Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
---
Na Ibrahim Bakari na Hussein Issa,Mwananchi
Dar es Salaam.
Serikali inapitia upya ulinzi wa
viongozi wastaafu ili kuepuka fedheha iliyotokana na vurugu
alizofanyiwa Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba hivi karibuni.
Mpango huo umeelezwa na Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Sefue mwishoni mwa wiki, akisema Serikali imekerwa na
kufedheheshwa kutokana na tukio hilo lililotokea wakati wa mdahalo wa
Katiba Inayopendekezwa katika Hoteli ya Blue Pearl, Dar es Salaam
Novemba 2, mwaka huu.
“Kimsingi tutakachokifanya ni kupitia upya mpango
wa ulinzi wa viongozi wote waliostaafu, japokuwa huwa tunafanya hivyo
mara kwa mara, lakini kwa hili la Mzee Warioba tunaliangalia kwa umakini
wake.
“Tumekerwa sana na tukio lile, halikutufurahisha
hata kidogo kama Serikali kwa kuwa limemvunjia heshima Mzee Warioba,
yule ni mzee wetu, anahitaji heshima, kwanza heshima yake na ulinzi.”
Kauli hiyo ya Sefue imekuja wakati mdahalo huo
uliovunjika baada ya Mzee Warioba kushambuliwa, ukiwa umetangazwa
kufanyika upya Jumapili Novemba 16, mwaka huu katika hoteli hiyohiyo.
Mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Humphrey Polepole alithibitisha jana kuandaliwa kwa mdahalo huo kuanzia
saa 9.00 alasiri siku hiyo.
Tukio la kufanyiwa vurugu Jaji Warioba lililaaniwa
na wananchi, wasomi, wanasiasa na wanaharakati mbalimbali wakisema
kuwashambulia viongozi na hasa katika mjadala wa Katiba ni kukosa
uvumilivu na ni kuashiria machafuko katika siku za usoni.
Balozi Sefue aliongeza: “Najua si jambo zuri,
iliwahi kutokea pia kwa Mzee (Ali Hassan) Mwinyi, alipigwa kibao... sasa
kingine ni mazingira yanapotokea matukio haya, wakati mwingine ni
ngumu.”
Mzee Mwinyi alipigwa kibao Machi 10, 2009 na mmoja
wa waumini wa dini ya Kiislamu katika Baraza la Maulidi wakati Rais
huyo mstaafu alipokuwa akihutubia.
Kutokana na matukio hayo, Balozi Sefue alisema: “Watanzania tumekuwa na tabia ya kuheshimiana lakini matukio haya yanatokea na kila mmoja hatarajii, kinachotakiwa ni sisi tuwaheshimu wazee wetu hawa.”
Kutokana na matukio hayo, Balozi Sefue alisema: “Watanzania tumekuwa na tabia ya kuheshimiana lakini matukio haya yanatokea na kila mmoja hatarajii, kinachotakiwa ni sisi tuwaheshimu wazee wetu hawa.”
Mdahalo wa wiki iliyopita ulioandaliwa na Taasisi
ya Mwalimu Nyerere, ulivunjika baada ya kutokea vurugu wakati Jaji
Warioba alipokuwa akihoji vitendo vya baadhi ya watu kutumia vibaya jina
la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Jaji Warioba alikuwa akihitimisha hotuba yake
akichambua hoja zilizomo katika Katiba Inayopendekezwa akilinganisha na
zile zilizoachwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba iliyoandaliwa na Tume
ya Mabadiliko ya Katiba aliyoiongoza.
Kwa Habari Zaidi
0 comments:
Post a Comment