SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Sunday, May 2, 2010

Dhahabu yamwaga damu

Kwa zaidi ya saa mbili, kijiji cha Mgusu wilayani Geita, Mwanza, kinachokaliwa na wachimbaji wadogo na kuendesha shughuli zao za uchimbaji wa dhahabu, jana kiligeuka 'uwanja wa vita’ baada ya kuibuka mapambano baina ya wachimbaji na polisi.

Polisi hao wapo katika eneo hili wakilinda machimbo hayo yaliyofungwa mapema mwaka jana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, baada ya kuporomoka na kuua wachimbaji wadogo zaidi ya kumi, huku wengine zaidi ya 20 wakiripotiwa kunusurika.

Lakini chanzo cha vurugu za jana, kinadaiwa ni kuchoshwa kwa wachimbaji hao kusubiri kufunguliwa kwa machimbo, kama ilivyokuwa imeahidiwa na Waziri Mkuu kwamba yangefungwa kwa siku 90 tu.

Hata hivyo, baada ya kuona mwaka mmoja unavuka huku serikali ikiwa kimya, wachimbaji hao alfajiri ya jana walijiamulia kuvamia machimbo hayo wakiwa katika kundi la zaidi ya watu 200, wakiwamo wanaume, wanawake na watoto.

Inadaiwa kwamba, kitu cha kwanza walichokifanya ni kuwashambulia polisi watano waliokuwa katika lindo, wakiwarushia mawe kuwataka waliache eneo hilo ili warudi katika uchimbaji wa madini.

Polisi nao waliamua kujibu mapigo kwa kutumia risasi za moto na mabomu ya machozi kwa lengo la kuwatawanya wachimbaji hao waliokuwa wanarusha mawe yaliyoonekana kuwazidi nguvu polisi hao.

Inaelezwa kutokana na hali hiyo, polisi walilazimika kuomba nguvu ya ziada kutoka Kituo Kikuu cha Polisi mjini Geita na baada ya muda, kundi la askari zaidi ya 15 waliingia eneo la tukio lililokuwa limeshamiri mapambano.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia wachimbaji wakitumia mbinu ya kuwatanguliza mbele watoto wadogo wenye umri wa kati ya miaka 6 na 10, kwa lengo la kusaka `huruma’ ya polisi.

Hata hivyo, polisi `hawakudanganyika’, kwani waliendelea kuwadhibiti wavamizi hao ambao baadaye walianza kutawanyika, kila mmoja akielekea upande wake kwa lengo la kujisalimisha.

Baadhi inadaiwa wamejeruhiwa, na mmoja ametolewa utumbo baada ya kudaiwa kupigwa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni risasi.

Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Geita aliyekuwa katika eneo la tukio kuongoza operesheni hiyo, ACP Hassan Kimea alisema vijana wake walilazimika kutumia nguvu kwa kuwa kitendo cha wachimbaji hao kuamua kuwashambulia kwa mawe askari wanaolinda eneo hilo, hakitavumiliwa.

“Hatuwezi kuwakamata hawa watu wote zaidi ya 200…..lakini tuna taarifa za uhakika tena kwa majina kuhusu watu walioratibu mipango yote hii hadi kuifikisha katika hali hii, ni lazima tuwakamate na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria…,” alisema ACP Kimea.

Kwa upande wake Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Paul Kihimbila alisema kuwa, katika tukio hilo askari wake kadhaa wamejeruhiwa kutokana na kupigwa kwa mawe na wachimbaji hao, na kuongeza kwamba kwa sasa ulinzi umeimarishwa zaidi katika eneo la tukio.

“Kwa kweli vurugu zilikuwa kubwa sana…ingawa hadi sasa hatuna taarifa za mwananchi yeyote kupigwa risasi, lakini tuna taarifa kwamba kuna baadhi wamejeruhiwa vibaya katika purukushani wakati wakikimbia na wengine nasikia wamevunjika miguu, na wengine kuumizwa… Isipokuwa kuna askari wangu mmoja ambaye nimemuona amejeruhiwa baada ya kupigwa na jiwe kichwani, ingawa nasikia kuna wengine zaidi nao wamepigwa mawe, lakini sijawaona…

“Kwa sasa ndiyo tunaendelea kukusanya taarifa kutoka kila upande, lakini kuna watu naambiwa wamejeruhiwa na kukimbizwa hospitali ya wilaya, kwa hiyo sina taarifa rasmi na nzuri kwa sasa…” alisema Kihimbila.

Hata hivyo, kwa upande wao baadhi ya wachimbaji waliopata nafasi ya kuzungumza na gazeti hili, walisema ugumu wa maisha umewafanya kushindwa kuvumilia, ndiyo maana wakalazimika kutumia mabavu kuingia eneo la machimbo.

Waziri Mkuu Pinda wakati wa maziko ya walioangukiwa na kufukiwa na kifusi katika eneo hilo Machi 14 mwaka jana baada ya kazi ya kuwaopoa kushindikana, alitoa siku 90 na kuwataka wachimbaji hao kusitisha shughuli za uchimbaji katika eneo hilo na kwamba baada ya muda huo serikali ingelitoa tamko lingine.

Pia Waziri mkuu aliagiza kujengwa kwa mnara na kuzungushiwa uzio katika eneo hilo na hasa shimo ambalo wachimbaji hao walifukiwa na hivyo serikali kuamua wazikwe ndani yake. Lakini kufikia jana, agizo hilo lilikuwa halijatekelezwa.

Mkuu wa wilaya ya Geita, Philemon Shelutete hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo na kauli ya serikali kwa ujumla juu ya eneo hilo, na hasa ikizingatiwa kwamba siku 90 zilizotolewa na Waziri Mkuu kwa ajili ya wachimbaji hao kusitisha shughuli za uchimbaji katika eneo hilo zimemalizika na sasa ni mwaka mmoja na siku 14.

Hadi tunakwenda mitamboni kulikuwa na taarifa kwamba serikali ingelitoa tamko juu ya kuwepo kwa eneo hilo juu ya kuendelea kuchimbwa ama la, kazi ambayo ilitarajiwa kufanywa na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja Jijini mwanza.

0 comments:

Post a Comment