MLINZI wa sekondari ya Aboud Jumbe, Kigamboni,Shemsa Mpelela (22),
aliyetoroka baada ya kutuhumiwa kuchoma moto nyumba na kuua watu watano
wa familia moja, ameonekana usiku wa kuamkia jana eneo la shule hiyo
akiwa na silaha.
Walioteketea kwa moto wakiwa katika nyumba yao yenye chumba kimoja
ni baba mwenye nyumba John Onesmo (32) ambaye ni mfanyabiashara wa
samaki eneo la Feri, Catherine John (25), anayefanya biashara
ndogondogo, watoto wao Oliver (2) na Joyce John (5) na Esther Amos (20)
ambaye ni mdogo wa Catherine.
Esther anadaiwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Shemsa na
kutokana na ugomvi baina yao, alidaiwa kuchoma nyumba hiyo usiku wa
kuamkia juzi.
Kaimu Mwalimu Mkuu wa Aboud Jumbe, Pasisi Mwinchumu, aliliambia
gazeti hili jana, kuwa alipewa taarifa kwamba Mpelela, anayeishi
Kisiwani Kigamboni, ambaye kwa mujibu wa ratiba yake alitakiwa kufika
kazini juzi saa 12.30 jioni, alifika saa 8:48 usiku akiwa na chuma
kizito na kuonekana akirandaranda shuleni hapo.
Taarifa zilisema mtuhumiwa akiwa na chuma hicho, alikwenda sehemu
iliyozoeleka kukaa mlinzi mwenzake na kunyatia na baada ya kukosa mtu
yeyote pale, aliendelea kuvinjari eneo la shule hiyo.
Wakati anavinjari watu walimwona na kutoa taarifa Polisi ambao hata
hivyo walifika eneo hilo saa 10 alfajiri jana wakiwa na gari aina ya
Land Rover Defender na kukuta mtuhumiwa ameshaondoka.
Ilielezwa kuwa baada ya polisi kufika, walifanya msako kwenye maeneo
kadhaa ya shule hiyo ikiwamo madarasani, lakini hawakuambulia kitu.
Mwinchumu alisema kuonekana kwa mlinzi huyo usiku huo, kumezusha
hofu shuleni hapo akisema, “hata mimi sasa hivi sikai ofisini kwangu
nakaa chumba cha walimu wote”.
Alisema jana jioni walitarajia walimu wakiongozwa na mwalimu mkuu
kufanya kikao cha kujadili hali hiyo sambamba na kuchukua hatua za
kiusalama.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, David Misime, alipotafutwa
kuzungumzia maendeleo ya msako dhidi ya mtuhumiwa huyo, alisema polisi
wanaendelea kumsaka ambapo juzi na jana walifanya msako ikiwamo kwenda
shuleni hapo mara kwa mara.
Hata hivyo, alisema hana taarifa kama mtuhumiwa huyo alifika shuleni
usiku wa kuamkia jana na alipoulizwa kama wamepanga taratibu zozote za
ulinzi katika eneo la shule hasa baada ya kuonekana kuwapo hofu miongoni
mwa watu, alisema “hao wenye hofu wangekuja kutwambia ili tuangalie cha
kufanya”.
Wakimzungumzia zaidi Mpelela, baadhi ya walimu walisema hivi
karibuni aliwaeleza kuwa na nia ya kufunga ndoa na mchumba wake ambaye
ni Esther.
“Alisema anataka kumwoa mchumba wake huyo, kwani sisi tunamjua
alishawahi kuja hapa shuleni wakati fulani Mpelela alipoumwa. Yeye
(Mpelela) alituomba tumchangie mahari, lakini tulikuwa hatujamchangia
kwani tulisubiri atuombe rasmi,” alisema mmoja wa walimu wa shule hiyo.
Inadaiwa Mpelela alikuwa mpole kwa mwonekano lakini mkali na
anafahamu kupigana karate, hali iliyowafanya wanafunzi kumwogopa.
“Wanapokuwapo walinzi wengine, baadhi ya wanafunzi hutoroka na wapo
wanaodiriki hata kuwapiga, lakini Mpelela wanamwogopa na anapokuwapo
hawathubutu kutoroka wala kumchezea, kwani ni mkali sana kwao,” alisema
mmoja wa walimu hao.
Mpelela anadaiwa kuchoma nyumba ya John na familia yake usiku wa
kuamkia juzi na kuua watu wote watano waliokuwa ndani. Anadaiwa kutumia
mafuta ya petroli.
Siku mbili kabla ya nyumba hiyo kuchomwa, Mpelela inadaiwa
aligombana na Esther na kumchoma kisu shingoni na tumboni na
kumsababisha akimbilie kwa dada yake, Catherine, na kupelekwa hospitali
kwa matibabu na kupewa barua ya Polisi ya kusakwa Mpelela ambaye
alitoroka nyumbani kwake tangu siku hiyo na hajulikani aliko.
Hata hivyo, licha ya kutoroka nyumbani kwake Kisiwani, Mpelela
alikuwa akienda kazini hadi siku za Jumapili na tangu watu hao wapotezea
maisha, hajaonekana kazini.
Watu hao watano wanatarajiwa kuzikwa leo Kisiwani baada ya kuagwa
katika hospitali ya Vijibweni.
Imeandikwa na Maulid Ahmed
Habari Leo.
Wednesday, May 26, 2010
Anayedaiwa kuua watu watano awinda wengine
Posted by
Ally Shaaban Mgido's
at
Wednesday, May 26, 2010
Email This
BlogThis!
Share to X
Share to Facebook
0 comments:
Post a Comment