Mwandishi mmoja wa habari wa
gazeti binafsi amepigwa risasi na kuuwawa nje ya nyumba yake huko Kigali
mji mkuu wa Rwanda.
Walioshuhudia wamesema mwandishi huyo, Jean
Leonard Rugambage, ambaye alikuwa kaimu mhariri wa gazeti la Umuvugizi
alipigwa risasi na watu wawili ambao baadaye walitoweka kwa gari.
Hivi karibuni serikali ya Rwanda iliagiza
kusimamishwa kwa uchapishaji wa gazeti hilo, na likaanza kuandika habari
kwenye mtandao.
Uchunguzi
Polisi wamesema hawajui nani aliyefanya mauaji
hayo, lakini mhariri mkuu wa gazeti hilo ambaye yuko uhamishoni, Jean
Bosco Gasasira, ameilaumu serikali.
Gasasira ambaye alitorokea Uganda mwezi Aprili
baada ya gazeti lake kusimamishwa, na anadai serikali ya Rwanda ilipanga
mauaji ya mwandishi Rugambage.
Amedai kwamba ana uhakika mwandishi huyo
alipigwa risasi na kuuawa na maafisa kutoka idara ya usalama wa taifa.
Gasasira amesema mauaji hayo yametokana na
taarifa zilizochapishwa kwenye tovuti ya gazeti la Umuvugizi kuhusiana
na jaribio la mauaji ya ya mkuu wa zamani wa jeshi la Rwanda, Luteni
Jenerali Faustin Kayumba Nyamwasa nchini Afrika Kusini, mwishoni mwa
wiki iliyopita.
Serikali ya Rwanda imeshakanusha kuhusika na
kupigwa risasi kwa Luteni Jenerali Nyamwasa. Mkuu huyo wa zamani wa
jeshi alikimbilia nchini Afrika Kusini mapema mwaka huu baada ya
kutofautiana na Rais Paul Kagame, akimlaumu Rais huyo kwa ufisadi.
Lawama
Bw Kagame amekanusha madai hayo, na serikali
yake imemlaumu Lt Gen Nyamwasa kwa kuhusika na mashambulizi ya grineti
yaliyotokea nchini Rwanda mapema mwaka huu.
Mwezi Aprili, Rais Kagame alifanya mabadiliko ya
uongozi jeshini, na maafisa wawili wa ngazi za juu wakasimamishwa, na
kuwekwa katika kifungo cha nyumbani.
Mapema mwezi huu baraza linalodhibiti vyombo vya
habari nchini Rwanda lilisimamisha kwa muda wa miezi sita gazeti la
Umuvugizi kwa madai ya kuchochea upinzani dhidi ya serikali.
Wavuti wa gazeti hilo uliozinduliwa mwezi Mei
kwa wakati huu hauwezi kupatikana kupitia watoaji wa huduma za internet
nchini Rwanda, na serikali imekanusha kwamba imehusika katika kubana
wavuti huo.
Bw Rugambage ambaye amemwacha mke na mtoto mmoja
aliondolewa mashtaka ya kuhusika na mauaji ya kimbari na mahakama ya
kijadi ijulikanayo kama Gacaca mwaka 2006.
Mshtuko
Mwandishi wa BBC mjini Kigali, Geoffrey
Mutagoma, amesema mauaji hayo yamewashtua waandishi wengi nchini Rwanda.
Uchaguzi wa Rais nchini Rwanda unatazamiwa
kufanyika mwezi Agosti, huo ukiwa uchaguzi wa pili kufanyika tangu
mauaji ya kikabila ya mwaka 1994.
Makundi ya kutetea haki za binadamu yamekuwa
yakiilaumu serikali ya Rwanda kwa kujaribu kunyamazisha vyombo vya
habari vya kibinafsi, lakini serikali inakanusha.
Serikali ya Rais Kagame imekuwa ikitoa
malalamiko kwamba lazima idhibiti vyombo vya habari pamoja na wanasiasa
ili kuepusha kutokea tena kwa mauaji ya kimbari kama ya mwaka 94, ambapo
watu 800,000 waliuawa.
Mapema wiki hii Katibu Mkuu wa umoja wa mataifa
Ban Ki-Moon alimteuwa Rais Kagame kuwa mmoja wa wenyekiti wa kamati
maalum ya watu mashuhuri katika kupambana na umasikini, ambayo ina
jukumu la kuchochea kufanikisha malengo ya Milenia ya Umoja wa Mataifa.
Rais Kagame pia amekuwa akisifiwa kwa kujaribu
kuimarisha uchumi wa Rwanda kwa kutumia mbinu za kisasa tangu
alipochukua uongozi mwishoni mwa mauaji hayo. bbc swahili
0 comments:
Post a Comment