Meli ya mafuta ya Ufaransa
imenusurika kutekwa na maharamia wanaoshukiwa kuwa wa Kisomali katika
ufuo wa Tanzania hapo jana.
Taarifa iliyotolewa na muungano wa Ulaya na
ubalozi wa Uingereza kwa waandishi wa habari nchini humo imethibitisha
tukio hilo na kudokeza kuwa meli ya maharamia hao imekimbilia kisiwani
Pemba baada ya kuzidiwa nguvu na wanamaji wa muungano wa Ulaya.Kwa mjibu wa mwandishi wa BBC mjini Dar es Salaam, John Ngahyoma hili ni jaribio la tatu ambalo limetekelezwa na maharamia katika eneo hilo.
Kutokana na tishio hilo, mabalozi kutoka muungano huo ikiwemo Uingereza na Uholanzi wanakutana baadaye hii leo mjini Dar es Salaam kujadili suala hilo.
Tukio hili linajari wakati raia watano wa Somalia wanaotuhumiwa kwa uharamia wakikanusha mashtaka katika mahakama mmoja nchini Uholanzi.
Hii ndiyo kesi ya kwanza ya uharamia kuwahi kusikizwa katika mahakama hiyo. Washukiwa hao wanatuhumiwa kujaribu kuteka meli inayomilikiwa na Uholanzi mnamo Januari mwaka wa 2009, katika ghuba ya Eden.
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita maharamia hao wameteka meli 200, hatua ambayo imetishia usalama na kuzorotesha uchumi unaochangiwa na usafiri wa bahari ya hindi.
BBC Swahili.
0 comments:
Post a Comment