Ghana inalenga kuweka historia ya kuwa timu ya
kwanza kutoka Afrika kufika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia
itakapochuana na Uruguay kwenye nusu fainali katika uwanja wa Soccer
City, mjini Johannesburg siku ya Ijumaa.
Cameroon ilifika hatua ya robo fainali mwaka
1990 na Senegal ikaiga mfano huo mwaka 2002.
Kocha wa Ghana Milovan Rajevac anasema shinikizo
kubwa zinazotokana na Ghana kuwa timu pekee kutoka Afrika iliyosalia
kwenye mashindano hazitawaathiri Black Stars kwenye mchuano wao dhidi ya
Uruguay.
Nchini Afrika Kusini inakofanyika michuano hiyo
ya Kombe la Dunia, chama tawala cha ANC kimewaomba wananchi wote kuvalia
mavazi ya rangi za Ghana na kuishabikia.
Pia kumekuwa na pendekezo la Ghana kubadili jina
la timu Black Stars na kuitwa The Black Stars of Afrika.
Rais wa chama cha soka cha Ghana Kwesi Nyantakyi
anasema anatumainia kwamba ushindi wa Ghana utasaidia kuleta umoja
katika bara la Afrika.
Ghana iliishinda Marekani mabao 2-1 ili kufuzu
kwa robo fainali, matokeo yaliyoleta hamasa kubwa sana kote barani
Afrika, hasa baada ya kuondolewa kwa timu zingine tano zilizokuwa
zinaliwakilisha bara hilo.
Ghana itakuwa bila kiungo Andre Ayew ambaye
alipata kadi mbili za njano kwenye michuano iliyopita na pia mlinzi
Jonathan Mensah aliyeonyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi dhidi ya
Marekani.
Sullay Muntari atatazamiwa kuchukua nafasi ya
Ayew ilhali safu ya ulinzi itaimarishwa na John Mensah na Samuel Inkoom.
Asamoah Gyan na Kevin-Prince Boateng wameshapona
majeraha ya iliyopita na wanatazamiwa kuisumbua ngome ya ulinzi ya
Uruguay.
Mlinzi Diego Godin ana jeraha, lakini bila yeye
Mauricio Victorino atatazamiwa kuwadhibiti Gyan na Boateng, kama
alivyoonyesha kwenye mchezo dhidi ya Mexico.
Diego Forlan na Luis Suarez wako imara katika
safu ya ushambuliaji ya Uruguay.
0 comments:
Post a Comment