Mahakama nchini Afrika Kusini imemkuta na hatia
ya ufisadi aliyekuwa mkuu wa polisi Jackie Selebi.
Bw Selebi, aliyekuwa pia Rais wa idara ya polisi
ya kimataifa Interpol, alishutumiwa kwa kushiriki katika uhalifu na
kupokea rushwa yenye thamani ya dola za kimarekani 156,000.
Lakini mahakama ilimkuta hana hatia ya kupotosha
haki. Bw Selebi alikana mashtaka yote mawili.
Waandishi wanasema kesi hiyo iliyodumu kwa miezi
tisa imeonekana kuwa moja ya kesi muhimu tangu siasa za ubaguzi wa
rangi kumalizika nchini humo.
Bw Selebi mwenye umri wa miaka 60 sasa
anakabiliwa na hukumu ya takriban miaka 15 gerezani, japo atakuwepo nje
kwa dhamana mpaka hukumu yake itakapotolewa tarehe 14-15 Julai huku
akiwa nia ya kukata rufaa.
Mwandishi wa BBC mjini Johannesburg, Karen Allen
amesema kesi hiyo ilijaa mvuto na mchanganyiko.
Lakini mwisho wa siku, licha ya kuwa na uhusiano
na wanasiasa wengi, Selebi amepatikana na hatia.
' Mikoba ya wabunifu wenye majina maarufu'
Kwenye kiini cha madai hayo ulikuwepo uhusiano
wa Bw Selebi na mfanyabiashara wa dawa za kulevya aliyekutwa na hatia
Glen Agliotti, ambaye pia anashutumiwa kuhusika na mauaji ya
mfanyabiashara maarufu wa madini mwaka 2005, Brett Kebble.
Waendesha mashtaka wamedai Agliotti, ambaye pia
alikuwa akitoa taarifa kwa polisi, amelipa hongo na kutoa zawadi kwa
kamsihna wa taifa wa polisi Afrika Kusini (Saps) na badala yake Selebi
asishughulike kupambana na biashara ya dawa za kulevya.
Katika ushahidi alioutoa Agliotti katika kesi
hiyo mwezi Oktoba alisema, " Mtuhumiwa na mimi tulipokutana, nilifurahia
kununua vitu mbalimbali naye pia alifurahi. Kwa kuwa ni rafiki yangu,
nilikuwa nikiwaambia wauzaji wa maduka hayo kulipia nguo zote kupitia
akaunti yangu."
Alisema wakati wa sherehe ya siku ya kuzaliwa
mkewe Selebi alimnunulia mkoba wa ngozi iliyopakwa rangi ngumu
inayong'aa sana ya mbunifu maarufu Louis Vitton wenye thamani ya dola za
kimarekani 1300.
Mawakili wa utetezi wa Selebi wanadai kwamba
mteja wao, anayejulikana kwa kuvaa suti kali, anafanyiwa ubaya na
waendesha mashtaka.
Wanasema kesi hii ni sehemu ya njama
iliyozingirwa na masuala ya kisiasa na madai ya kuwa karibu sana wakati
wa uongozi wa aliyekuwa Rais, Thabo Mbeki.
Selebi alikuwa mshirika wa karibu na Bw Mbeki,
mpinzani mkuu wa Rais aliye madarakani, Jacob Zuma.
Lakini wakati wa kutoa uamuzi siku ya Ijumaa,
Jaji Meyer Joffe alitupilia mbali madai ya mawakili wa utetezi na kusema
waendesha mashtaka walitoa ushahidi wa kutosha kuwa Selebi alipokea
takriban randi 120,000 kutoka kwa Agliotti.
Selebi aliteuliwa na licha ya kutokuwa na uzoefu
wowote wa masuala ya polisi alipokuwa mtu wa kwanza mweusi kuwa mkuu wa
SAPS mwaka 2000.
Alijiuzulu kama rais wa Interpol mwaka 2008
baada ya waendesha mashtaka upande wa serikali kuthibitisha madai
yanayomkabili na kusimamishwa kazi na SAPS.
0 comments:
Post a Comment