Mabingwa mara tano wa Kombe la
Dunia, Brazil, wameondolewa kwenye michuano ya mwaka huu baada ya
kuzidiwa maarifa na kuchapwa mabao 2-1 na Uholanzi, katika mechi ya
robo fainali iliyopigwa uwanja wa Nelson Mandela Bay, mjini Port
Elizabeth.
Kipindi cha kwanza kilimalizika Brazil wakiongoza
bao 1-0, lililofungwa katika dakika ya 10 na Robinho, lakini kwenye
dakika ya 53 mlinzi Felipe Melo alijifunga na kuwapa Uholanzi bao la
kusawazisha, na baadaye akazidi kuandamwa na mkosi akaonyeshwa kadi
nyekundu.
Bao la ushindi la Uholanzi lilifungwa kwa kichwa na
Wesley Sneijder katika dakika ya 68 kumalizia mpira wa kona.
Kona hiyo ilitokana na mlinzi Juan kuutoa nje mpira
pasipo ulazima akiwa hajaandamwa na wachezaji wa Uholanzi, na ni
miongoni mwa makosa ambayo Brazil itaendelea kujutia.
Felipe Melo alionyeshwa kadi nyekundu baada ya
kumkanyaga Arjen Roben akiwa chini.
Kwa ushindi huo, Uholanzi wamelipiza kuondolewa
mara mbili na Brazil kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1994 na
1998.
Nusu fainali
Uholanzi wanasubiri kuchuana kwenye nusu fainali na
mshindi kati ya Ghana na Uruguay siku ya Jumanne.
Hata hivyo watakuwa bila mlinzi Gregory van der
Wiel na kiungo Nigel de Jong ambao wote wawili wana kadi mbili za njano.
Katika dakika ya nane Robinho alifunga bao, lakini
bendera ya msaidizi wa mwamuzi ikawa imenyanyuka kuashiria aliotea.
Hazikupita zaidi ya dakika mbili tena kabla ya
Robinho kuipenya tena ngome ya Waholanzi na kuipatia Brazil bao la
kuongoza.
Baada ya Uholanzi kufunga bao la pili na Melo
kuonyeshwa kadi nyekundu Brazil walififia kimchezo, kiasi kwamba
Uholanzi walitishia kufunga mara kwa mara huku wakiwadhibiti
washambuliaji wa Brazil.
0 comments:
Post a Comment