Meneja
Uhusiano wa Jamii wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam
(DAWASA) Bi.Neli Msuya akizungumza na viongozi wa Jumuiya 15 za Watumia
Maji zilizojengwa chini ya mradi wa Maji Yetu uliofadhiliwa na Serikali
ya Ubelgiji uliogharimu shilingi Bilioni 14.5 alipokutana nao leo jijini
Dar es salaam.
Mshauri wa Ufundi wa DAWASA –BTC Mhandisi
Praygod Mawalla akitoa elimu kwa viongozi wa Jumuiya 15 za Watumia Maji
katika jiji la Dar es salaam namna ya kuifanya miradi wanayoisimamia
ijiendeshe na kuwa endelevu kwa manufaa ya wananchi.
Mshauri wa Ufundi wa DAWASA –BTC Manjolo
Kambili akitoa akitoa ufafanuzi kuhusu Programu ya za utoaji wa mafunzo
kwa watumiaji wa Maji katika maeneo yenye miradi hiyo wakati wa mkutano
na viongozi wa Jumuiya 15 za Watumia Maji za jiji la Dar es salaam.
Viongozi
wa Jumuiya 15 za Watumia Maji zilizojengwa chini ya mradi wa Maji Yetu
wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa na watendaji wa
DAWASA leo jijini Dar es salaam.
Afisa Uhusiano na Jamii wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASA) Bi. Mecktridis Mdaku Mtaalamu kutoka akiwasisitiza
viongozi wa Jumuiya 15 za Watumia Maji katika jiji la Dar es salaam
kupanda miti na kuiendesha miradi katika hali ya Usafi ili kulinda afya
za watumiaji wa huduma za maji.
Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa DAWASA Bi. Mary Ntikula akipanda mti mara baada ya mkutano na viongozi wa Jumuiya ya Watumia Maji Dar es salaam kama sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Maji na Utunzaji wa Mazingira. Kulia ni Meneja Uhusiano wa Jamii wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASA) Bi.Neli Msuya
Baadhi
ya watendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam
(DAWASA) wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Jumuiya 15 za
Watumia Maji jijini Dar es salaam.
Na. Aron Msigwa –Dar es salaam.
Mamlaka
ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASA) imewataka viongozi wa
Jumuiya za watumia maji katika jiji la Dar es salaam na baadhi
ya maeneo ya Kibaha na Bagamoyo mkoani Pwani kusimamia kikamilifu
mapato na matumizi ya miradi ya maji ili kuepuka migogoro
inayosababishwa na matumizi mabaya ya fedha jambo linalochangia baadhi
ya miradi kushindwa kujiendesha na kuwa kero kwa wananchi.
Kauli
hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Meneja Uhusiano wa Jamii wa
Mamlaka hiyo Bi.Neli Msuya wakati akitoa elimu kwa viongozi hao kuhusu
uendelezaji wa miradi inayosimamiwa na Jumuiya 15 za Watumia Maji
zilizojengwa chini ya mradi wa Maji Yetu kwa ufadhili wa Serikali ya
Ubelgiji.
Amesema DAWASA
imekukutana viongozi hao kuwakumbusha wajibu walio nao katika
kuhakikisha miradi wanayoisimamia inakidhi matarajio ya wananchi kwa
kutoa huduma bora na kujiendesha kwa faida kwa na kuwafikia wananchi
wengi zaidi.
“Kwa kuzingatia idadi ya watu zaidi ya Laki mbili (200,000) wanaohudumiwa
na mradi huu kwa kupata maji safi na salama na gharama kubwa
iliyotumika kuanzisha mradi huu shilingi Bilioni 14.5 ,tumeona kuna
umuhimu wa kuendelea kuweka msisitizo wa uangalizi kwa kuwa miradi hii
ni muhimu na iko kwa wananchi” Amesisitiza.
Amewaeleza
viongozi hao kuwa majukumu ya DAWASA kama mmiliki wa miundombinu ya
majisafi na majitaka ni kugharamia matengenezo makubwa na kufanya
uwekezaji wa kupanua miundombinu ya majisafi na majitaka jijini Dar es
Salaam na maeneo yaliyoainishwa chini ya Sheria ya DAWASA Namba.20 ya
Mwaka 2001.
Bi.
