Mabaharia waliotekwa na
maharamia wa kisomali kwenye meli ya biashara inayomilikiwa na raia wa
Libya wamefanikiwa kuidhibiti tena meli hiyo katika ghuba ya Aden.
Jeshi la majini la Ulaya linalopambana na
uharamia katika pwani ya Somalia limesema baadhi ya maharamia
wanaaminiwa kuuawa wakati wa tukio hilo.
Jeshi hilo la Umoja wa Ulaya, Navfor, limesema
mmoja wa mabaharia katika meli ya biashara ya MV Rim amejeruhiwa.
Wakati huo huo, meli nyingine imetekwa katika
ghuba ya Aden.
Maharamia wameteka meli hiyo yenye tani 15,000,
MV QSM Dubai, katika ghuba ya Aden mapema Jumatano.
Meli hiyo ina mabaharia 24 yenye raia wa Ghana,
Misri, Pakistan na Bangladesh.
Meli ya kivita ya Marekani imeripoti kuona
angalau haramia mmoja kwenye meli hiyo iliyotekwa akiwa na guruneti.
'Taarifa za kukanganya'
Taarifa kutoka Navfor imesema, meli ya kivita ya
EU, SPS Victoria, ilipelekwa kwenye ghuba ya Aden kutoa msaada wa
kitabibu kwa mabaharia wa MV Rim.
Imesema kulikuwa na "taarifa za kukanganya"
kwamba meli hiyo ilikuwa imevamiwa tena na maharamia.
Lakini helikopta kutoka meli hiyo ya kivita
ilipofika kwenye eneo la tukio, iliweza kufahamika haraka kuwa mabaharia
hao waliweza kudhibiti meli hiyo.
MV Rim, yenye mabaharia wake 10 kutoka Syria
ilitekwa mwezi Februari na maharamia waliodai kikombozi cha dola za
kimarekani milioni tatu ili kuwaachia wakiwa salama.
Baada ya kutekwa, waandishi wanasema maharamia
waliivusha meli hiyo kwenye mji wa Laasgoray, mpakani mwa miji ya
Somalia inayojitawala yenyewe ya Somaliland na Puntland.
Takwimu zilizotolewa na shirika la kimataifa
linalosimamia safari za majini (IMB) zinaonyesha kuwa mashambulio ya
maharamia duniani yameporomoka kwa asilimia 34 katika miezi mitatu ya
mwaka 2010 ukilinganisha na mwaka mmoja uliopita, kutokana na kuwepo kwa
meli za kigeni kwenye ghuba ya Aden.
Takriban meli 20,000 hupita kwenye ghuba ya Aden
kila mwaka, zikielekea na kurudi kutoka mfereji wa Suez.
0 comments:
Post a Comment