SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Sunday, July 27, 2014

Mama Kikwete ahimiza wanafunzi wa kike wa vyuo vya ualimu kuvaa mavazi ya heshima

Na Anna Nkinda - Maelezo,  Nachingwea

Wanafunzi wa kike wa vyuo vya ualimu nchini wametakiwa kuvaa mavazi  nadhifu  yanayoendana na maadili ya kazi yao  ili wanafunzi na jamii inayowazunguka ijifunze  kutoka kwao kwani wao ni kioo cha jamii.

Mwito huo umetolewa  hivi karibuni  na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na baadhi ya wanafunzi wa kike  wa chuo cha Ualimu Nachingwea mara  baada ya kumalizika kwa futari aliyoiandaa kwa ajili ya viongozi wa wilaya iliyofanyika  chuoni hapo. 


Mama Kikwete ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa kupitia wilaya ya Lindi mjini alisema siyo jambo jema kwa mwalimu kuvaa mavazi yanayoonyesha sehemu za miili yao ikiwemo kata mikono, nguo zinazobana na sketi fupi  kwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na haiba ya ualimu. 

Alisema, “Sikuhizi kuna baadhi ya watu  wanavaa mavazi yasiyoendana  na utamaduni wa mtanzania,  nyinyi kama walimu ambao ni kioo cha jamii na mnawafundisha  wanafunzi madarasani msifanye hivyo  kwa kufanya hivyo watoto  wataiga na kufikiria  kuwa kuvaa mavazi hayo ni sawa”.

Mama Kikwete pia  aliwataka wanafunzi hao kutokuchagua  maeneo ya kwenda kufanya kazi pindi wamalizapo masomo yao na kupangiwa vituo vipya vya kazi kwani kazi ya ualimu ni wito na kama mtu  hakuipenda kazi hiyo basi angechagua fani nyingine za kusoma.

“Baadhi ya walimu wamekuwa wakikataa kwenda kufanya kazi katika maeneo ya vijijini, na wengine wakipangiwa vituo vya mbali na mjini wanaogopa na kudiriki hata kuacha kazi,  kama ni hivyo kwa nini ulipoteza fedha  na muda wako kusomea ualimu?” , aliuliza Mama Kikwete.

MNEC huyo alimalizia kwa kuwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kujiepusha na mahusiano ya kimapenzi wawapo masomoni kitendo ambacho kitawasaidia  kumaliza masomo yao salama na kurudi nyumbani bila ya kufukuzwa chuo kwa ajili ya kupata ujauzito.

Mama Kikwete ambaye kitaaluma ni mwalimu miaka ya nyuma alisoma chuo cha ualimu Nachingwea na juzi akiwa chuoni hapo alitembelea Bweni la wasichana la Kawawa  ambalo ndilo alilokuwa analala wakati akiwa mwanafunzi wa chuo hicho.

0 comments:

Post a Comment