SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Monday, July 11, 2016

TANAPA YAFANIKISHA UJENZI WA ZAHANATI KATIKA KIJIJI CHA IKUZA WILAYANI MULEBA.

Diwani wa kata ya Ikuza iliyopo katika Kisiwa cha Ikuza , wilayani Muleba mkoa wa Kagera,Fortunatus Matta (Kulia) akimueleza jambo Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Pascal Shelutete alipoongozana na wanahabari kutembelea kijiji hicho cha Ikuza.Wengine ni wakazi wa kijiji hicho.
Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) akizungumza na wakazi wa kijiji cha Ikuza mara baada ya kutembelea jengo la Zahanati lililojegwa na TANAPA kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Muleba kwa ajili ya wakazi wa kata hiyo.
  Sehemu mbalimbali za Jengo la Zahanati ya kijiji cha Ikuza wilayani Muleba lililojengwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa ushirikiano na Halmashauri ya wilaya ya Muleba mkoani Kagera.
Mzee William Lugaga akizungumza namna wananchi wa Kisiwa cha Ikuza wanavyopata shida katika kupata huduma ya afya hali ambayo imewalazimu kusafiri wa kutumia mitumbwi kwenda kutafuta huduma hiyo vijiji vya jirani . 
Pelagia Samson,mkazi wa kijiji cha Ikuza wilayani Muleba akizungumza namna akina mama wanavyopata shida hasa wakati wa kujifungua kutokana na kutokuwepo kwa Zahanati katika kijiji hicho ambapo baadhi yao wamelazimika kujifungulia kwenye mitumbwi wakati wakipelekwa kupata huduma katika kituo cha afya kilichopo kijiji cha jirani.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ikuza wilayani Muleba wakisikiliza kwa makini maelezo yaliyokuwa yakitolewa kwa wanahabari (hawapo pichani) walipotembelea kijiji hicho.
Baadhi ya Wanahabari waliotembelea kijiji cha Ikuza ,wilayani Muleba mkoani Kagera ,wakiwa katika picha ya pamoja na Diwani wa kata hiyo Fortunatus Matta pamoja na Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Pascal Shelutete.

Na Dixon Busagaga wa Michuzi Blog,aliyekua Muleba, Kagera.

JUMLA ya Sh. Milioni 226 zimetumika kwa ajili ya kujenga zahanati katika kijiji cha Ikuza wilayani Muleba mkoani Kagera.

Kwa mujibu wa Diwani wa kata ya Ikuza, Fortunatus Matta ni kwamba Zahanati hiyo ilijengwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Muleba na Wananchi.

Alisema ili kukamilisha ujenzi huo, TANAPA ilitoa Sh. Milioni 101, halmashauri ikatoa Sh. Milioni 80 huku wananchi wakichangia Sh. Milioni 22.

“Tunaishukuru sana TANAPA  kwa kupitia Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, ambayo inapakana na kijiji chetu kwa kuonyesha nia kusaidia mradi huu wa ujenzi kwa ajili ya kuokoa maisha ya wananchi wetu,” alisema.

Alisema ujenzi wa jengo hilo kutaleta matumaini kwa wananchi ambao walikuwa wanatumia kilomita 83 kwa ajili ya kufuata huduma za afya kwenye kituo cha Afya cha Kanisa la AICT kilichopo Kasenyi.

Aidha, alisema licha ya jengo hilo kukamilika lakini bado kumekuwa na tatizo la kupata watumishi, vifaa tiba na dawa.

Wakizungumza na waandishi wa habari, wananchi wa kijiji cha Ikuza, wameishukuru TANAPA kwa kuwajengea Zahanati hiyo.

Mkazi wa kijiji hicho, William Lugaga alisema: “Nashukuru Mungu, hakuna mwanamke yeyote ambaye aliwahi kuzama kwenye ziwa kwa ajili ya kufuata huduma za afya.”

Kwa upande wake, Peragia Samson alisema wakinamama wanapata shida sana wanatumia muda wa saa tatu kwa ajili ya kufuata huduma ya Afya.

“Wakinamama wanajifungulia njia kabla hata ya kufika hospitali na wengine kwenye boti,” alisema.

Naye, Kisanti Joseph alisema naona uchungu kuona wanawake wajawazito wanapotaka kujifungua lazima wapande boti kwenda Kasenyi. 

“Kuna wanawake wengine wanajifungulia kwenye boti…hii yote ni kukosa huduma ya Afya,”alisema.

0 comments:

Post a Comment