Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisalimiana na mwendesha pikipiki maarufu na hodari, Zaina Amour wa
kijiji cha Nandagara wilayani Ruangwa Aprili 10, 2016. Alikuwa katika
ziara ya jimbo lake la uchaguzi la Ruangwa. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
……………………………………………………………………………………….
WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema serikali
inatarajia kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Nanganga,
Ruangwa hadi Nachingwea.
Hatua hiyo itawezesha kutatuliwa
kwa kero ya changamoto ya miundombinu ya barabara inayowakabili
wananchi wa wilaya za Ruangwa na Nachingwea kwa muda mrefu.
Waziri Mkuu, Majaliwa amesema
barabara hiyo ambayo kwa sasa haipo katika hali nzuri itajengwa kwa
kiwango cha lami, ambapo serikali inatarajia kuanza kuifanyia upembuzi
yakinifu katika mwaka wa fedha wa 2016/2017.
Hayo yamesemwa jana jioni (10
Aprili, 2016) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipozungumza kwa nyakati
tofauti na wananchi wa vijiji vya Likunja, Nkowe na Namahema katika
mikutano ya hadhara aliyoifanya wilayani Ruangwa wakati akiwa kwenye
ziara yake ya kikazi.
Amesema serikali imejipanga
katika kuboresha miundombinu ya barabara kwenye maeneo mbalimbali nchini
na kwamba mara baada ya kumalizika kwa upembuzi yakinifu ujenzi wa
barabara hiyo utaanza, hivyo amewataka wananchi kuwa na subira.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu, Majaliwa amewataka wananchi wa vijiji hivyo kushirikiana katika
shughuli za maendeleo na kuweka kando itikadi zao za kisiasa kwa sababu
uchaguzi ulishamalizika tangu Oktoba 25 mwaka jana.
“Mimi nitaendelea kuwaheshimu,
kuwasikiliza na kuwahudumia, nawaomba tushirikiane na tuweke kando
masuala ya itikadi za vyama, sasa ni wakati wa kazi, hivyo ni bora
tukashirikiana kufanya kazi kwa maendeleo ya Ruangwa jambo ambalo
linawezekana.
Hata kama wewe ambaye najua
ulinichukia mimi nimekusamehe kutoka moyoni, wewe ni wangu hata kama
hukunichagua nitakuhudumia na kukutumikia kwa sababu mimi ndiye mbunge
wako hivyo naomba tushirikiane,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Rashid Nakumbya aliomba wakazi wa
wilaya hiyo kushirikiana kwa pamoja kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya
wilaya yao na hatimaye iweze kupiga hatua.
0 comments:
Post a Comment