SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Wednesday, June 16, 2010

Leo ni zamu ya mabingwa wa Ulaya Spain na Uswisi: Bafana Bafana na Uruguay.

 BAFANA BAFANA
   Kombe la dunia 2010 linaendelea leo kwa wenyeji Bafana Bafana -Afrika kusini, siku ya ukumbusho wa machafuko ya Soweto,1976, ikijaribu kuilaza Uruguay, mabingwa mara 2 wa dunia, na kuondoka na pointi 3 ili kuhakikisha yaingia duru ijayo.
   Ni siku pia ya kuwaona Waspain,mabingwa wa ulaya, wakicheza na Uswisi. Spain, imekuwa ikipigiwa upatu mno kwamba, ndio timu ya usoni kabisa kutwaa Kombe la dunia mwaka huu na hasa baada ya jana Brazil, kutolewa jasho na Korea ya Kaskazini. Kabla ya mapambano hayo 2, kwanza timu mbili za Amerika kusini: Chile na Hondurus, zitafungua dimba la hii leo huko Nelsprut.
   Afrika Kusini, ilioanza kwa sare ya bao 1:1 na Mexico, siku ya ufunguzi wa Kombe hili ijumaa iliopita, inarudi uwanjani ikijua lazima ishinde leo kuweka hayi matumaini i ya kucheza duru ijayo.Katika kundi hili timu zote 4 ziko pointi sawa-Ufaransa,Uruguay,Mexico na Afrika kusini yenyewe. Isitoshe, mpambano wa leo unachezwa katika ile wanayoiita "Siku ya Vijana" - siku ya mapumziko kwa ukumbusho wa machafuko ya Soweto,1976.
   Spain,mabingwa wa Ulaya, wanatazamiwa nao kutamba mbele ya Uswisi na kupeleka salamu zao kwa timu nyengine kubwa kama Ujerumani,Brazil na Argentina kuwa huu ni mwaka wao. 

Kombe la dunia:Matumaini ya Afrika yaelekezwa kwa Ghana na Ivory Coast 
Timu zote 6 za Afrika tumeshaziona uwanjani katika kombe hili la kwanza kabisa la dunia barani Afrika 2010.
   Tumewaona wenyeji  Bafana Bafana walipomudu suluhu tu na Mexico ya bao 1:1, Algeria,ikatolewa kwa  bao 1:0 na chipukizi Slovenia; simba wa nyika-Kameroun, walishindwa kunguruma katika mbuga za Kruger Park Afrika Kusini na  ilichapwa  bao 1:0 na mabingwa wa Asia Japan.Ni Black Stars, Ghana,bila ya stadi Michael Essien,  waliokuwa wa kwanza kupepea bendera ya Afrika  walipoitoa Serbia  kwa bao 1:0.
   Sasa timu gani ya Afrika, imetoa matumaini ya kufika duru ya pili ? na vipi matarajio ya kufika na kupindukia pale  kameroun ikicheza na mzee Roger Milla ilipotamba  1990 huko Italia na Senegal ,ikicheza na nahodha Al haj Diouf, zilipowasili hadi robo-finali.
   Hata Nigeria,haikufua dafu  wala kuweka matumaini.Hili lakini sio ilisemekana ni Kombe la Afrika na kombe litabaki Afrika hapo Julai 11 ?
   Afrika kusini, Bafana Bafana,walishangiria  kutia bao la kwanza kabisa katika kombe hili la dunia walipocheza na Mexico.lilikuwa bao maridadi lililoashiria makubwa.Lakini, mashabiki wa Bafana bafana wakihanikiza kwa vuvuzela,mazumari yao,yalizimwa pale mnamo dakika ya 80  ya mchezo,Mexico ilipowatilia kitumbua chao mchanga na kusawazisha. Nafasi nyingi walizopata washambulizi wa afrika Kusini kuondoka na ushindi hawakuzitumia.
   Simba wa nyika, wakirudi katika  kombe lao la 6 la dunia,tangu kucheza mara ya kwanza Spain,1982,wamebainisha nao hata bila ya nahodha Samuel Eto-o aliyechukua usukani kutoka  kwa nahodha wa zamani Rigobert Song,sio simba wa zamani.
   Wameshinmdwa kunguruma na wamedhihirisha kwanini hawakufika mbali katika Kombe la Afrika,huko Angola.
   Eto-o kama alivyolalamika mzee Roger Milla, bado hakuifanyia Kameroun lolote lenye maana kinyume na Barcelona na Inter Milan,timu alizotawazwa nazo mabingwa wa Spian,Itali na Ulaya.
Nigeria, ilikwisha pia bainisha katika Kombe la Afrika huko Angola, kwamba haina stadi kati ya uwanja  mfano wa J.J Okocha au  usoni kama Rashidi Yakin,wachezaji wenye fikra na ufundi wa kuchangamsha mchezo na kutia mabao.
   Algeria, pengine, wanajuta kwanini waliwatoa mafirouni -Misri,mabingwa wa afrika, nje ya Kombe hili la dunia.Kwani, nani ajuwae,pengine Misri, ikipepea bora zaidi bendera ya Afrika.
   Kushindwa mpambano mmoja hakuna maana ndio timu za Afrika zimeshatolewa duru ya kwanza:la,hasha.lakini sio dalili njema huonekana asubuhi ?
   Dalili tulizoziona hadi sasa,hazitupi matumaini,kwamba Simba na Tembo  wa Afrika watatamba barani mwao.
   Kama katika Kombe lililopita la dunia,Black Stars-Ghana, ndio nyota  pekee ilionawiri hadi sasa katika mawingu ya Afrika,kwani ndio ilioondoka hadi sasa na ushindi na pointi 3.
   Ivory Coast,ingawa bila ya ushindi dhidi ya Ureno, haikuvunja moyo licha ya kuangukia tena kama 2006,katika kundi la kufa-kupona.
   Kwa kutoka sare na Ureno 0:0, zote mbili zitategemea  sasa ushindi wazi dhidi ya Korea ya kaskazini ili kuifuata Brazil kutoka kundi hili duru ya pili.
   Ivory Coast,bila ya kuwa nahodha wao Drogba si fit sawa sawa, yatoa matumaini kwa Afrika. Ghana imeshapiga hatua moja kwenda duru ijayo kama ilivyofanya Kombe lililopita la dunia.
   Ivory Coast na Ghana, simba wa nyika Kameroun, wakitusamehe, ndizo hadi sasa zilizotimiza matarajio kuwa   ndio tumaini la Afrika 2010.
Mwandishi: Ramadhan Ali/AFPE

0 comments:

Post a Comment