SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Saturday, July 5, 2014

Cheka mbaroni, amtwanga mtu baa


9
Bingwa wa ngumi za kulipwa duniani, Francis Cheka ‘SMG’ akiwa  amebebwa na mashabiki wake.(Picha na Maktaba).


Na Mwandishi wetu
Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamshikilia bingwa wa ngumi za kulipwa duniani, Francis Cheka ‘SMG’ kwa tuhuma za kumchapa Meneja wa baa ya Vijana Social Hall iliyopo Kata ya Sabasaba, Manispaa ya Morogoro.
Kwa mujibu wa maelezo ya meneja huyo, Bahati Kabanda ‘Masika’ (39), Cheka alifika katika baa hiyo majira ya jioni na kuanza kumtukana na kumshambulia kwa maneno machafu kisha kumvamia na kuanza kumchapa ngumi na mateke sehemu za tumboni.
Kwamba ni tukio la Juni 2, mwaka huu katika baa hiyo inayomilikiwa na promota wa ngumi za kulipwa mkoani Morogoro, Zumo Makame.
Kabanda amedai wakati akipewa kichapo na Cheka, hakuna mtu aliyesogea kuamulia ugomvi huo kutokana na watu kumuogopa bondia huyo aliyewahi kuwapiga mabondia wa ndani na nje ya nchi.
Alidai Cheka alifika katika baa hiyo na dalili za kulewa pombe na baada ya kuondoka, wasamaria wema walimchukua yeye hadi katika hospitali ya rufaa ambako alilazwa na kupatiwa vipimo na matibabu ya maumivu aliyoyapata.
Kabanda alidai kuwa hakuwa na ugomvi na bondia huyo, na hivyo hajui chanzo cha kupigwa na kuongeza kuwa kama alikuwa na ugomvi nae angemfikisha kwenye vyombo vya sheria na sio kujichukulia sheria mkononi.
Masika alidai kuwa pamoja na kupatiwa matibabu, lakini bado hali yake kiafya sio nzuri kutokana na maumivu aliyoyapata ya mbavu, hivyo kumfanya ashindwe kutembea vizuri.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa walimuona Cheka akimuangushia kipigo meneja huyo, lakini walishindwa kuamulia ugomvi huo kutokana na kumwogopa Cheka ambaye ni bingwa wa ngumi duniani.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, Ritha Lyamuya, alikiri kumpokea Masika hospitalini hapo Juni 2, akiwa na maumivu ya mbavu na walipompima X-ray ilionekana amepata maumivu, hivyo walimpatia matibabu na kumruhusu kurudi nyumbani.
Alisema hadi anaruhusiwa hospitalini hapo, Masika alikuwa anaendelea vizuri.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Leonard Paulo, amekiri Cheka kufanya shambulio hilo kwa meneja huyo kwa kumpiga sehemu za tumboni na kichwani.
Paulo alisema Cheka amekamatwa na anashikiliwa na polisi kwa mahojiano na kwamba katika maelezo yake, anadai kuwa yeye na Masika walikodi baa hiyo na kufanya biashara kwa pamoja, lakini baadaye walianza kukosana katika suala na mapato.
Cheka aliendelea kudai kuwa siku ya tukio alifika katika baa hiyo kwa lengo la kutaka kujua namna mauzo yanavyokwenda, lakini meneja huyo alimzuia kuingia kaunta na ndipo ilitokea kutoelewana na baadae ugomvi huo kutokea.
Kamanda Paulo alisema pamoja na maelezo hayo ya Cheka, lakini ameiagiza timu ya askari kuchunguza kwa kina tukio hilo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

0 comments:

Post a Comment