Polisi nchini Rwanda wanamzuilia
kiongozi wa chama cha upinzani cha PS Imberakuri, Bernard Ntaganda kwa
madai ya uchochezi na kubuni chama cha waasi.
Hii ni baada ya Rais Paul Kagame kuzungumzia
jaribio la kufanyika maandamano hapo jana, wakati tume ya uchaguzi
nchini humo ilipoanza kupokea majina ya watu wanaotaka kugombea kiti cha
urais utakaofanyika mwezi wa nane.
Rais Kagame anasema wahusika lazima wafuate
sheria lakini upande wa upinzani unadai kuwa vyombo vya dola vinawabana.
Msemaji wa polisi Eric Kayiranga,
amethibitisha kukamatwa kwa Bernard Ntaganda, lakini amesema bado haja
funguliwa mashtaka.
Kiongozi mwingine wa Upinzani Victoire Ingabire
amesema wajumbe wa chama chake cha United Democratic Forces
walikamatwa wakati wa maandamano mjini Kigali.
*******************************
Waziri wa ulinzi wa Burundi amesema anatumai
kiongozi wa chama kikuu cha upinzani na aliyekuwa kiongozi wa waasi
Agathon Rwasa hajajificha.
Kauli hiyo ameitoa kufuatia ripoti kuwa Bw
Rwasa, aliyetia saini makubaliano ya amani mwaka jana kusalimisha
silaha, hajaonekana tangu Jumatano asubuhi.
Mapema mwezi huu alijitoa kwenye uchaguzi
unaotarajiwa kufanyika Jumatatu.
Uchaguzi huo utakuwa wa pili tangu kumalizika
kwa mauaji ya kikatili ya wenyewe kwa wenyewe yaliyokuwa kwenye misingi
ya kikabila yaliyodumu miaka 12.
Rais Pierre Nkurunziza na Bw Rwasa waliongoza
zaidi kundi la waasi la Kihutu waliokuwa wakipigana dhidi ya jeshi la
serikali lililodhibitiwa na Watutsi walio wachache.
Bw Rwasa alikataa kuacha mapigano wakati makundi
mengine yalipoamua kuunda serikali ya muungano yaliyofuatiwa na
uchaguzi mwaka 2005.
Aliiongoza National Liberation Force (FNL)
kusalimisha silaha Aprili 2009 na amekuwa akidhaniwa kuwa mpinzani mkuu
wa Rais Nkurunziza katika uchaguzi wa wiki ijayo. bbc swahili
0 comments:
Post a Comment