa kishindo na nyota wao Diego
Forlan, akasawazisha katika dakika ya 55. Huku muda ukiyoyoma na mikwaju
ya penalti ikinukia- Afrika ikapumua na kuingia matumaini pale Luis
Suarez alipotumia mkono kuzuia bao la pili la Ghana ambalo lilikuwa
liwafungishe virago Uruguay.
Saurez alipewa kadi nyekundu na Asamoh Gyan alikabidhiwa jukumu la
kufunga penalti- ambayo kama ingeingia basi Ghana ingekuwa timu ya
kwanza ya Afrika kufika semi fainali. Ghana baadaye ilipoteza mikwaju
miwili ya penalti- na Uruguay ikajikatia tiketi yake ya nusu fainali.
Mjini Accra- barabara za mji huo- zilikuwa tupu muda mfupi tu baada
ya Black Stars kushindwa katika mikwaju ya penalti. Raia waliokusanyika
katika mikahawa kuitizama mechi hiyo, nchini humo ingawa walivunjika
moyo, walisema wanajivunia jinsi Black Stars walivyoonyesha ustad´i na
uchezaji mzuri katika dimba hili la dunia.
"Ni hali ya kabumbu" wengine walisikika wakisema - "leo haikuwa
bahati yetu" - ndio msemo ulioenea nchini Ghana na Afrika nzima- ama
kweli Black Stars walikuwa wamebeba matumaini ya bara zima- ambalo kwa
mara ya kwanza lilikuwa na matumaini pengine wakati wetu ni sasa- kufika
angalau semi fainali za kombe la dunia.
Na kama mechi hiyo katika uwanja wa Soccer City ilikuwa ya aina yake-
robo fainali ya kwanza iliwaacha wengi mdomo wazi pale mabingwa mara
tano Samba wa Brazil walipoonyeshwa kidumbwedumbwe na Uholanzi. Wesley
Sneijder ndie alikuwa nyota wa Uholanzi huku Felipe Melo akiwa donda
sugu wa Brazil.
Wesley
Sneijder wa Uholanzi, baada ya kutia goli lililowafungisha virago
Brazil.
Sneijder ndie aliepiga pasi safi ambayo Melo aliingiza katika wavu wa
Brazil- kuisawazishia Uholanzi baada ya Robinho wa Brazil kutia bao la
kwanza. Sneijder baadaye alifunga bao la pili la Uholanzi ambalo
lilitosha kuwafungisha virago Brazil.
Cocha Dunga ambaye ameiongoza Brazil kwa miaka minne- alitangaza
kwamba muda wake madarakani umemalizika baada ya vijana hao wa Samba
kuyaaga mashindano ya Kombe la Dunia katika robo fainali.
Ilikuwa raha kwa Uholanzi ambao walishindwa na Brazil mara mbili
katika kombe la dunia. Mwaka wa 1994 Brazil iliitimua Uholanzi katika
raundi ya pili ya dimba- miaka minne baadaye Uholanzi tena ikapata
kichapo kutoka kwa Brazil katika robo fainali. Na leo, Uholanzi ilikuwa
na miadi ya kulipa deni.
Sasa Uholanzi itakutana na Uruguay jumanne ijayo katika nusu fainali
ya kwanza. Leo ni zamu ya Ujerumani na Argentina na mabingwa wa Ulaya -
Spain wana miadi na Paraguay- nafasi mbili za nusu fainali zitajazwa
usiku huu baada ya mechi hizi mbili.
Mwandishi: Munira Mohamed
0 comments:
Post a Comment