Chavez: Iwapo Venezuela itashambuliwa, hatutaipatia mafuta Marekani
Rais Hugo Chavez wa Venezuela ametishia kwamba, iwapo mivutano itaongezeka kati ya serikali ya Venezuela na Colombia na kuchukuliwa hatua za kijeshi dhidi ya Caracas, serikali ya Venezuela itachukua uamuzi wa kukatisha kusafirisha mafuta yake nchini Marekani. Uhusiano wa Venezuela na Colombia uliingia dosari wiki iliyopita na kupelekea kukatika uhusiano wa kidiplomasia wa pande hizo mbili, baada ya Rais wa Colombia kudai kwamba Venezuela inawahifadhi mamia ya waasi wa Colombia, suala ambalo limekadhibishwa vikali na serikali ya Venezuela. Rais Chavez ameamua kufuta safari yake aliyoipanga kuelekea Cuba kutokana na kuongezeka mivutano kati ya nchi hizo mbili. Rais Chavez amesema kuwa, nchi yake iko tayari kuzima jaribio lolote la kijeshi litakalofanywa na Colombia, nchi ambayo inahesabiwa kuwa ni kibaraka wa Marekani katika eneo la Amerika ya Latini.
0 comments:
Post a Comment