SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Sunday, May 2, 2010

AJALI YA MTUMBWI MTWARA: Mtoto wa miezi 8 anusurika kifo

IKRAM Athuman mwenye umri wa miezi minane, anaweza kuelezewa kuwa ni mtoto mwenye bahati, kwani imefahamika kuwa ni miongoni mwa majeruhi saba walionusurika kifo katika ajali ya mtumbwi uliopinduka na kuzama juzi mjini Mtwara.

Mtumbwi huo unaofanya safari kati ya eneo la Shangani na Msangamkuu mjini Mtwara linalotenganishwa na bahari ya Hindi kwa kilometa zisizozidi tatu, unahofiwa kuwa umesababisha vifo vya watu 21 kati ya 28 waliokuwa wanasafiri nao.

Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Stephen Buyuya alisema jana mjini hapa kuwa, mtoto huyo na mama yake, Fatuma Hamisi waliozama majini na baadaye kuokolewa, ni miongoni mwa watu saba walionusurika na sasa wanaendelea na matibabu katika hospitali ya Ligula.

“Kati ya majeruhi saba, mmoja ni mtoto wa kiume mwenye umri wa miezi minane…..kiujumla wote afya zao zinaendelea vizuri na wanaweza kuruhusiwa kadri hali zao zinavyozidi kuimarika …hakuna mwili wowote uliopatikana hadi sasa licha ya wazamiaji kuendelea na kazi ya kuitafuata,” alisema Buyuya.

Aliwataja majeruhi wengine kuwa ni Idd Hamad, Rukia Mohammed, Fatuma Ismail, Zainabu Ismail na Rukia Salum, wote wakazi wa Msangamkuu.

Aidha Kamanda Buyuya alisema nahodha aliyemtaja kwa jina la Cletus na msaidizi wake anayefahamika kama `Chaijaba’ inadaiwa waliruka baada ya mtumbwi kuanza kupoteza mwelekeo. Mpaka sasa hawajulikani walipo.

“Inasemekana kuwa hawa wapo hai, sisi kama jeshi la Polisi tunazifanyia kazi ….inadaiwa pia mtumbwi huo ulikuwa umetoboka na ulizibwa kwa viroba ambavyo vinadaiwa vilizibuka na kuanza kuingiza maji,” alisema Buyuya.

Kamanda huyo alibainisha kuwa kwa mujibu wa wataalamu miili ya watu hao itaanza kuelea baharini leo, hivyo ametoa wito kwa wakazi wa mikoa ya Lindi, Pwani na Dar es Salaam kutoa taarifa polisi pindi watakapoiona miili hiyo.

0 comments:

Post a Comment