Neli amefafanua kuwa DAWASA iliingia mkataba wa uendeshaji na Shirika
la Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASCO) kutoa huduma ya
uondoshaji wa majitaka katikA jiji la Dar es salaam, Kibaha na Bagamoyo
mkoani Pwani.
Aidha, amesema kupitia mkataba huo, DAWASCO
huuza maji kwa wateja, kutayarisha Ankara za maji, kukusanya maduhuli,
kulipia gharama za uendeshaji na kufanya matengenezo ya mfumo mzima wa
usambazaji maji na uondoshaji majitaka katika maeneo mbalimbali ya jiji
la Dar es salaam.
“Kupitia
elimu inayotolewa leo mtagundua kuwa ninyi ni muhimu katika kuwahudumia
wananchi, mtaona kuwa ninyi ni DAWASCO ndogondogo kwenye maeneo yenu
kwa kuwa mnauza maji kwa wateja, mnatayarisha Ankara za maji ,
mnakusanya fedha za malipo ya huduma mnafanya matengenezo ya mifumo ya
maji kwa wateja wenu” Amesisitiza.
Amesema
kwa sasa DAWASA imewekeza kwenye miradi mikubwa na kupanua chanzo cha
Maji cha Ruvu chini ambacho huzalisha lita milioni 270 kwa siku, ujenzi
wa Bomba kubwa lenye urefu wa Kilometa 56 kutoka Ruvu Chini hadi matenki
yaliyopo chuo Kikuu Ardhi jijini Dar es salaam.
Aidha
amesema kwa upande wa Ruvu juu maboresho makubwa yamefanyika kwa
kupanua mitambo ya uzalishaji ambayo sasa itazalisha lita milioni 196
kutoka milioni 82 kwa siku.
Ameongeza
kuwa upande wa maeneo ya kaskazini na kusini mwa jiji la Dar es salaam
kuelekea wilaya ya Mkuranga DAWASA inaendelea kuwekeza katika uchimbaji
wa visima virefu vya maji na kuweka mifumo ya usambazaji wa maji ili
kuwawezesha wananchi kupata maji safi na salama kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake Mshauri wa Miradi ya Maji kutoka DAWASA –BTC
Bw. Manjolo Kambili amewaeleza viongozi hao kuwa wao kama viongozi wa
Jumuiya za watumia maji wanatakiwa kufuata sheria na taratibu za
Serikali kwa kuwa miradi hiyo ni ya Serikali.
Ameeleza
kuwa jukumu la kusimamia na miradi hiyo liko kisheria hivyo viongozi
hao wanapaswa kutekeleza kikamilifu majukumu yao likiwemo la kuhakikisha
kuwa miradi yote inaajiri wahasibu wenye taaluma kwa lengo la kuandika
na kutunza kumbukumbu za kila siku zinazohusu mapato na matumizi yao.
“Naomba
nisisitize katika hili, nyie mmepewa jukumu la kusimamia miradi ya maji
ya Serikali, lazima mlitambue hili miradi yenu itakaguliwa na wataalamu
ndio maana tuliwaomba muajiri wahasibu kwa kuwa vitabu vyenu
vitakaguliwa kujua mwenendo wa mapato na matumizi yenu” Amesisitiza.
Amewataka
viongozi hao kuhakikisha kuwa kila mradi wa jumuiya unakuwa na akaunti
ya Benki pamoja na kusimamia suala la utoaji wa risiti halali zenye
nembo za jumuiya husika ili kuweka uwazi na imani wa walipiaji Ankara za
maji.
Naye
Afisa Uhusiano na Jamii wa Mamlaka hiyo Bi. Mecktridis Mdaku
amewasisitiza viongozi hao kusimamia suala la Usafi wa mazingira,
upandaji wa miti na utunzaji wa vituo vya miradi, majengo na miundombinu ya maji ili kuwakinga wananchi dhidi ya magonjwa ya milipuko ikiwemo.
“Ninyi
kama viongozi wa Kamati za miradi ya maji lazima msimamie suala la
usafi wa mazingira ili maeneo ya miradi yavutie pia kuwakinga wateja
wenu na ugonjwa wa kipindupindu” Amesisitiza Bi. Mdaku.Ametoa wito kwa viongozi hao kuepuka kuyatumia majengo ya miradi ya maji ya wananchi kwa shughuli nyingine nje ya maji ikiwemo kuhifadhi na kufanyia biashara ya mkaa.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment